Sh19 milioni kukarabati handaki Kongwa

Muktasari:
- Ili kuendeleza thamani na kutunza historia ya ukombozi wa bara la Afrika, Serikali imetoa Sh19 milioni kukarabati handaki lililotumika na wapigania uhuru katika kipindi cha ukombozi wa nchi za Afrika lililopo Wilayani Kongwa.
Dodoma. Katika mwaka wa fedha 2023/24 Wilaya ya Kongwa inatarajia kutumia Sh19 milioni kwa ajili ya ukarabati wa handaki lililotumika kwenye harakati za ukombozi wa Bara la Afrika ili kuendelea kuhifadhi utamaduni na utalii wa eneo hilo.
Hata hivyo, ukarabati huo umetajwa kuwa ni mwanzo wa ukarabati wa maeneo mengi ya kihistoria yanayopatikana katika wilaya hiyo yakiwemo maeneo ya makaburi na barabara za kuelekea kwenye maeneo hayo ya utalii.
Hayo yameelezwa leo Novemba 16, 2023 na Mkuu wa wilaya hiyo, Remidius Mwema wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea mchezo wa mbio zenye lengo la kutangaza utalii kupitia vivutio vilivyotumika kwenye harakati za ukombozi wa bara la Afrika.
“Dhamira ya Serikali kwenye ukarabati wa maeneo hayo ni kuwepo muda wote lakini tumekuwa tukifanya utaratibu huo kwa awamu na kwa mwaka wa fedha 2023/24 tutaanza na handaki na baadae maeneo mengine yatafuata,”amesema.
Hata hivyo Mwema amesema zipo nchi za Afrika ambazo zimeonesha utayari wa kusaidia ukarabati wa eneo hilo ikiwemo nchi ya Namibia.
Akizungumzia kuhusu mbio za Kongwa African Liberation Marathon zitakazofanyika Novemba 25, 2023, Mwema amesema sehemu ya fedha zitakazopatikana kwenye mchezo huo zitakarabati maeneo mengi ya kihistoria kwenye wilaya hiyo na kuchangia kwenye sekta ya elimu.
Mwema amesema baadhi ya nchi zenye historia na eneo hilo kama Zimbbwe, Namibia, Msumbiji, Angola na Afrika Kusini zimetumiwa mwaliko wa mchezo huo utakaohusisha viongozi wa Serikali akiwemo Waziri wa Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Damas Ndumbaro na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Mjumbe wa Kamati ya uratibu wa mbio hizo Kelvin Msumule amesema mshindi wa jumla atazawadiwa Sh1 milioni na mbio hizo zitahusisha umbali wa kilomita 5, 10 na 21.