Sh203 bilioni kujenga mradi wa maji Iringa

Muktasari:
- Wakati huduma ya maji safi ikifikia asilimia 98 katika Manispaa ya Iringa, zaidi ya Sh203 bilioni zinatarajia kutumika kwa ajili ya ujenzi wa mradi mkubwa wa maji safi na maji taka katika mji wa Iringa, Ilula na Kilolo.
Iringa. Zaidi ya Sh203 bilioni zinatarajia kutumika kwa ajili ya mradi wa maji safi na maji taka ambao utainufaisha Manispaa ya Iringa, Mji wa Kilolo na Ilula.
Mradi huo unakuja wakati tayari huduma ya maji safi kwa wakazi wa Manispaa ya Iringa ikiwa imefikia asilimia 98 huku changamoto ikiwa kwenye mtandao wa maji taka.
Akizungumza na Mwananchi ofisini kwake leo, Agosti 30, 2023, Afisa Uhusiano wa Mamlaka ya Maji safi na Usafi wa Mazingira Iringa (Iruwasa), Restuta Sakila amesema kwa upande wa maji safi, mradi huo utajengwa kwenye chanzo kipya cha maji ya Mtitu wilayani Kilolo.
“Mpaka sasa huduma ya maji Iringa imefikia asilimia 98, ujio wa mradi huu utasaidia maji kufikia asilimia 100,” amesema.
Hata hivyo amesema Iruwasa imefanikiwa kutoa huduma ya maji kwa maeneo ya nje ya mji, ikiwemo kata za Kising’a, Kihorogota, Isimani, Ndolela, Kalenga, Kiwele na Luhota ambako kulikuwa na shida ya maji.
Amesema fedha hizo zitafanikisha ujenzi wa kidaka maji, mtambo wa kusukuma maji, tenki kubwa na ulazaji wa bomba za maji kilometa 25.
Kwa upande wa maji taka, Sakila amesema wameelekeza kwenye ujenzi wa mabwawa mapya ya maji taka na kuhamisha bwawa la sasa la Donbosco ambalo limesogelewa na makazi ya watu.
‘Kata ambazo hazikuwa kwenye mtandao wa maji taka zitanufaika na mradi huu. Kata hizo ni Kihesa, Gangilonga, Mtwivila, Nduli, Mwangata na baadhi ya maeneo ya ngelengele, Mkwawa,” amezitaja.
Amesema mabwawa hayo yatajengwa katika Kijiji cha Kidete na Kipululu – Kigonzile.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa wamesema huduma ya maji safi ni nzuri isipokuwa tatizo kubwa lipo kwenye bili.
‘Bili ya maji ni kubwa, ni Imani yetu mradi huu utashusha gharama za maji, vinginevyo sijawahi kushuhudia maji yakikatika kwa zaidi ya miaka kumi, tangu nihamie Iringa,” amesema Meshaki Ndenda, mkazi wa Kihesa, Manispaa ya Iringa.