Sh24.4 bilioni kusaidia vijana kuacha dawa za kulevya

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge Sera na Uratibu ,Jenesta Mhagama akizungumza katika matembezi hayo jijini Arusha  leo

Arusha. Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Bunge, Sera na Uratibu Jenista Mhagama amesema Serikali ametenga Sh24.4 bilioni kuwasaidia vijana waliotumia madawa ya kulevya.

Ameyasema hayo leo Juni 24, 2023 jjjini Arusha katika matembezi ya kupinga matumizi ya dawa za kulevya yanayoenda sambamba na maadhimisho ya kitaifa ya kupinga vita dawa za kulevya duniani.

Amesema, pamoja na biashara ya dawa za kulevya lengo kubwa ni kuhakikisha vijana wanakuwa salama na kuokolewa kutoka kwenye uraibu wa matumizi wa dawa za kulevya.

Aidha Mhagama amesema asilimia kubwa ya vijana ndiyo nguvu kazi ya Taifa katika kuleta maendeleo ndio maana serikali imeamua kuwekeza nguvu kubwa katika kuwasaidia vijana kuweza kujikwamua katika changamoto hiyo.

"Serikali inatumia gharama kubwa kutibu watumiaji wa dawa za kulevya na tayari mikakati ya kujenga kituo kikubwa cha kuwahudumia inaendelea," amesema.

Kwa upande wake Kamishna Jenerali Aretas Lyimo kutoka Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya(DCEA) amesema mpaka sasa wananchi 16 wamechukuliwa hatua kwa kujihusisha na ulimaji wa zao la bangi mkoani Arusha.

Lyimo amesema elimu zaidi inaendelea kutolewa kwa wananchi katika kutambua madhara ya matumizi ya madawa hayo kwani yamekuwa yakiathiri afya za binadamu.

"Tumekuwa tukitoka elimu kwa wananchi juu ya madhara ya dawa za kulevya kwani zimekuwa zikileta  athari kubwa kwenye ubongo  wa binadamu na tunataka  kuhakikisha  zao hilo linaisha  kabisa kwa jiji la Arusha na kwa watakaokaidi  watachukuliwa hatua kali za kisheria "amesema .

Aidha  ametoa wito kwa vijana waliotoka kwenye uraibu wa matumizi  ya  madawa ya kulevya na kuacha biashara ya madawa wana haki ya kuomba fedha katika mfuko wa halmashauri ili waweze kujiajiri pamoja na kuitaka jamii kuacha kuwanyanyapaa  vijana  wanaotumia madawa ya kulevya.

Kwa upande wa vijana waliotumia madawa ya kulevya wameiomba serikali pamoja na wadau kuweza kuboreshewa huduma kwa watumiaji wa madawa ya kulevya huku wakisema wamekuwa waelimisha Rika kwa jamii na kuwa mabalozi kwa jamii.