Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh296 milioni kupunguza kero ya maji Rombo

Chanzo cha maji cha mto Ungwasi, kilichopo kata Mrao Keryo, Wilaya ya Rombo.

Muktasari:

  • Mradi huo unatarajiwa kuzalisha lita 1,296,000 za maji kwa siku na hivyo kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wa vijiji vya Mrao, Momwe na Kiraeni kata ya Mrao Keryo, Wilaya ya Rombo.

Rombo. Mamia ya wananchi wa vijiji vya Mrao, Momwe na Kiraeni katika Kata ya Mrao Keryo, Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, wataondokana na changamoto ya muda mrefu ya upatikanaji wa maji safi na salama baada ya Serikali kukamilisha mradi wa chanzo cha maji kutoka Mto Ungwasi.

Mradi huo uliogharimu zaidi ya Sh296 milioni, unatarajiwa kuzalisha takribani lita 1,296,000 za maji kwa siku, hatua inayolenga kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto ya maji ambayo imekuwa ikiwakabili wananchi wa eneo hilo kwa zaidi ya miaka 20.

Akizungumza kuhusu mradi huo leo Jumatatu, Juni 15, 2026 baada ya kuukagua, Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Rombo (Rombowasa), Tumaini Marandu amesema kukamilika kwa mradi huo ni hatua muhimu katika kuboresha huduma ya maji wilayani humo.

“Mradi wa maji wa Mto Ungwasi ulianza kutekelezwa mwaka 2025 na ulikamilika Januari mwaka huu kwa gharama ya zaidi ya Sh296 milioni,” amesema Marandu.

Amesema mradi huo utanufaisha jumla ya wananchi 3,907 wa vijiji vya Mrao, Momwe na Kiraeni, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakikabiliwa na uhaba wa maji safi na salama.

Marandu ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, mamlaka hiyo inatarajia kutekeleza miradi mitatu ya maji yenye thamani ya Sh11.5 bilioni ili kuimarisha zaidi upatikanaji wa huduma hiyo wilayani Rombo.

Amesema miradi hiyo itaongeza uzalishaji wa maji kwa lita 10,065,000 kwa siku kutoka vyanzo vya Ziwa Challa, Nfuweni, Kitasha na Kitendekimu, sambamba na kupanua mtandao wa mabomba kwa kilomita 22.8.

Aidha, itahusisha ukarabati wa kilomita 76.91 za miundombinu chakavu ya mabomba pamoja na ujenzi wa matanki matatu yenye uwezo wa kuhifadhi lita 2,300,000 za maji.

Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Mrao Keryo, Gody Mrosso amesema wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa zaidi ya miaka 20, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli zao za kila siku.

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Maji ya Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira Rombo (ROMBOWASS) wakikagua chanzo cha maji cha mto Ungwasi, kilichopo kata ya Mrao Keryo, Wilaya ya Rombo, Mkoani Kilimanjaro.Picha na Janeth Joseph

Amesema kukamilika kwa mradi huo kutachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha maisha ya wananchi pamoja na kuimarisha shughuli za kijamii na kiuchumi zinazotegemea maji.

Akizungumzia miradi ya maji wilayani humo, Mbunge wa Rombo, Profesa Adolf Mkenda amesema Serikali imepiga hatua kubwa katika kutatua changamoto ya maji kupitia miradi mbalimbali inayoendelea kutekelezwa.

“Chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan kumekuwa na jitihada kubwa za kutatua changamoto ya maji. Kwa kiasi kikubwa tumepunguza tatizo hilo na tunaendelea kuboresha huduma,” amesema Profesa Mkenda.

Ameongeza kuwa endapo kasi ya utekelezaji wa miradi itaendelea, Wilaya ya Rombo inaweza kufikia kiwango cha kujitosheleza kwa huduma ya maji ifikapo mwaka 2031.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wameeleza furaha yao kutokana na kukamilika kwa mradi huo, wakisema utapunguza adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji.

Rehema Moshi, mkazi wa Kijiji cha Mrao amesema awali walilazimika kutumia muda mwingi kutafuta maji, hasa nyakati za kiangazi, hali iliyokuwa ikiathiri shughuli za uzalishaji.

“Tulikuwa tunatumia saa kadhaa kutafuta maji. Sasa tunategemea maisha yatakuwa rahisi zaidi kwa kuwa huduma ya maji imekaribia,” amesema.

Naye mkazi wa Kijiji cha Momwe, Joseph Kileo amesema upatikanaji wa maji safi na salama utasaidia kuboresha afya za wananchi na kupunguza magonjwa yanayotokana na matumizi ya maji yasiyo salama.