Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh345.45 bilioni kuneemesha wakulima wadogo

Muktasari:

  • Wakulima wa mahindi, ngano, mpunga na alizeti  wanatarajiwa kunufaika baada ya Japan kuipatia Tanzania mkopo nafuu wa Sh345.45 bilioni.

Dar es Salaam. Tanzania inatarajiwa kupata mkopo nafuu wa Sh354.45 bilioni kutoka Serikali ya Japan kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa uendelezaji kilimo vijijini.

Mkopo huo utawanufaisha wakulima wadogo hususan wa mpunga, mahindi, ngano na alizeti.

Mradi huo utatekelezwa chini ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB), ukisimamiwa kwa karibu na Shirika la Maendeleo la Japan (Jica) kwa niaba ya Serikali ya Japan.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba wa mkopo kati ya Wizara ya Fedha na Jica, Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba amesema utekelezaji wa mradi huo utachochea ukuaji wa sekta ya kilimo kwa kuongeza uzalishaji kwa wakulima kupitia upatikanaji wa mitaji nafuu.

Amesema mikopo ya muda wa kati na mrefu kwa itatolewa kwa wakulima, vikundi vya uzalishaji na taasisi zinazojihusisha na kilimo kwa kuziwezesha kuwekeza katika kilimo cha kisasa, kupata pembejeo bora na teknolojia ya juu ya kilimo.

“Upatikanaji wa mitaji ya kilimo utawezesha pia wakulima kuwa na mazao mchanganyiko na kuwa na kilimo kinachostahimili mabadiliko ya tabia nchi, ambako kutachangia usalama wa chakula, maendeleo vijijini na uimara wa uchumi kwa ujumla,” amesema.

Amesema utekelezwaji wa mradi huu unaendana na Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ambao una maudhui ya kufikia ushindani na uchumi wa viwanda kwa maendeleo ya watu ili kuongeza tija na uzalishaji kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Mradi huo unaendana na Mpango wa Pili wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ambao unalenga kuimarisha na kuchochea matumizi ya zana za kisasa za kilimo, usalama wa chakula na lishe, kuwezesha upatikanaji wa masoko na kuwezesha uongezaji wa thamani.

“Hivyo, unaweza kuona jinsi ufadhili huu ulivyo wa muhimu. Napenda kuwahakikishia kwamba Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itachukua hatua zote muhimu kuhakikisha mradi huu unatekelezwa kwa ufanisi ili kufikia malengo yaliyokusudiwa,” amesema.

Amesema Tanzania inatambua na kushukuru kwa ufadhili ambao umekuwa ukitolewa na Serikali ya Japan ambao hutekelezwa na Jica.

“Uhusiano huu wa muda mrefu umechangia kwa kiasi kikubwa kuchochea ukuaji endelevu wa uchumi na kuboresha maisha ya Watanzania. Utayari wa Serikali ya Japan kuchochea ukuaji wa uchumi na kuendelea kuimarisha ushirikiano ni wa kupigiwa mfano. Serikali ya Tanzania itaendeleza ushirikiano huu kwa ajili ya kufikia malengo yetu ya pamoja,” amesema.

Mkurugenzi Mtendaji wa TADB, Frank Nyabundege amesema upatikanaji wa fedha hizo ni mwendeleo wa yale yanayofanyika katika kilimo.

Amesema tangu Serikali ya awamu ya sita iingie madarakani zaidi ya Sh954 bilioni zimeelekezwa TADB ili kuhakikisha Watanzania wengi wananufaika na kilimo kwa kuwatoa katika kilimo cha kujikimu kwenda cha biashara.

“Serikali imekuwa ikisaidia sekta ya kilimo ili iweze kufanya vizuri na wenzetu wanasema ukitaka kutajirika nenda katika kilimo,” amesema.

Amesema fedha hizo zitatolewa kwa riba ndogo kuwezesha wakulima wadogo kumudu kuzichukua ili walime kwa tija na kujiinua kiuchumi.

“Uwekaji wa fedha nyingi unalenga kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo nchini inakuwa na tija kwa Watanzania kwani asilimia 65 wako huko, hivyo tunaona kuna umuhimu gani wa kuibeba sekta ya kilimo ili maisha ya Watanzania yaimarike,” amesema.

Makamu wa Rais wa Jica, Katsura Miyazaki, amesema  mradi unalenga kuchangia kuboresha tija ya kilimo na kuongeza mapato ya wakulima na kuongeza thamani katika mnyororo wa mazao manne yaliyopewa kipaumbele.

“Mazao manne yaliyopewa kipaumbele ni mpunga, mahindi, ngano na alizeti yaliyoorodheshwa katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa Serikali ya Tanzania  (FYDP III) na itaimarisha mnyororo wa thamani na usalama wa chakula,” amesema.

Amesema fedha hizo pia zitagharimia sekta ya kilimo cha bustani na kutengeneza fursa za ajira kwa wanawake na vijana.