Sh5 milioni za Rais Samia zaibua mzozo kwenye familia

Muktasari:

  • Bryan alifariki Aprili 12, 2024 mkoani Arusha, wakati akijaribu kuokoa wanafunzi wa Ghati Memorial wasife baada ya gari la shule walilokuwemo aina ya Toyota Hiace kutumbukia kwenye Korongo Mbaash lililojaa maji, lakini hata hivyo alizidiwa na maji na kufariki dunia. Katika tukio hilo wanafunzi wanane pia walifariki dunia baada ya kusombwa na maji.

Arusha. Serikali imezuia fedha za mkono wa pole (rambirambi) Sh5 milioni zilizotolewa na Rais Samia Suluhu kwa familia ya marehemu Bryan Nguyaine (34) aliyefariki wakati akiwaokoa wanafunzi, hadi watakapokubaliana anayestahili kukabidhiwa fedha hizo.

Bryan alifariki Aprili 12, 2024 mkoani Arusha wakati akijaribu kuwaokoa wanafunzi wa shule ya msingi Ghati Memorial baada ya gari la shule walilokuwemo aina ya Toyota Hiace kutumbukia kwenye korongo lililojaa maji, hata hivyo alizidiwa na maji hayo na kufariki dunia.

Katika tukio hilo wanafunzi wanane wa shule hiyo walifariki dunia baada ya kusombwa na maji.

 Kutokana na moyo wake wa kujitoa na ujasiri wake, Rais Samia Suluhu alitoa mkono wa pole kwa familia yake, lakini kabla ya kukabidhiwa fedha hizo, kukatokea mvutano mkali wa nani anayestahili kupewa fedha hizo, kati ya mke wa marehemu au ndugu zake waliozaliwa naye.

Akizungumza na Mwananchi leo Aprili 19, 2024, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Felician Mtahengerwa ameeleza kusikitishwa na mvutano wa familia hiyo na hivyo Serikali imeamua kusitisha uhamisho wa fedha hizo, hadi familia watakapokubaliana nani anayestahili kupewa kati ya mwanamke aliyekuwa akiishi na marehemu au ndugu zake wa kuzaliwa.

Mtahengerwa amesema siku ya msiba walitoa Sh1 milioni pekee kwa familia zote zilizofiwa na kugharamia mazishi ikiwemo kununua majeneza na wanaotaka kusafirisha, walisaidiwa huku wakiitaka familia ya Bryan kufungua akaunti kwa ajili ya kufanyiwa uhamisho wa rambirambi maalumu iliyotolewa na Rais.

“Rais alitoa Sh1 milioni kwa familia ya Bryan baada ya kuguswa na moyo wa msamaria huyu ambaye amekufa kishujaa akijaribu kuokoa maisha ya wale watoto, bahati mbaya naye akafariki,” amesema Mtahengerwa.

Amesisitiza kwamba wameipa muda familia wakakubaliane ili waamue anayestahili kupewa fedha, kama hawatafikia uamuzi huo, basi watamwita mama mzazi wa marehemu ili afanye uamuzi wa mwisho.

“Siku ile (ya kuaga miili) hatukukabidhi, bali tulitaka familia ifungue akaunti ya kuingiziwa fedha hizo, lakini kabla hatujafanya hivyo, siku ya msiba tu tukasikia mwanamke anayedai ni mke wa marehemu akilalamika anataka kudhulumiwa na ndugu wanaodai hawamtambui tena, wamemfukuza msibani.

“Kwa sababu fedha hizi tuliambiwa tumpe mke wa marehemu na ndugu wanasema marehemu hakuwa na mke, tumeamua kusitisha kwanza hadi wakubaliane, lakini ikishindikana tutamwita mama mzazi wa marehemu aje aseme nani hasa apewe, na neno lake ndio itakuwa uamuzi wa Serikali,” amesema mkuu huyo wa wilaya.

Alichokisema mke wa Bryan

Akizungumza na waandishi wa habari, Aprili 14, 2024, mwanamke anayedai kuwa mke wa marehemu, Lucy George alisema ameishi na marehemu zaidi ya mwaka mmoja sasa na kushirikiana na ndugu wa mume wake vizuri kabla ya kukutwa na mauti, lakini anashangaa ndugu hao hawamtambui tena baada ya Serikali kutangaza kutoa Sh5 milioni kwake.

“Hata siku alipokufa, wifi yangu mkubwa alinipigia simu kunijulisha juu ya kifo cha Bryan na tukakubaliana kwa sababu nyumba yangu ndogo, basi msiba uwekwe katika nyumba ya wazazi iliyoko kwa Mrombo na baada ya hapo tulilia na kuomboleza pamoja,” alisema Lucy na kuongeza:

“Nashangaa siku ya kuaga miili kwa pamoja na Serikali kutoa ile Sh5 milioni ya kusaidia msiba iliyopokelewa na mjomba wa marehemu na kuahidiwa ije kwangu, wakaanza kusemezana hiyo siyo sawa na hapohapo wakaniacha uwanjani bila kupanda tena gari la familia kurudi nyumbani pamoja na ndugu.”

Alisema aliamua kurudi mwenyewe nyumbani kusubiri siku ya pili yake kwa ajili ya kuzika lakini ndugu walianza kumtenga hadi sare ya msiba hawakumpa,  wala ushirikiano wowote na hata kwenye kuweka shada la maua walilitoa jina lake.

“Niliuliza kwa nini kwenye shada siko kama mke wa marehemu wakati nilikuwa naishi naye, wifi akaniambia wakifanya hivyo mchungaji atagoma kumsomea sala ya kumzika kwani itaonekana alikuwa anazini kwa sababu hajafunga ndoa,” alisema Joyce.

Alisema aliamua kuweka shada kama moja ya marafiki wa marehemu lakini mara baada ya kumalizika msiba, ndugu walimfukuza nyumbani hapo kwa madai hana chake tena.

“Walinifukuza wakidai sina changu tena, licha ya kuwaambia nina ujauzito wa ndugu yao waniache nipumzike lakini wakanifukuza, hivyo naomba Serikali wasikubali kutoa hela ile ya rambirambi hadi ijulikane nani hasa anastahili kupewa” alisema Joyce.

Alipoulizwa kuhusu madai hayo, mjomba wa marehemu, Isaya Nguanei amesema hajui chochote kuhusu madai hayo, hivyo akampa simu mwanamke mmoja aliyedai yeye ni dada wa marehemu, aliyezungumza kwa sharti la kutotaja jina lake, ambaye amesema kaka yao hakuwa na mke wala mtoto, hivyo dada huyo anaedai ni mke wa marehemu athibitishe.

“Mdogo wangu hajawahi kuoa na hata chumba alichokuwa anaishi eneo la Engosengiu, alikuwa akikwama ananipigia na namlipia mimi kodi ya nyumba, na hajawahi kusema ana mke na huyo mwanamke hajawahi kuja kwetu kusema anaishi na Bryan. Kama kweli yupo, aje athibitishe kwetu, sio kwenu waandishi wa habari,” amesema mwanamke huyo anayedai ni dada wa marehemu.