Wasimamizi wa mirathi kuwekewa kibano

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Eliezer Feleshi bungeni jijini Dodoma. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Dodoma. Serikali imewasilisha bungeni mapendekezo ya kuwabana wasimamizi wa mirathi kwa kuwataka kuwasilisha mahakamani hesabu na orodha ya mali za marehemu, pale wanapoondolewa kwenye jukumu la usimamizi.

Hayo yamo kwenye muswada wa marekebisho ya sheria, ambao umesomwa juzi bungeni kwa mara ya kwanza.

Muswada huo ulioandaliwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Pindi Chana na kutolewa kwa waandishi wa habari, kama utapitishwa na Bunge, utakuwa kitanzi kwa wasimamizi wa mirathi wenye tabia ya kudhulumu mali za familia za marehemu.

Mbali na mapendekeo hayo, pia Serikali imependekeza wenza wa Katibu Mkuu Kiongozi na Spika wapate mafao na Jaji Mkuu mstaafu abadilishiwe gari kila baada ya miaka saba.

Pia, muswada unapendekeza adhabu kwa mawakili ‘vishoka’ kuongeza sifa na muda wa uongozi wa viongozi wa Chama cha Wanasheria wa Tanganyika (TLS).


Wasimamizi wa mirathi

Muswada huo unapendekeza marekebisho sehemu ya XXI ya Sheria ya Mirathi na Wosia sura ya 352 kifungu cha 49 kwa kuongeza maneno yanayosomeka;

“Wasimamizi wa mirathi watakapoondolewa au kusimamishwa jukumu hilo na Mahakama, wanatakiwa ndani ya mwezi mmoja tangu tarehe waliyoondolewa au kusimamishwa, wawasilishe mahakamani hesabu au orodha au akaunti ya mali waliyokuwa wakiisimamia.”

Kwa mujibu wa muswada huo, kifungu cha 49 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka masharti kwa wasimamizi wa mirathi kuwasilisha mahakamani taarifa za mali za urithi pale wasimamizi hao wanapotenguliwa au kusimamishwa kuwa wasimamizi wa mirathi.

Lengo la marekebisho hayo ni kusaidia kulinda mali za urithi pamoja na Mahakama kujua kazi alizotekeleza msimamizi wa mirathi kabla ya usimamizi wake kutenguliwa.


Sifa uongozi Baraza la TLS

Muswada huo sehemu ya 23 unapendekeza kufanya marekebisho katika Sheria ya Chama cha Wanasheria Tanganyika, Sura ya 307 kwa kurekebisha kifungu cha 15 ili kuongeza sifa za wajumbe wa Baraza na muda wa wajumbe wa Baraza la Uongozi wa chama kuwa madarakani.

Kwa mujibu wa muswada huo, lengo la marekebisho hayo ni kuimarisha uongozi na kuweka muda wa kutosha kwa viongozi kutekeleza vipaumbele vya baraza.

Mapendekezo mapya yanaelekeza: “Mwanachama mwandamizi wa chama awe na uzoefu wa kufanya kazi ya uwakili kwa miaka 10 au zaidi au awe na kampuni ya uwakili, ilioajiri wafanyakazi watano au zaidi au amefanya kazi kwenye bodi inayotambulika, mwanachama wa chama cha mawakili vijana.

“Awe jaji mstaafu au hakimu mstaafu ambaye amekuwa mwanachama hai wa TLS, au mtumishi mstaafu ambaye amefanya kazi ya kisheria kwa miaka 10 au zaidi.”

Pia, kifungu kidogo cha tano kimefanyiwa marekebisho, kwa kuondolewa ukomo wa uongozi wa mwaka mmoja na kupendekeza miaka mitatu.

Muswada unapendekeza adhabu ya faini au kifungo jela au vyote viwili kwa watu wasiokuwa na taaluma ya uwakili kufanya kazi hiyo kinyume cha sheria.


Wenza wa Spika, Katibu Mkuu Kiongozi

Muswada mwingine ulioandaliwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Eliezer Feleshi na kuwasilishwa bungeni juzi kwa mara ya kwanza, umependekeza kifungu cha 26 kurekebishwa ili kumwezesha mjane au mgane wa Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu aliyefariki dunia kulipwa mafao ya pensheni ya kila mwezi.

Muswada huo unapendekeza, “Pale Katibu Mkuu Kiongozi anapokuwa amefariki dunia, mjane au mgane apewe kila mwezi pensheni ya asilimia 40 ya mshahara wa Katibu Mkuu Kiongozi aliye kazini.”

Pia, kifungu cha 18 kinapendekezwa kurekebishwa ili kuweka utaratibu wa mwenza wa Spika mstaafu aliyefariki dunia kupokea pensheni ya kila mwezi.


Jaji Mkuu mstaafu

Jedwali la Sheria ya Stahiki na Mafao ya Majaji, Sura ya 424 inapendekezwa kurekebishwa ili kuwezesha Jaji Mkuu mstaafu kubadilishiwa gari kila baada ya miaka saba. Lengo la marekebisho hayo ni kulinda hadhi ya Jaji Mkuu.

Mapendekezo mengine ya muswada huo katika Sheria ya Stahiki na Mafao ya Majaji, Sura ya 424, ni kuongeza kifungu kipya cha 10A, ili kuweka masharti ya kufanyika kwa gwaride la heshima kila mwaka kwa ajili ya kuwaaga majaji wanaostaafu.

Lengo la marekebisho haya ni kutambua na kuthamini mchango wa majaji katika utoaji haki nchini.


Maoni ya wadau

Wakili wa kujitegemea, Alute Mghway alisema sifa walizoongeza ni kuongeza ugumu katika kupata uongozi ndani ya Baraza la Uongozi la TLS.

Alisema kwa masharti hayo, itafanya nafasi hizo kuchukuliwa na watu wenye umri mkubwa na kuwaacha watu wenye umri wa kati na vijana, ambao ndiyo wengi kwenye chama hicho. “Japokuwa sijaupata muswada wenyewe, ila unanieleza tu naona kwamba hao wajumbe wa baraza la uongozi watakuwa ni watu wazima wenye uzoefu mkubwa. Mbaya, itanyima uwakilishi kwa mawakili ambao ni vijana ukiondoa mwakilishi wao (wa vijana),” alisema.

Alisema si vibaya kuwa na viongozi wenye umri mkubwa, lakini chama chochote cha kitaaluma kinatakiwa kuwa na viongozi wa rika la chini kwa sababu hata viongozi vijana wana uwezo wa kuleta mabadiliko.

Mngway ambaye ni mwanachama wa TLS , alisema kwenye mikutano yao wameshapeleka mapendekezo na mawazo ya kubadilisha sheria, ili kuongeza muda wa uongozi kwa sababu mwaka mmoja hautoshi kulipima Baraza. “Mapendekezo yalikuwa ni kila baada ya miaka miwili kufanyike uchaguzi ili kuweza kupima ufanisi wa viongozo na mwaka mmoja ni mfupi sana. Hivyo kwangu ninaona ni sawa,” alisema.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga alisema marekebisho hayo yatasaidia kuwabana wasimamizi wa mirathi wasio waaminifu.

“Marekebisho haya yatasaidia sana kuwabana wasimamizi wa mirathi ambao si waaminifu, kwani hivi sasa wamekuwa tatizo kubwa,” alisema.

Nyongeza na Sharon Sauwa