Sh500 milioni kuokoa wanafunzi kufuata masomo umbali mrefu

Kamati ya mipango na fedha Halmashauri ya wilaya ya Chunya mkoani Mbeya ikiwa imefika katika kata ya Kambikatoto kwa ajili ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa shule ya sekondari inayojengwa katika kata hiyo kwa gharama ya zaidi y sh.500 milioni

Muktasari:

  • Wanachi wa Kata ya Kambikatoto wilayani Chunya, Mkoa wa Mbeya kuondokana na kuwapeleka wanafunzi kwenda kusoma kata jirani kufuatia kupatiwa fedha na serikali zaidi ya Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari.

Chunya. Wananchi wa Kata ya Kambikatoto wilayani Chunya mkoani Mbeya wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuwapatia Sh500 milioni kwa ajili ya ujenzi wa shule ya sekondari katika kata hiyo ambayo  pamoja na ukubwa wa kijiografia wa kata hiyo, umbali kutoka makao makuu ya wilaya, kutoka kata moja hadi  nyingine lakini haikuwa na  shule ya sekondari tangu kata hiyo ianzishwe.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti mbele ya kamati ya fedha, uongozi na mipango ya baraza la madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya inayoendelea na ziara ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo baada kamati hiyo kufika kwenye kata hiyo wananchi wamesema wanashukuru Serikali kwa kuwajari kwani siyo muda mrefu wamejengewa kituo cha afya na sasa sekondar. Wamedai watoto wao walikuwa wanakwenda kusoma kata jirani ambako nako ni mbali zaidi ya kilometa 39.

Mwita Chacha ni mmoja wa wananchi katika kata hiyo ya Kambikatoto anasema kwa wakati mmoja wamejengewa madarasa 12, anaamini watoto wao wanakwenda kusoma wakiwa maeneo jirani na ungalizi wa wazazi na  kuwapunguzia gharama walizokuwa wanakumbana nazo wanapowapeleka kata jirani.

Anasema hakuwahi kufikiria kuwa kata hiyo  itakuwa na shule ya sekondari kutokana  na kuwa ni kata iliyopo pembezoni mwa Wilaya ya Chunya naishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna ilivyoweza kutujali na kutusogezea huduma kwama kutujengea shule ya sekondari  yenye vyumba kumi na mbili tunakwenda kuongeza wasomi katika kata yetu.

Wananchi pia walitumia fursa hiyo kumuomba wenyekiti wa halmashauri awasaidie kutazama upya bei za milango na fremu iliyowekwa na fundi alipewa zabuni hiyo wakidai bei hiyo ni sawa na za mjini wakati eneo lao mbao zinapatikana kwa urahisi  kuliko mjini hivyo wananchi  wanamashaka na eneo hilo la bei za milango na fremu zake,” amesema mwananchi aliyejitambulisha kwa jina Mathias Songo.

Blandina Chingwile ameishukuru kamati hiyo kufika kutembelea mradi huu pamoja na kuwapatia fedha za mradi kwani amedai kwenye kata jirani wanafunzi walikuwa wanaishi huko wakiwa wamejipangia vyumba hivyo wengi wao walikuwa wakishindwa kumaliza masomo yao kutokana na vishawishi ikiwa ni pamoja na kupata mimba za utotoni.

Kamati ya fedha, uongozi na mipango imewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika ujenzi wa shule hiyo kwani shule hiyo ni yao. Pia itawasaidia wao wenyewe na familia na kwamba kwa kufanya hivyo watakuwa wametekeleza na kuulinda utaifa na uzalendo kwani serikali inapowaletea fedha haina maana wananchi hawatakiwi kushiriki kabisa.

Aidha kamati hiyo kupitia Mwenyekiti wa Halmashauri, Bosco Mwanginde imewaagiza viongozi wanaosimamia mradi huo kuandaa taarifa ya mapato na matumizi ya fedha inayotokana na nguvu za wananchi wa kata hiyo na baada ya kupata taarifa hiyo kamati ya wilaya itafanya ziara tena ili kuzungumza na wananchi maana serikali ya awamu ya sita inataka uwazi na ushirikshwaji wa jamii kuwa kipaumbele cha kwanza.

Kaimu Ofisa Elimu Sekondari, Nikusuma Kamoma amewataka wananchi kusimamia  matumizi ya fedha walizoletewa na serikali.

Amesema mradi utakapokamilika na fedha zitakazobakia wanaweza kutumia kuanzisha mradi mwingine katika kata hiyo jambo ambalo litafanya kata hiyo kuwa na kasi katika maendeleo kinyume na hapo mkifanya ovyo kwenye usimamizi mtaichafua Wilaya ya Chunya jambo litakalosababisha wilaya ikakosa uaminifu na kupelekea serikali kutoleta fedha za maendeleo.

Kata ya Kambikatoto ina jumla ya wanafunzi 298 wanaosma elimu ya Sekondari madarasa tofauti tofauti nje ya kata hiyo ambapo shule iliyo karibu kwa sasa hadi kuifikia kuna umbali wa zaidi ya kilometa 40 ina kidato cha kwanza pekee, wakati shule nyingine iko umbali wa kilometa 80 kutoka Kambikatoto.

 Hivyo ujenzi wa shule hiyo ni ukombozi wa kielimu wa wananchi wa Kata ya Kambikatoto kwa ujumla.