Sh500 milioni zatengwa kupeleka maji Mbopo-Chekanao

Muktasari:

  • Wananchi zaidi ya 2,000 wa Mtaa wa Mbopo-Chekanao wanatarajia kunufaika na mradi wa maji unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa) unaotarajia kukamilika Juni 2023.

Dar es Salaam. Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (Dawasa), imetenga zaidi ya Sh500 milioni ili kupeleka huduma ya maji kwa wananchi wa mtaa wa Mbopo-Chekanao, kata ya Mabwepande, wilayani Kinondoni.

Mradi wa maji Mbopo-Chekanao unaotekelezwa na Dawasa unatarajiwa kumaliza tatizo la maji lililodumu kwa kipindi kirefu ambao utakamilika Juni 2023 na kuwanufaisha zaidi ya wananchi 2,000.

Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo kutoka Dawasa, Mhandisi Adam Makindai amesema kazi zinazotekelezwa kwa sasa ni uchimbaji na ulazaji wa bomba za ukubwa wa inchi tofauti tofauti zikiwemo 8, 6, na 1.5 kwa umbali wa kilomita 18.1

"Kazi inaendelea kwa kasi na kama Mamlaka tunayofuraha tunakwenda kumaliza tatizo la maji kwa wananchi hawa kwa mara ya kwanza kabisa, niwatoe hofu hakuna mwananchi atakayekosa huduma ya maji katika mtaa huu wa Mbopo-Chekanao," amesema Mhandisi Makindai


Mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mbopo-Chekanao, Mohamed Bushiri amesema mradi huo utakapokamilika utakuwa faraja kwa wananchi ambao kwa sasa wanaisotea huduma hiyo.

"Mradi huu kwetu ni faraja, mtaa wetu haukua na mtandao wa majisafi kabisa, wananchi walihangaika kutafuta maji kwa gharama kubwa, lakini sasa kila mmoja ana matumaini ya maisha bora na uhakika wa majisafi pindi mradi utapokamilika," amesema Ndugu Bushiri.

Naye Rachel Michael, mkazi wa mtaa wa Mbopo-Chekanao ameahidi ushirikiano wa kutosha kwa Dawasa huku akiipongeza kwa kuwapelekea mtandao wa maji.

Mkazi huyo amesema, watahakikisha wanatoa ushirikiano wakati wa utekelezaji wa mradi pamoja na kuulinda pindi utakapokamilika,”ili uweze kudumu zaidi, kwani tukiacha miundombinu ukaharibiwa, tutaumia tena.”