Sh60 bilioni kuboresha bandari 15 Kanda ya Ziwa

Waandishi kutoka Klabu ya waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga wakiwa kwenye ziara ya kujifunza mambo ya uwekezaji wa Bandari. Picha na Suzy Butondo

Muktasari:

Serikali imetenga Sh60 bilioni kuboresha miundombinu ya bandari 15 zilizopo mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa, zinazosafirisha mizigo kwenda nchi za Afrika Mashariki.

Shinyanga. Serikali imetenga Sh60 bilioni kuboresha miundombinu ya bandari 15 zilizopo mikoa mitano ya Kanda ya Ziwa, zinazosafirisha mizigo kwenda nchi za Afrika Mashariki.

Akizungumza na waandishi wa habari Agosti 31, 2023 Meneja wa Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) Kanda ya Ziwa Victoria, Ferdinand Nyathi amesema maboresho hayo yataongeza shehena za mizigo na kipato.

Nyathi aliyekuwa akizungumza na waandishi hao waliotembelea bandari hiyo kwa ajili ya kujifunza mambo mbalimbali yanayofanywa na TPA amesema licha ya changamoto ya uchakavu wa miundombinu kusababisha mizigo kuja kwa uchache lakini kwa mwaka wanauwezo wa kupokea tani 3000.

"Serikali imetoa  fedha kwaajili ya kufanya ukarabati bandari hizi ikiwemo ya Kemondo na Bukoba,  hivyo tunatarajia  ukuaji wa uchumi kwa uingizaji wa mizigo kutoka kwenye nchi za Afrika Mashariki.” amesema Nyathi

Amesema kwa Kanda ya Ziwa kuna bandari kubwa sita na ndogo tisa katika mikoa mitano ya Shinyanga, Mwanza, Mara, Kagera na Simiyu huku fedha hizo zikiwa zimeanza kufanya maboresho ikiwemo bandari ya Ziwa Victoria Kaskazini iliyotengewa Sh18.6 milioni tayari imeanza kukarabatiwa likiwemo jengo la wasafiri.

Kwa upande wake Ofisa Bandari Kavu ya Isaka, Abel Mshang’a amesema wanapokea mizigo kwa njia ya reli ambapo kituo hicho kilijengwa mwaka 1995 na kuanza kazi rasmi mwaka 2017 kwa ajili ya kutoa huduma za kibandari na kina uwezo wa kuchukua makasha 300 hadi 350 yenye urefu wa futi 40 pamoja na kuchukua makontena 22 kwa wakati mmoja.

“Bandari ya Isaka inarahisisha  mizigo kufika kwa haraka na watumiaji wa bandari wanapata manufaa makubwa ya kusafirisha mizigo pasipo na shaka na hurudishwa kasha likiwa tupu bure baada ya mzigo uliobebwa kutolewa na wananchi wanaozunguka eneo la bandari wanafaidika kutoa huduma mbalimbali na kukuza uchumi wao.”amesema Mshang’a

Mkuu wa kituo cha reli ya kati Isaka, Zacharia Mwantunge amesema wamekuwa wakipokea mizigo kama ngano kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda, Nakuru, Congo na wamekuwa wakipokea mizigo midogo midogo ya mahindi na mpunga kwa wananchi wa kawaida kutoka Katavi na Mpanda.

“Katika makasha 57 yaliyohudumiwa mwezi huu na Shirika la Reli ni Makasha 17 ya mabomba ya mafuta yaliyokuja kwa njia hiyo, hivyo bado kuna manufaa makubwa ya utumiaji wa reli na Bandari kwa masaa 24 ikifanya kazi.”amesema Mwatunge.

Baadhi ya wananchi wanaozunguka eneo la Bandari ya Isaka wilayani Kahama Mkoani Shinyanga,  Bakari Athuman na Joseph Nkuba wamesema wao wamekuwa wakifaidika na bandari hiyo pale wanaposhusha mizigo inayoletwa bandarini hapo ambapo wamekuwa wakifanya kazi hizo na kujipatia kipato.

Mama Lishe, Mariam Joseph amesema bandari kavu iliyopo Isaka imesaidia kina mama wanaouza chakula kujiongezea kipato kwani madereva wanakwenda na magari makubwa  na kushusha mizigo wamekuwa wakiwahudumia kwa chakula hivyo kujiongezea kipato kinachowasaidia kuwasomesha watoto wao.

Naye, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru amesema katika ziara hiyo wamejifunza mambo mengi ya uwekezaji wa bandari ambayo ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi hapa nchini akidai kupitia kalamu zao wataielimisha jamii ili iweze kuelewa kazi zinavyofanyika katika bandari hizo.