Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Sh787 bilioni zatengwa kukopesha wanafunzi 250,000

Muktasari:

  • Serikali imetenga Sh787 bilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa jumla ya wanafunzi 250,000, idadi hiyo imeongezeka kutoka wanafunzi 224,056 mwaka 2023/2024.

Dar es Salaam. Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza rasmi kufunguliwa kwa dirisha la uombaji mikopo ya elimu ya juu kwa njia ya mtandao 'Online Loan Application Management System' (OLAMS) kwa mwaka wa masomo 2024/2025.

Dirisha hilo la maombi litakuwa wazi kwa muda wa siku 90 kuanzia Juni 1 hadi Agosti 31, 2024 huku waombaji wakisisitizwa kuzingatia muda uliowekwa.

Hatua hiyo imekuja baada ya Mei 27 mwaka huu katika viwanja vya Shule ya Sekondari Popatlal iliyopo jijini Tanga Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Adolf Mkenda kuzindua miongozo mitano ya utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2024/2025 ambao utaanza Oktoba mwaka huu.

Miongozo hiyo inahusu utoaji mikopo kwa wanafunzi wa shahada za awali, stashahada, stashahada ya umahiri katika mafunzo ya sheria kwa vitendo, shahada za uzamili na uzamivu pamoja na ruzuku za Samia kwa mwaka 2024/2025.

Akizungumza leo Juni 6, 2024 jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dk Bill Kiwia ametoa rai kwa wanafunzi, wazazi na walezi kuisoma na kuielewa miongozo hiyo kabla ya kuingia hatua ya uombaji wa mikopo.

"Miongozo hiyo ipo katika lugha ya Kiswahili na Kiingereza ili wadau wetu wakiwemo wazazi na walezi waweze kuisoma na kuielewa, tunasisitiza wanafunzi wanaoomba mkopo kuisoma na kuzingatia maelekezo yaliyomo katika miongozo hiyo," amesema.


Mambo ya kuzingatia

Dk Kiwia pia amegusia mambo muhimu ya kuzingatia kwa waombaji wa mikopo ikiwemo kuhakikisha namba ya mtihani wa kidato cha nne anayotumia kuomba mkopo iwe hiyohiyo atakayotumia kuomba udahili chuoni.

Pia mwombaji mkopo yeyote atapaswa kuwa na akaunti ya benki yoyote aipendayo.  "Ni muhimu kukumbusha kuwa mwombaji mkopo ahakikishe majina yanayosomeka katika akaunti ya benki yanafanana na yaliyomo katika namba yake ya kidato cha nne," amesema.

Pia ameongeza kuwa kwa wale waombaji wenye namba ya kitambulisho cha Taifa (Nida) watapaswa kuiweka wakati wa kuomba mkopo, na iwapo mwombaji hana anaweza kuendelea na maombi bila namba hiyo.

Awali Kiwia amesema Serikali imetenga Sh787 bilioni kwa ajili ya mikopo na ruzuku kwa jumla ya wanafunzi 250,000.

Idadi hiyo inaelezwa kuongezeka kutoka wanafunzi 224,056 mwaka 2023/2024 hivyo kufanya ongezeko la jumla ya wanafunzi takribani 25,944.

Akizungumza katika uzinduzi huo Mkurugenzi wa Upangaji Mikopo (HESLB), Dk Peter Mmari amewataka waombaji wa mikopo hiyo kutumia muda uliotolewa vizuri na kuacha tabia za kuanza kuomba mikopo siku chache kabla ya dirisha kufungwa.

"Tabia hii itawafanya kushindwa kufanya maombi hayo kwa ufanisi kwani nyaraka nyingine zitahitaji muda kidogo wa kufuatilia," amesema.