Sh950 milioni kufungua Saccos 20 za wakulima

Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila (watatu kushoto) akifungua mkutano wa 33 wa Chama Kikuu cha Ushirika mkoani humo (KCU -1990 Ltd) uliofanyika mjini Bukoba. 

Muktasari:

Kuanzishwa kwa saccos hizo kunalenga kuwawezesha wakulima wa kahawa kupata fursa ya mikopo nafuu ili kuondokana siyo tu na mikopo umiza, bali pia tabia ya kuuza kahawa ambayo bado iko shambani maarufu kama obutura.

Bukoba. Wakulima wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa Kagera (KCU-1990 Ltd) wamepitisha Sh950.3 milioni kama mtaji kwa ajili ya kufungua Saccos kwenye vyama vya msingi (Amcos) 20 za mkoa huo.

Kuanzishwa kwa saccos hizo kunalenga kuwawezesha wakulima wa kahawa kupata fursa ya mikopo nafuu ili kuondokana siyo tu na mikopo umiza, bali pia tabia ya kuuza kahawa ambayo bado iko shambani maarufu kama obutura.

Umuamuzi wa kupitisha fedha hizo ulifikiwa wakati wa mkutano mkuu wa 33 wa KCU-1990 LTD uliofanyika mjini Bukoba mwishoni mwa wiki iliyopita

Akitoa taarifa ya matokeo ya mkutano huo, Mwenyekiti wa KCU-1990 LTD, Ressy Mashulano amesema mapendekezo ya kufungua Saccos hizo ni matokeo ya ziara ya mafunzo waliyofanya wajumbe wa bodi ya chama hicho cha ushirika nchini Rwanda.

“Mtaji wa zaidi ya Sh950.3 milioni zitakazotumika kuanzisha saccos hizo zitatokana na ziada ya fedha za ustawi wa jamii kwa msimu 2021/22 na 2022/23,” amesema Mashulano

Kwa mujibu wa mchanganuo, Sh453.6 milioni zitatokana na ziada ya fedha za ustawi wa jamii kwa msimu 2021/22 huku Sh496.7 milioni zikitana na ziada ya ustawi wa jamii kwa msimu wa 2022/23.

“Kila Amcos (Chama cha Msingi cha Ushirika) kitaanzisha sacoos yake kwa mtaji wa Sh47 milioni; na tutaanza na vyama vinavyouza kahawa nyingi kwa msimu,” amesema Mashulano

Amesema kuanzishwa kwa Saccos hizo kutawawezesha wakulima kupata mikopo kwa ajili ya kilimo na mahitaji mengine ya kifamilia ikiwemo ada za watoto wao na kurejesha baada ya mavuno.

Chama cha KCU - 1990 Ltd kinachonunua kahawa katika Wilaya za Bukoba, Muleba na Misenyi kina jumla ya vyama vya msingi 135, vyama 35 kati ya hivyo vikiwa vya kahawa hai.

Kwa mujibu wa Mhasibu Mkuu wa chama hicho, Thatianus Kamoi, KCU-1990 LTD kinatarajia kukusanya kilo 12 milioni za kahawa ya maganda katika msimu wa 2023/24 huku makisio ya kahawa safi aina ya Arabika na Robusta ikiwa ni kilo 2.5 milioni

Msimu 2022/2023, chama hicho kilikisia kukusanya kilo 16 milioni za kahawa maganda lakini zilizokusanywa zilikuwa kilo 9 milioni wakati makisio ya makusanyo ya kahawa safi ilikuwa kilo 2.4 milioni, lakini zilizokusanywa zilikuwa kilo 2.3 milioni.

Mhasibu huyo amesema bei ya kahawa ya maganda kwa msimu huu wa 2023/2024 itategemea mnada huku bei ya kahawa hai aina ya Robusta inatarajiwa kuwa Sh5, 300 huku Arabika ikitarajiwa kuwa Sh4, 700.

Awali akifungua mkutano mkuu wa KCU-1990 LTD, Katibu Tawala Mkoa wa Kagera, Toba Nguvila amewataka wakulima wa kahawa mkoani humo kuacha tabia ya kuuza kahawa kimagendo kwa wafanyabiashara wasio waaminifu kwa sababu kufanya hivyo siyo tu ni kinyume cha sheria, bali pia inawakosesha mapato stahiki na kodi ya Serikali.

"Serikali kupitia vyombo vys ulinzi na usalama infuatilia kwa karibu taarifa za biashara za magendo ya kahawa wilayani Kyerwa ambayo baadhi ya wanunuzi wanaivusha kwenda nchi jirani kinyume cha sheria. Nawasihi wakulima kuzingatia taratibu za nchi,” amesema Nguvila.

Amesema ni nia ya Serikali kuendelea kulinda maslahi ya wakulima ndiyo maana ikaanzishwa mfumo wa kuuza kahawa kwenye mnada huku akiwaagiza maafisa ugani, Bodi ya Kahawa na Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika mkoa wa Kagera kuhakikisha mizani ya zamani ya rula haitumika kupima mazao ya wakulima, badala yake itumike mizani ya kidigitali.

Amewataka wakulima kuzingatia kanuni na taratibu za kilimo kwa kuvuna kahawa iliyoiva na kuianika sehemu sahihi kulinda na kuongeza thamani ya mazao yao kwenye soko la ndani nan je ya nchi,toanika kwenye udongo ili kahawa hiyo iweze kuwa na thamani inapopelekwa kwenye viwango vya kimataifa.