Shaffih Dauda aachiwa kwa dhamana, Soudy Brown, Maua waendelea kusota rumande

Muktasari:

Mtangazaji wa Clouds katika kipindi cha Shilawadu, Soud Kadio ‘Soud Brown’ aliyekamatwa siku tano zilizopita na kuwa rumande katika Kituo Kikuu cha Polisi cha Dar es Salaam, amefikishwa jana Septemba 24, 2018, mahakamani alikosomewa shtaka moja la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali.


Dar es Salaam. Baada ya kusota mahabusu kwa siku tisa, Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaa jana iliwaachia kwa dhamana watangazaji wawili wa Kituo cha Televisheni cha Clouds, Shaffih Dauda na Sudi Kadio ‘Soudy Brown.’

Hata hivyo, Soudy Brown ambaye ni mtangazaji wa kipindi cha Shilawadu baada ya kupata dhamana katika kesi inayomkabili ya kusambaza maudhui bila kibali alirudishwa kituo kikuu cha polisi kwa ajili upelelezi kuhusiana na kesi nyingine inayomkabili.

Soudy Brown na Maua Sama wanaendelea kushilikiwa polisi kwa madai ya kuonekana katika video mtandaoni wakikanyaga fedha.

Mbali na watangazaji hao wengine walioachiwa kwa dhamana ni Benedict Kadege, Antony Luvanda ‘MC Luvanda’ na kampuni yake ya Home of Company Limited, Michael Mligwa na John Lusingu.

Watuhumiwa hao waliokamatwa Septemba 16 walifikishwa mahakamani hapo jana kujibu tuhuma zinazowakabili huku Msanii Maua Sama na meneja wake Fadhili Kondo na Soudy Brown wakiendelea kusota mahabusu ya Kanda Maalumu ya Dar es Salaam.

Washtakiwa hao sita walisomewa mashtaka yanayowakabili mahakamani hapo kwa nyakati tofauti na kwa mahakimu tofauti.

Mahakimu waliowasomea mashtaka washtakiwa hao ni Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba, Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi, Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustino Rwizile, Hakimu Mkazi Mkuu, Hamza Wanjah na Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Kelvin Mhina.

Akimsomea mashtaka MC Luvanda, wakili wa Serikali Mkuu, Tumain Kweka alidai mbele ya Hakimu Shaidi kuwa mtuhumiwa na kampuni anayomiliki ya Home of Company Limited walitumia kikoa (.tz) ambacho hakijasajiliwa Tanzania.

Alidai kati ya Februari 24 na Septemba, 2018 katika jiji la Dar es Salaam, mshtakiwa huyo alianzisha na kutumia mtandao wa www.mcluvanda.com ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Katika shtaka la pili, Kweka alidai katika kipindi hicho mshtakiwa huyo alianzisha na kutumia mtandao huo ambao haukuwa na kikoa cha .tz.

Shtaka la tatu ni la kutoa huduma ya online bila ya kuwa na kibali.

MC Luvanda anadaiwa katika kipindi hicho alitoa huduma hiyo kupitia online TV ya MC Luvanda pasipokuwa na kibali kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Mawasiliano Tanzania (TCRA).

Mshtakiwa huyo alikana shtaka huku upande wa mashtaka ukidai upelelezi bado haujakamilika.

Wakili Jebra Kambole anayemtetea mshtakiwa huyo aliiomba Mahakama itoe dhamana kwa mteja wake kwa sababu shtaka linadhaminika.

Hakimu Shaidi alimtaka mshtakiwa kuwa na mdhamini mmoja mwenye barua na kitambulisho ambaye atasaini bondi ya Sh5 milioni. Mshtakiwa alikidhi masharti na kesi iliahirishwa hadi Oktoba 23.

Kwa upande wake Soudy Brown, anakabiliwa na shtaka la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kuwa na kibali.

Wakili wa Serikali Mkuu Faraja Nguka akishirikiana na wakili Estazia Wilson walimsomea shtaka hilo mshtakiwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustino Rwizile. Nguka alidai kati ya Juni 11 na Septemba jijini Dar es Salaam, kwa kutumia online TV inayojulikana kwa jina la Shilawadu mshtakiwa huyo alitoa maudhui katika mtandao huo bila ya kuwa na kibali kutoka TCRA.

Baada ya kusomewa shtaka hilo, mshtakiwa huyo alikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi bado haujakamilika. Kesi iliahirishwa hadi Oktoba 18.

Pia, washtakiwa wawili, Shaffih Dauda na Benedict Kadege walipandishwa kizimbani wakikabiliwa na shtaka la kutumia maudhui mtandaoni bila ya kibali.

Wakili wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka akishirikiana na mawakili Mutalemwa Kishenyi na Mwanaamina Kombakono waliwasomea shtaka hilo washtakiwa hao mbele ya Hakimu Mfawidhi, Kelvin Mhina.

Akisoma shtaka hilo, wakili Kombakono alidai kati ya Juni 14 hadi Septemba ndani ya jiji la Dar es Salaam kwa kutumia online TV inayojulikana kwa jina la Shaffih Dauda, walitoa maudhui katika mtandao huo bila ya kibali kutoka TCRA.

Baada ya kusomewa shtaka hilo washtakiwa hao walikana na upande wa mashtaka ulidai upelelezi wa kesi hiyo bado haujakamilika.

Hata hivyo, wakili Kambole anayewatetea washtakiwa hao aliomba wateja wake wapewe dhamana kwa sababu shtaka linadhaminika.

Wakili wa Serikali Kweka alidai hawapingi kutoa dhamana ila kama Mahakama itaridhia kutoa dhamana izingatie kifungu cha 148 (6)(7) cha Sheria ya Makosa ya Jinai.

Akitoa masharti ya dhamana kwa washtakiwa hao, Hakimu Mhina alimtaka kila mshtakiwa awe na wadhamini wawili wenye kitambulisho na barua ambazo zinatambulika.

Pia, kila mdhamini alitakiwa kusaini bondi ya Sh15 milioni na hawaruhusiwi kusafirisha nje ya Tanzania bila kupata kibali cha Mahakama.

Pia, wametakiwa kuwasilisha hati zao za kusafirisha mahakamani Oktoba 8.

Hata hivyo, washtakiwa walifanikiwa kupata dhamana na kesi iliahirishwa hadi Oktoba 8 itakapotajwa kwa ajili ya kuangalia upelelezi kama utakuwa umekamilika au la.

Naye Mpigapicha Michael Mlingwa alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba akikabiliwa na shtaka la kutumia mtandao bila kusajiliwa na TCRA.

Akimsomea mashtaka mshtakiwa huyo, Wakili wa Serikali, Faraja Nguka alidai mshtakiwa huyo katika kipindi cha Februari 24 jijini Dar es Salaam alimiliki na kutumia mtandao wa www.Slidevisual. Com bila leseni kutoka TCRA.

Mshtakiwa alikana shtaka hilo na yuko nje kwa dhamana yenye masharti ya kuwa na wadhamini wawili, waliosaini dhamana ya maandishi ya Sh10 milioni. Kesi iliahirishwa hadi Oktoba 8.

Mshtakiwa mwingine, John Lusingu alifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Hamza Wanjah kwa shtaka la kutumia mtandao wa www.magazetini.com bila leseni.

Mshtakiwa alikana mashtaka hayo anayodaiwa kuyatenda Februari 24 na Septemba yuko nje kwa dhamana hadi Oktoba 5 kwa ajili ya kesi yake kutajwa.