Shahidi aieleza mahakama Diwani aliyopigwa

Aliyekua Mkuu wa wilaya ya Hai,Lengai Ole Sabaya (katikati) na watuhumiwa wenzake wakiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza kwaajili ya  kujibu tuhuma zinazowakabili kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi  Arusha jana.Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Wakati Shahidi wa pili, Numan Jasin (17) akieleza Mahakama namna walinzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, walivyompiga Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi, mawakili wa Sabaya wameshinda pingamizi dogo kuzuia shahidi kuulizwa maswali yanayoelezwa kuwa ni majibu.

Arusha. Wakati Shahidi wa pili, Numan Jasin (17) akieleza Mahakama namna walinzi wa aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya, walivyompiga Diwani wa Sombetini (CCM), Bakari Msangi, mawakili wa Sabaya wameshinda pingamizi dogo kuzuia shahidi kuulizwa maswali yanayoelezwa kuwa ni majibu.

Awali wakili Edmund Ngemela aliwasilisha pingamizi kuhusu maswali aliyoulizwa shahidi hasa kuwatambua watuhumiwa na kudai kuwa yanakiuka sheria.

Hata hivyo, Wakili Mwandamizi, Abdallah Chavula alipinga hoja hiyo na kueleza shahidi anaulizwa kwa kuzingatia sheria.

Akitoa uamuzi wa suala hilo, Hakimu Mkazi, Odira Amworo aliutaka upande wa mashtaka kutouliza maswali yenye kuelekeza majibu.

Sehemu ya mahojiano kati ya Wakili wa Serikali Mkuu Tumaini Kweka na shahidi huyo yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili Kweka: Endelea kuieleza Mahakama mabaunsa wameshaamriwa kumsachi Bakari Msangi nini kilifuata.

Shahidi: Huyo kiongozi alimwambia Bakari umekuja kusaidia magaidi wenzako.

Wakili: Baada ya kueleza hivyo, nini kilitokea?

Shahidi: Bakari alikuwa analia kwa nguvu na kuomba msamaha, lakini kiongozi huyo aliamuru apigwe tena.

Wakili: Nini kilichosabanisha alale chini?

Shahidi: Baada ya kupigwa kipigo kizito kiongozi (Sabaya) aliamuru wamkalishe tena, walimnyanyua wakamkalisha.

Baadaye kiongozi wao alichukua silaha yake aina ya bastola akawa anamnyooshea Bakari akamwambia ana kiherehere na anamfuatilia, atammaliza.

Wakili: Mmmh.

Shahidi: Bakari akawa anamuomba msamaha huyo kiongozi akamwambia mke wake na mtoto wake ni wagonjwa kwa hiyo asimuue.

Wakili: Endelea.

Shahidi: Basi huyo kiongozi aliamuru mabaunsa wamfungue Bakari pingu.

Wakili: Hebu isaidie Mahakama umezungumzia Bakari kufunguliwa pingu wakati gani alifungwa pingu?

Shahidi: Alipowekwa chini ya ulinzi.

Wakili: Ni nani aliyehusika kumfunga pingu?

Shahidi: Ni mmoja wa mabaunsa baada ya kupewa amri na kiongozi wao (Sabaya).

Wakili: Katika kundi hilo lote alitambulika kama nani.

Shahidi: Kiongozi wao.

Wakili: Walikuwa wakimuita kiongozi?

Shahidi: Ndiyo

Wakili: Nini kilitokea baada ya kuamuru afunguliwe?

Shahidi: Bakari akawa anaendelea kuomba msamaha na huyo kiongozi wao alinifuata akaniambia nimpigie kijana aliyekuwa na yule dada nimuite dukani (Abumansoor) aje dukani haraka.

Wakili: Nini hasa zilikuwa sababu za kumpigia simu huyo kijana aje?

Shahidi: Aliniambia kuna biashara alifanya na yule dada mwenye lafudhi ya kikenya ambaye alikuwa mteja wetu Februari 8 na 9 na alikuwa chini ya ulinzi na sisi pale.

Wakili: Baada ya kukwambia ulifanyaje?

Shahidi: Nilimpigia Abumansoor nikamwambia unatakiwa uje dukani haraka kuna tatizo, lakini alinijibu hajisikii vizuri na kutokana na muda kuisha hatoweza kuja. Kiongozi huyo alichukua simu mkononi kwangu akamwambia anampa dakika tano awe amefika dukani, alikata simu na akanirudishia. Halafu akaniambia nimpigie mwenye duka akasema hatuhitaji sisi anamhitaji Mohamed Saad na atakapofika sisi wote tutaachiwa huru.

Wakili: Baada ya kukwambia umpigie huyo ulifanyaje?

Shahidi: Nilijaribu kumpigia akawa hapatikani, nikamwambia atuachie huru, kaniambia nitafute namna yoyote apatikane na akasema akija yeye atatuachia wote.