Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shahidi: Baba Levo aliahidi Sh2 milioni ujenzi wa kanisa

Muktasari:

  • Mbunge wa Kigoma Mjini, maarufu kwa jina la Baba Levo anakabiliwa na kesi ya uchaguzi ambayo imeendelea kusikilizwa ushahidi wa upande wa walalamikaji wanaopinga ushindi wake.

Kigoma.  Shahidi wa pili katika kesi ya uchaguzi inayomkabili Mbunge wa Kigoma Mjini (CCM), Clayton Chipando, maarufu Baba Levo, Pendo Kombolela ameieleza Mahakama kuwa mbunge huyo aliahidi kuchangia Sh2 milioni katika ujenzi wa Kanisa la Moravian.

Pia ameeleza siku ya uchaguzi, mbunge huyo alimfanyia fujo akimtaka asimharibie uchaguzi kwani alishatumia pesa nyingi na kwamba alitaka kumteka, lakini akashindwa baada ya wapiga kura wengine kumsaidia.

Shahidi hiyo ambaye ni mmoja wa walalamikaji ametoa maelezo hayo leo Jumatano Julai 8, 2026 wakati kesi hiyo ilipoendelea kusikilizwa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma.

Baba Levo alitangazwa mbunge katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, akimshinda mpinzani wake mkubwa kutoka ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe.

Shahidi huyo Pendo na wenzake watatu, Johary Kabourou, Lumu Mwitu, Pendo Kombolela na Luma Akilimali wamefungua kesi wakipinga ushindi wake.

Kesi hiyo ya uchaguzi namba 28949 ya Mwaka 2025 mbali na yeye Baba Levo ambaye ni mlalamikiwa wa pili katika kesi hiyo walalamikiwa wengine ni Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kigoma Mjini na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Walalamikaji hao wanadai kuwa uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki kwa kuwa uligubikwa na kasoro nyingi za Sheria na Kanuni za Uchaguzi.

Wanabainisha kasoro hizo kuwa ni pamoja na ukiukwaji wa taratibu, kanuni na Sheria za Uchaguzi, vitendo vya rushwa na udini vilivyooneshwa na mlalamikiwa wa pili, Baba Levo.

Hivyo wanaiomba mahakama hiyo pamoja na mambo mengine iamuru ufanyike upekuzi na uhesabuji upya wa karatasi za kupigia kura na kisha ibatilishe na kutengua uchaguzi huo.

Akiongozwa na wakili wa walalamikaji shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa atatoa ushahidi wake kwa njia ya maandishi, ambayo tayari yalishawasilishwa mahakamani na akaiomba mahakama iupokee.

Kiongozi wa jopo la mawakili wa Serikali, Mark Mulwambo na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa wamesema kuwa hawana pingamizi ushahidi wake huo wa maandishi kupokewa.

Jaji Victoria Nongwa anayesikiliza kesi hiyo ameupokea ushahidi huo wa maandishi wa shahidi huyo na shahidi huyo akaanza kuhojiwa maswali ya dososo na mawakili wa walalamikiwa, ambao wamemuhoji maswali mbalimbali kuhusiana na ushahidi wake huo wa maandishi.

Katika mahojiano yake na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Stanley Kalokola shahidi huyo ameieleza mahakama kuwa katika ushahidi wake wa maandishi ameandika kuwa ni mwanachama wa ACT- Wazalendo.

Amesema kwamba alielezwa na mawakala wa chama hicho kuwa waliondolewa katika kituo cha kupigia kura kwa kuwa walikuwa na daftari la wapigakura.

Hata hivyo alipopewa nakala ya hati ya madai ambayo amesema kuwa kama mlalamikaji aliisaini imeandikwa kuwa mawakala wa chama hicho walizuiwa kuingia kituoni kwa kuwa walikuwa na daftari hilo (na si kuwa walitolewa).

Hata hivyo amefafanua kuwa walizuiwa lakini walipoingia walitolewa, ndipo akaenda kuwauliza sababu ya kutolewa.

Kwa mujibu wa ushahidi wake wa maandishi, alipoingia kituoni alikuta karatasi za kura zikiwa zimechanwachanwa lakini hakuona kama tayari zilikuwa na alama ya tiki au la.

Katika mahojiano hayo amesema kuwa Baba Levo alimfanyia vurugu siku ya kupiga kura na akamuonya kuwa asimharibie uchaguzi kwa kuwa ameshatoa pesa nyingi.

Lakini alipopewa maelezo yake kuyasema yanasomeka kuwa Baba Levo alimuomba amuharibie uchaguzi lakini akadai kuwa kuna makosa ya uchapaji.

Katika ushahidi wake ameeleza kuwa Baba Levo alitoa rushwa na akafafanua kwa mdomo kuwa pia alitoa ahadi ya kuchangia Sh2 milioni za ujenzi wa Kanisa la Moravian, na ahadi kama hiyo wakati wa uchaguzi ni rushwa.

Hata hivyo, amedai kuwa hakwenda kuripoti polisi kuhusu tukio la kufanyiwa vurugu na kupigwa na Baba Levo kwa kuwa alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi kama mtuhumiwa.

Amedai kuwa kwa sasa yuko hapa kwa ajili kesi ya uchaguzi, lakini pia ana mpango wa kumfungulia kesi kwa kumpiga.

Wakati akihojiwa na wakili wa Baba Levo, Thomas Msasa shahidi huyo ameeleza kuwa awali taarifa ya Baba Levo kutoa mchango kanisani aliambiwa na rafiki yake aitwaye Neema, lakini baadaye naye akaona kwenye mitandao ya kijamii ikiwamo Instagram.

Akihojiwa na wakili wa walalamikiwa, John Seka katika majibu yake ya maswali ya ufafanuzi wa maswali ya mawakili wa walalamikiwa, amedai kuwa wakati Baba Levo na watu wake aliowaelekeza wamteke walishindwa kwa kuwa watu waliokuwa katika kituo cha kupigia kura walimsaidia.


Endelea kufuatilia Mwananchi