Shahidi kesi ya ‘Mfalme Zumaridi’ augua mahakamani, kesi yapigwa kalenda

Muktasari:

Kesi inayomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 imeshindwa kuendelea baada ya shahidi wa upande wa Jamhuri ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti Evodius kuugua muda mfupi kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Mwanza. Kesi inayomkabili Diana Bundala maarufu Mfalme Zumaridi na wenzake 83 imeshindwa kuendelea baada ya shahidi wa upande wa Jamhuri ambaye ni askari wa Jeshi la Polisi, Sajenti Evodius kuugua muda mfupi kabla ya kuanza kutoa ushahidi wake.

Katika kesi hiyo ya jinai namba 12/2022 Mfalme Zumaridi na wenzake wanashtakiwa kwa kosa la kufanya kusanyiko lisilo na kibali.

Akitoa ombi leo Alhamisi Juni 30,2022 mahakamani mbele ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, Monica Ndyekobora, Wakili Mwandamizi wa Jamhuri, Emmanuel Luvinga ameiomba mahakama hiyo iahirishe mchakato wa utoaji wa ushahidi katika shauri hilo baada ya shahidi wa upande huo kuugua ghafla.

Lubinga amesemea shahidi huyo alifika muda sahihi na alianza kujisikia vibaya baada ya kupata maumivu ya kichwa lakini wakamsihi avumilie, hata hivyo kesi hiyo ilishindwa kuanza muda iliyotarajiwa badala yake ikaanza saa 8:02 mchana jambo ambalo shahidi ameshindwa kuhimili na hivyo wakaiomba mahakama kupangiwa tarehe nyingine.

Shahidi huyo namba mbili katika kesi hiyo alikuwepo mahakamani hapo na alisimama kizimbani lakini kutokana na kujisikia vibaya ameshindwa kutoa ushahidi wake.

"Mheshimiwa hakimu shahidi amefika kama alivyotakiwa lakini alianza kujisikia vibaya tukamuomba avumilie akakubali kwasababu alijua kesi itaanza mapema, lakini maumivu yameendelea na tangu anasema amevumilia sana kwakuwa anaumwa tunaomba tupangiwe tarehe nyingine," amesema Luvinga.

Kwa upande wake Wakili wa utetezi, Steven Kitale amesema hawana pingamizi na ombi hilo huku akiiomba mahakama itoe upendeleo pale shauri hilo litakapoletwa tena mahakamani lipewe upendeleo na liende haraka kama ilivyokusudiwa.

Baada ya ombi hilo kutoka kwa wakili wa upande wa Jamhuri, Hakimu Mkazi wa mahakama hiyo, Monica Ndyekobora ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 13,2022 kwa ajili ya kuendelea na usikilizaji wa ushahidi kutoka kwa shahidi huyo.

Washatakiwa wengine 83 wanaoshtakiwa katika kesi hiyo walifika wote mahakamani hapo mapema asubuhi huku wakionekana wenye furaha ambapo walikuwa wanabadilishana mawazo kwenye vikundi nje ya mahakama kabla ya shauri lao kuanza saa 8 mchana.

Baada ya kufika mahakamani Mfalme Zumaridi alionekana mwenye furaha akibadilishana mazungumzo na mawakili wake huku vicheko vikisikika akifurahia kupigwa picha na waandishi wa habari tofauti na hali ilivyokuwa wakati shauri hilo linatajwa kwa mara ya kwanza, ambapo baada ya kesi kuhairishwa wafuasi wake (washtakiwa wenzake) walikwenda kuchukua baraka kwake na kutoka nje ya ukumbi wa mahakama wakifurahi na kuweka mikono yao vifuani.