Shamba la miti Mtibwa lakumbwa na changamoto ya uvamizi wa wafugaji

Mvomero. Shamba la miti Mtibwa lililopo maeneo ya Pagale wilayani hapa linakabiliwa na changamoto ya wafugaji kuvamia kambi za wahifadhi zaidi ya mara 10 kati ya Januari hadi sasa na kupora ng’ombe waliokamatwa katika hifadhi pamoja uharibifu wa mali mbalimbali kambini hapo.

Hayo yamebainika jana wakati Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Misitu Tanzania (TaFF) ilipotembelea shamba hilo linalomilikiwa na Wakala wa Hudumu za Misitu (TFS) ili kufanya ukaguzi wa shughuli zilizotekelezwa kwa kutumia fedha za ruzuku ya zaidi ya Sh500 milioni iliyotolewa na  TaFF kuanzia mwaka wa fedha 2017/18 hadi 2021.

Akizungumzia tatizo hilo Kamshina Mhifadhi Mkuu wa Misitu (TFS), Prof. Dos Santos Silayo amesema changamoto kubwa kwa shamba la miti Mtibwa ni mazoea watu kuchunga katika maeneo ya hifadhi au kupita, wafugaji wengi hapa kuonekana hawana makazi katika vijiji vya jirani hivyo wanalazimisha kubaki katika eneo la msitu jambo ambalo halikubaliki.

“Nitoe wito kuendelea kuisimamia rasilimali hii nashukuru kwa askari waliopo katika eneo hii wanafanya kazi vizuri. Mwenyekiti na Bodi yako naomba muendelee kusaidia shamba hili katika kutekeleza hadhi yake na kazi kubwa ni kuhakikisha hakuna uharibifu wa kile ambacho tumekifadhiri,”

“Sisi TFS tutaendelea kutoa kila msaada unaohitaji kwa ajili ya usimamizi wa shamba hili pia tutashukuru kama bodi yako itaendelea kusaidia upande wa pili wa kutekeleza umuhimu wa sheria ili wananchi wapate uelewa kuwa hii ni rasilimali ya taifa na hawapaswi kuingia katika maeneo ya misitu na hatua kali zitachukuliwa kadri inavyowezekana,” alisema Prof Silayo.

Awali Mhifadhi Msaidizi wa shamba la miti Mtibwa, Karimo Mangachi amesema ndani ya siku nne tayari wameshakamata ng’ombe karibu 900 katika eneo la ndani ya kama kilomita tatu hivi kuzunguka kambi hii.

“Tangu Januari hadi leo kumekuwa na matukio ya kuvamiwa zaidi ya kumi kwa changamoto hii imekuwa ni tishio kwa wenzetu tuliowapa jukumu la ulinzi ambao ni Suma JKT wanaonekana kuzidiwa nguvu kwa misingi.

Askari wakienda katika doria ya kawaida wanafanikiwa kukamata ng’ombe wale watu wametengeneza vikundi vya wahuni kuja kuvamia maeneo ya kambi.

“Mfano wiki mbili zilizopita walikamatwa mifugo kama miambili waliletwa kwenye zizi saa tatu usiku iliingia timu kubwa na kuharasi maeneo ya kambi kwa lengo la kupora mifugo iliyokamatwa,” anasema Mangachi.

“Sasa wakija hapa wanaingia hadi ndani wanavunja milango, madirisha waliingia na kuiba vifaa vya kijeshi vya Suma JKT walichukua butu za kijeshi na baadhi ya kombati za kijeshi,” alisema Mangachi na kuongeza kuwa.

“Siku iliyofuatia walileta ng’ombe hadi ndani ya eneo la kilometa moja kutoka kambi, Jeshi lilifanikiwa kukamata ng’ombe 28 ila wale ng’ombe waliokamatwa majira ya saa nane mchana ilipofika saa 11 jioni kilikuja kikundi cha watu wahuni na silaha za jadi waliwashambulia askali waliokuwa eneo hii na kutoka na mifugo.”

“Mifugo ni mingi ndani ya hifadhi, tunaomba wizara ifanye mapitio ya sheria ili kuongeza faini na tozo kwa wafugaji wanaoingiza mifugo kwenye hifadhi,” alisema Mangachi

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini wa Mfuko wa Misitu Tanzania, Prof. Romanus Ishengoma alisema TFS ni Jeshi Usu kwa hiyo mna taratibu zenu za kulinda katika kukabiliana na tatizo hilo.

“Hili tatizo la mifugo yaliyomengi uhenda yapo nje ya Mfuko, tukiongea ulinzi upo chini ya TFS ni Jeshi Usu kwa hiyo mnataratibu zenu za kijeshi za kulinda, kuhusu faini ndogo lipo kwa mujibu wa kanuni, sheria na taratibu si mamlaka yetu, hata hivyo kwa kuelewa ukubwa wa tatizo basi yanapoletwa maombi tutayachakata kwa uwelewa huo,” alisema Prof Ishengoma.

Wakati Prof. Suzana Agustino alitaka kujua ni hatua gani zinachukuliwa wakati ng’ombe hao wanapokamatwa na wahusika wanapochelewa kuwagomboa.

Akijibu swali hilo Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Mtibwa, Abdallah Mchomvu alisema iwapo wahusika watachelewa basi ng’ombe hao watataifishwa kwa kufuata utaratibu na sheria zote.

Katibu Tawala wa Mfuko wa Misitu, Dkt Tuli Msuya aliwapongeza viongozi wa shamba hilo kwa jitihada zao kubwa za kupambana na changamoto hizo na kuwataka kuendelea kuitunza miti iliyopandwa katika eneo hilo.