Shamte wa Katani na wenzake washtakiwa kwa uhujumu uchumi

Mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte

Muktasari:

Mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga akikabiliwa na mashtaka matatu.

Tanga.  Mkurugenzi wa zamani wa kampuni ya Katani Limited, Salum Shamte amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Tanga akikabiliwa na mashtaka matatu.

Shamte amefikishwa mahakamani leo Alhamisi Oktoba 31, 2019 pamoja na wenzake,  Juma Shamte ambaye ni mkurugenzi wa sasa wa kampuni hiyo na mjumbe wa bodi ya Katani, Fatma Diwani.

Mashtaka yanayowakabili ni uhujumu uchumi, utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Sh1.14 bilioni kwa vyama vya msingi vya ushirika (Amcos).

Akisoma mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao mbele ya hakimu mkazi Desidery Kamugisha, wakili wa Serikali, Peter Maugo amesema kati ya Januari 2008 na Agosti 2018 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Tanga na Mkoa wa Tanga, walikula njama kutekeleza mpango wa uhalifu.

Maugo aliyekuwa pamoja na wakili wa Takukuru,

Barry Galinoma  na Winlucky Mangowi wa ofisi ya mwendesha mashtaka wa Serikali,  amesema shtaka la pili ni kusababisha hasara katika vyama vitano vya Amcos kiasi cha Sh1.14.bilioni  na shtaka la tatu ni utakatishaji fedha wa Sh1.14 bilioni.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo waliitakiwa kutojibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Mawakili wa Serikali wamesema upelelezi wa kesi hiyo iliyoahirishwa hadi Novemba 13, 2019 haujakamilika, washtakiwa kurudishwa rumande.

Oktoba 25, 2019 Taasisi ya Sekta Binafsi (TPSF) ilimteua Angelina Ngalula kuwa kaimu mwenyekiti wa taasisi hiyo wakati taratibu za kisheria zikiendelea kufanyika dhidi ya mwenyekiti wake, Salum Shamte ambaye siku hiyo alikuwa amefikisha takribani siku 10 polisi.

Shamte alikamatwa mkoani Tanga wiki iliyopita kwa tuhuma za kuhusika kwenye upotevu wa Sh54 bilioni zikiwemo fedha za Serikali kupitia kampuni ya Katani Limited ambayo inadaiwa ana maslahi nayo.