Shehena ya mbao yanaswa Mwanza

Muktasari:

Ni katika msako unaoendeshwa na Wakala wa Misitu nchin (TFS

Mwanza. Wakala wa Mistu nchini (TFS) mkoani hapa imekamata mbao 995 zenye thamani ya Sh15 milioni zilizokuwa zinamilikiwa kinyume na sheria ya misitu namba 14 ya mwaka 2002.

Ofisa Mistu Mkoa wa Mwanza, Emmanuel Mgimwa alisema mbao hizo zilikamatwa wakati wa msako uliofanyika Februari 4, mwaka huu katika eneo la biashara la mfanyabiashara, mkazi wa Igoma.

Inadaiwa kuwa mfanyabiashara huyo ambaye anashikiliwa na polisi pia alibainika kuwa na maeneo mengine matatu ya kuuza mazao ya misitu ambayo hayajagongwa mihuri maalumu ya nyundo inayogongwa na TFS kinyume na sheria.

Akizungumzia tukio hilo, Kaimu Meneja wa Mistu mkoani humo, Hamza Omari alisema ofisi yake imeanzisha utaratibu wa kuendesha operesheni maalumu ya ukaguzi katika maeneo ya biashara ya bidhaa za misitu kutokana na baadhi ya wafanyabiashara wa mbao kuingiza usiku kukwepa ukaguzi.

Alisema baadhi ya bidhaa hizo uingizwa kupitia njia za panya usiku kupitia vivuko vya Ziwa Victoria.