Sheikh Ponda ahoji mauaji ya watu mkoani Pwani

Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda

Muktasari:

  • Sheikh Ponda alisema endapo mfumo wa nchi katika Mahakama, Bunge na Serikali una upungufu, busara ni kuuboresha na siyo kuuhama na kuanzisha utaratibu mwingine kinyemela.

Dar es Salaam. Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Sheikh Ponda Issa Ponda ameitaka Serikali kutoa tamko litakalofafanua sababu inayochangia watu kuuawa bila ya kufikishwa mahakamani huku akionyesha masikitiko yake juu ya mauaji ya Salum Mohamed Almasi,eneo la Kurasini jijini Dar es Salaam juzi

Sheikh Ponda alisema endapo mfumo wa nchi katika Mahakama, Bunge na Serikali una upungufu, busara ni kuuboresha na siyo kuuhama na kuanzisha utaratibu mwingine kinyemela.

Sheikh Ponda alitoa kauli hiyo jana kupitia barua yake aliyoithibitisha katika gazeti hili, kwamba, amemwandikia Waziri wa Mambo ya Ndani, Mwigulu Nchemba ,akihitaji kauli ya serikali juu ya mauaji yaliyofikia idadi ya watu 29 mkoani Pwani.

“Barua tulimtumia jana(juzi), kwa njia ya mtandao na akajibu kwamba, ameshaipokea na ameisoma. Sisi tunataka kuisaidia Serikali na Taifa kurejea katika hali nzuri, ninaamini kabisa Jeshi la Polisi likitumia wananchi linaweza kupata taarifa sahihi,”amesema huku akiishauri Serikali kufuata mfumo sahihi katika kushughulikia matukio ya uhalifu nchini.

Waziri Mwigulu alipopatikana kwa njia ya simu alijibu kwa ujumbe mfupi wa maneno akisema asingeweza kuzungumza kwa kuwa alikuwa katika vikao vya Bunge vinavyoendelea mjini Dodoma.