Sheria ya uchawi yawagawa wanasheria

Muktasari:

Wanasheria nchini wamegawanyika kuhusu ulazima wa Tanzania kuendelea kuwa na sheria ya uchawi au la.

Dar es Salaam. Wanasheria nchini wamegawanyika kuhusu ulazima wa Tanzania kuendelea kuwa na sheria ya uchawi au la.

Wakati wengine wakidai sheria hiyo haihitajiki katika zama hizi za sayansi na teknolojia, wengine wametaka iendelee kuwepo ili kudhibiti imani za kishirikina na kupunguza madhara yake.

Katika miaka ya hivi karibuni, Tanzania imeshuhudia ongezeko la mauaji au uharibifu wa mali uliosababishwa na tuhumiana kwa uchawi.

Kwa mfano, Machi mwaka huu, wanawake watatu waliuawa kwa kuchomwa moto katika Kijiji cha Kisharita kilichopo wilayani Iramba Mkoa wa Singida baada ya kuwatuhumu kumuua Agnes Msengil, kwa ushirikina.

Miezi miwili kabla, mkazi wa Kijiji cha Mtisi cha Halmashauri ya Nshimbo aliuawa na wanchi waliomtuhumu kutengeneza radi iliyompiga na kumuua mwanakijiji mwenzao, Angelina Revocati (16).

Takwimu za Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) zinaonyesha watu 3,180 waliuawa kati ya mwaka 2012 na 2021 kutokana na imani za kishirikina.

Hii ni wastani wa watu 31 kuuawa Tanzania kila mwezi kutokana na imani za kishirikina.

Matukio kama haya yamekithiri karibu kila kona ya Tanzania na sheria ya uchawi ipo, inayonaweza kukufunga jela.

Hivi karibuni Mahakama Kuu ilitengua kifungo cha miaka mitano alichohukumiwa Severini Charles, mkazi wa Njombe kwa madai ya kumroga ukichaa mtoto wa kaka yake hivyo kuibua maswali mengi.

Moja ya swali ambalo wengi wanajiuliza ni; je, Tanzania ina sheria ya uchawi? Na kama ipo, ina maanisha Serikali inaamini uchawi? Je, ushahidi wa kesi za uchawi unathibitishwaje?

Ukweli ni kwamba Tanzania inayo Sheria ya Uchawi (Witchcraft Act) ambayo ni Sura ya 18 ya Sheria za Tanzania zilizofanyiwa mapitio mwaka 2002.

Kifungu cha 3 cha Sheria ya Uchawi kinatamka kuwa mtu yeyote ambaye kwa kauli au matendo yake akibainika kuwa na nguvu za kichawi, au anamiliki zana za kichawi, au anasambaza zana hizo, au anashauri watu kutumia uchawi au kutishia kutumia uchawi dhidi ya mtu yeyote au vitu, atakuwa ametenda kosa la jinai.

Kifungu cha 5 (1) (a) cha sheria hiyo pia kinatamka kuwa mtu yeyote anayetenda kosa la uchawi kwa lengo la kusababisha kifo, ugonjwa, majeraha au madhila kwa jamii yeyote au mnyama anastahili kifungo kisichopungua miaka saba akitiwa hatiani.

Sheria ya Uchawi ilitungwa wakati wa utawala wa wakoloni baada ya kukuta jamii nyingi za Kiafrika zinaamini nguvu ya uchawi hata katika kupambana nao.

Sheria ya Kudhibiti Uchawi (Witchcraft Suppression Act) inampa mamlaka mkuu wa wilaya, mkuu wa mkoa au Rais kumpeleka uhamishoni mtuhumiwa wa uchawi atakayethibitika.


Wanasheria wagawanyika

Wanasheria waliotoa maoni kuhusu Sheria ya Uchawi wamegawanyika kuhusu haja ya kuwa au kutokuwa na sheria hiyo nchini.

Mkurugenzi wa Utetezi na Maboresho wa LHRC, Fulgence Massawe anasema Tanzania haihitaji kuwa na Sheria ya Uchawi kwani ni kandamizi iliyotungwa na wakoloni kwa maslahi yao.

“Hii ni sheria ya hisia si uhalisia. Haitakiwi wala hatutakiwi kuwa nayo kwenye dunia ya sayansi na teknolojia iliyostaarabika,” anasema Massawe.

Massawe anasema sheria hiyo ilitungwa na wakoloni ili kupambana na watu waliokuwa wanatumia imani za kishirikina kuupinga utawala wao.

“Kuthibitisha uchawi kisheria ni vigumu sana labda na wewe uwe mchawi. Unajua kipimo cha kuthibitisha kosa kwenye jinai lazima kiwe beyond reasonable doubt (bila kuacha mashaka),” alisema.

Sheria ya Uchawi ni moja kati ya sheria 40 ambazo tume ya Rais iliyoongozwa na Jaji Francis Nyalali iliiainisha kuwa kandamizi na kupendekeza ifutwe.

Katika mapendekezo yake, Jaji Nyalali alisema “…Sheria hiyo ni ya zamani tangu enzi ya wakoloni na imeendelea kuwepo hadi leo. Sheria hiyo haina maana, inatakiwa iondolewe.”

Hata hivyo, mapendekezo ya Jaji Nyalali yalipingwa na Tume ya Marekebisho ya Katiba ikisema imani na vitendo vya uchawi vimeleta hofu na vitisho vilivyochochea kutoelewana na chuki katika jamii.

Tume hiyo ilisema kuwapo kwa sheria hiyo ni muhimu ili kupambana na matokeo ya imani za kichawi.

Licha ya kuwapo kwa sheria hiyo, vitendo vya kichawi na matukio yanayohusishwa na imani za kishirikiana yameendelea kuongezeka nchini na kuwafanya wasioamini kuona haifanyi kazi.

Aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Francis Stolla anasema Tanzania inahitaji kuwa na Sheria ya Uchawi ili kudhibiti kukua kwa imani hizo.

“Tunahitaji kuwa na Witchcraft Act. Unajua dhana yake haieleweki, watu wanadhani dola inaamini katika uchawi kumbe haiamini bali imetunga sheria kukomesha na kuadhibu vitu vinavyotokana na imani ya wananchi kwenye uchawi.

“Imani za kichawi zinasababisha madhara makubwa hadi vifo, kwa hiyo sheria imewekwa kuzuia vitendo vya kichawi pamoja na vifaa vinavyotumika,” anasema Stola.

Stola alisema kwenye falsafa ya kutunga sheria huwezi kuitunga bila kuwa na sababu akikumbusha kuwa wakati wa uhujumu uchumi “tuliweka sheria ya kupambana na watu waliokuwa wanaficha hata kilo moja ya sukari, sabuni au mafuta. Sababu ya kutunga hiyo sheria ilikuwepo lakini leo haipo kwa sababu hakuna anayeficha sukari uvunguni tena.”

Hata hivyo, alisema sheria ya kudhibiti uchawi inahitajika kwa sababu watu wengi wanaamini mambo hayo hata mauaji wa albino yanaelezwa kutokana na imani za kishirikina kwa hiyo sheria imejielekeza kupambana na imani za uchawi na si uchawi kama wengi wanavyoamini.

Mwanasheria mwandamizi, Dk Rugemeleza Nshalla anasema hakuna sababu ya kuiondoa Sheria ya Uchawi isipokuwa inahitaji maboresho ili iendane na wakati.

“Maadam kuna hilo tatizo la imani potofu lazima kuwe na namna ya kupambana na hilo tatizo,” anasema.

Dk Nshalla anaamini jitihada pekee inayoweza kusaidia kuondoa tatizo la imani potofu hasa za uchawi ni kuwaingiza wataalamu wa ustawi wa jamii, viongozi wa dini ambao anasema wana utaalamu unaoweza kutumiwa kupambana na imani hizo.