Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Shigella: Maofisa masuhuli acheni ‘ubosi’ tekelezeni maagizo

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewataka maofisa hao kuhakikisha promosheni zinakwenda sambamba na mabadiliko ya mishahara na uainishaji mpya wa kada.

Geita. Mkuu wa Mkoa wa Geita, Martin Shigella amewataka maofisa masuhuli, utumishi kuacha tabia ya kujiona mabosi na badala yake kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Rais kuhusu upandishaji wa madaraja kwa watumishi wa umma.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa Programu ya Mwalimu Spesho iliyoandaliwa na Benki ya NMB na kuwashirikisha walimu zaidi ya 300 wa Wilaya ya Geita.

 Shigella amesema ipo tabia ya maofisa utumishi kutotekeleza maagizo yanayotolewa bila sababu.

Shigella amewataka maofisa hao kuhakikisha promosheni zinakwenda sambamba na mabadiliko ya mishahara na uainishaji mpya wa kada.

Kutokana na hilo Shigella amemtaka katibu tawala mkoa kusimamia na kuhakikisha kila mtumishi mwenye sifa anapewa haki yake.

"Rais alishatoa agizo. Hapa Geita watumishi zaidi ya 9,000 tayari wamepandishwa madaraja, tunataka kuona maofisa utumishi mnatekeleza watumishi wote wenye sifa ya kubadilishiwa kada, kupanda madaraja wahudumiwe na iende sambamba na mabadiliko ya mishahara,” amesema Shigella.

Akizungumzia programu hiyo, Shigella amesema imesaidia walimu wengi kuachana na mikopo umiza baada ya kupata elimu kuhusu uwekezaji na namna ya kuweka akiba.

"Zamani walimu walikuwa wakikimbia hadi maeneo yao kwa sababu ya mikopo yenye riba kubwa. “Leo hii tunashuhudia walimu wakipata mikopo ya nyumba, wakijenga makazi yao na sasa wana miradi ya kujikwamua kiuchumi. Hii ni hatua kubwa," amesema Shigella.

Kwa upande wake, Meneja wa Kanda ya Ziwa wa NMB, Faraja Ng’ingo amesema benki hiyo imewakutanisha walimu 300 kwa lengo la kuwapa elimu ya fedha na kuwa mabalozi wa kuwaelimisha wenzao kuhusu fursa zinazopatikana kupitia programu hiyo.

"Lengo letu ni kufahamu changamoto wanazopitia walimu na kushirikiana kuzitatua. Tunawataka walimu kuchangamkia fursa hizi ili ziwe kichocheo cha maendeleo yao ya kiuchumi," amesema Ng’ingo.

Baadhi ya walimu walioshiriki programu hiyo wamesema imewasaidia kwa kiasi kikubwa kujiimarisha kiuchumi na kuondokana na utegemezi wa mikopo yenye masharti magumu.

Swalala David amesema kupitia mfumo wa kidijitali, unawasaidia walimu kupata mikopo chapchapu na kuwasaidia kuachana na mikopo umiza ambayo iliwafanya wakimbie maeneo yao kwa kuogopa kukamatwa.

“Zamani tulikuwa hata darasani hatuwezi kufundisha maana ukikopa ukiwa hujarudisha kwa wakati wanakuja hadi shuleni kukukamata ili usikamatwe inabidi ukimbie kujificha, ilikuwa ni mateso lakini sasa tuna sehemu sahihi ya kupata mikopo,” amesema Constansia Method.