Shinyanga kuchanja watoto 132,389 dhidi ya polio

Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko
Muktasari:
- DC Mboneko amesema malengo yao ni kuwafikia walengwa 88,376 kwa Halmashauri ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga ni 44,013.
Shinyanga. Wazazi na walezi wenye watoto wenye umri chini ya miaka mitano wametakiwa kuwapeleka kupatiwa chanjo ya kuzuia ugonjwa wa polio ili kujikinga na ugonjwa wa kupooza, ulemavu hadi kifo.
Licha ya wazazi hao pia viongozi wa dini na viongozi wote kuanzia mitaa vitongoji na kata wametakiwa kuhamasisha na kutoa elimu kwa wananchi ili wawe na uelewa wa chanjo hiyo.
Agizo hilo limetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko leo Agosti 31 kwenye kikao cha kamati ya afya Wilaya ya Shinyanga, akisema wamejipanga kikamilifu kufanikisha Kampeni ya chanjo ya Polio awamu ya tatu inayoanza Septemba 1 hadi 4, 2022.
“Malengo yetu tuliyojiwekea ya walengwa 88,376 kwa Halmashauri ya Shinyanga na Manispaa ya Shinyanga ni 44,013 naomba isipungue, tuone namba imeongezeka,” amesema Mboneko.
Kwa upande wake afisa Mipango wa Taifa wa Chanjo kutoka Wizara ya Afya, Immaculate Dotto amesema lengo la kampeni hiyo awamu ya tatu ni kukinga watoto walio chini ya miaka mitano ili wasipatwe na virusi vya ugonjwa huo, ambao unaambukizwa kwa njia ya vinyesi vinavyozagaa ovyo.
"Ili tufanikishe lengo hili ni vizuri kila kiongozi mtendaji aelimishe jamii na kuwaeleza faida za chanjo ya polio, itakayofanyika kwa siku nne kuanzia Septemba 1 hadi 4, 2022.
“Ugonjwa huu unasababishwa na virusi vya polio vinavyosababisha kupooza na kusababisha ulemavu hatimaye kifo kabisa, kwani virusi hivi huingia mwilini kwa njia ya mdomo, kwa kunywa maji au chakula kilichochafuliwa na kinyesi kutoka kwa mtu aliyeambukizwa virusi na hauna tiba,” amesema.
Naye Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Getruda Gisema na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Shinyanga, David Rwazo wamesema wamejipanga vizuri kuhakikisha wanafanikisha vizuri kampeni hiyo ikiwa ni pamoja na kuwa na takwimu sahihi.
Kaimu Ofisa chanjo Wilaya ya Shinyanga, Said Mankiligo amesema uzinduzi wa chanjo utafanyika katika Kijiji cha Nindo ambapo tayari wameshaanza kuhamasisha na manispaa utafanyika katika Zahanati ya Chamaguha Manispaa ya Shinyanga.