Shuhuda aeleza alivyoruka kitandani tetemeko pwani ya Pemba, Tanga

Muktasari:

  • Mashuhuda wanadai kuwa tetemeko hilo lilitokea majira ya saa kumi na mbili jioni na kudumu kwa sekunde zaidi ya tano.

Tanga. Taasisi ya Jiolojia nchini imethibisha kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Tanga na Pemba na kueleza kuwa hakuna taarifa ya kuwepo madhara, huku mashuhuda wakieleza jinsi walivyobaini mtikisiko.

Akiongea na Mwananchi kwa njia ya simu leo Alhamisi Februari 9, 2023  Mkuu wa Kitengo Majanga ya Asili (GST), Dk Gabriel Mbogoni amesema tetemeko lilitokea saa 12:32 jioni maeneo ya pwani ya Tanga na Pemba.

Amesema tetemeko la hilo la ardhi linakadiriwa kuwa na ukubwa wa Magnitude 4.7 kutoka kwenye vipimo vya Richa na limepiga katika  maeneo ya pwani ya Pemba na Tanga.

Ameongeza kuwa mpaka sasa hakuna madhara yoyote ambayo yameonekana au kuripotiwa, hivyo kuwataka wananchi ambao wapo maeneo hayo kuchukua tahadhari.

"Tunashauri kwamba mtu akisikia mtikisiko asitaharuki na kukimbia,kwani inaonyesha kuwa watu wanaotaharuki na kukimbia ndio hupata madhara zaidi, kwa kuwa mawimbi ya tetemeko la ardhi husafiri kwa kasi zaidi, kwani husafiri kilomita 13 kwa sekunde moja," amesema Dk Mbogoni.

Mkazi wa Segera, Handeni Success Miamba amesema wakati tetemeko hilo linatokea alikuwa ndani amelala na kushuhudia kitanda kikitingishika, ndio kutoka nje aone kuna nini na kubaini ni tetemeko la ardhi, ila kwa ambao limepita kama hujatulia huwezi kubaini.

Aidha mkazi wa Chuda Tanga mjini  Zawadi Masuo amesema ilibidi aruke kitandani baada ya kitanda kutikiswa wakati akichezea simu na baadaye kugundua ni tetemeko la ardhi.

"Nilikuwa juu ya kitanda saa 12 jioni nikaona natikiswa nikaruka chini nione kuna nini, baadaye nikagundua ni tetemeko la ardhi maana imechukua kama sekunde tano tu," amesema Zawadi.

Mwaka 2020  mwezi wa tatu na nane pia kulitokea tetemeko la ardhi katika baadhi ya maeneo ya Mkoa wa Dar es Salaam, Pwani, Morogoro, Arusha na Kilimanjaro na katika wilaya za Lushoto, Handeni na Tanga mjini usiku ambalo liliripotiwa kuwa na  ukubwa wa Richa 5.9.