Tetemeko latikisa baadhi ya maeneo Pwani ya Tanzania

Muktasari:

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kiwango cha 4.7 limetokea jana umbali wa kilomita 33 kutoka visiwani Pemba na kusikika katika baadhi ya miji nchi ya Tanzania na Kenya, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha.


Dar es Salaam. Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa kiwango cha 4.7 limetokea jana umbali wa kilomita 33 kutoka visiwani Pemba na kusikika katika baadhi ya miji nchi ya Tanzania na Kenya, Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) imethibitisha.

Mawimbi ya tetemeko hilo yamedaiwa kusikika jana Februari 8 majira ya saa 12:30 jioni, huku baadhi ya wakazi wa jiji la Tanga nao wakieleza kuwa walilihisi tetemeko hilo.

“Nilikuwa naoga, nikaona nyumba inatikisika kwa dakika kadhaa nilishtuka. Mpaka sasa nimepata taarifa wengi walilisikia lakini sijasikia madhara yoyote,” alisema Khadija Yusuph mkazi wa Tanga.

Tetemeko hilo linalodhaniwa kutokea katikati ya Bahari ya Hindi limekuja ikiwa ni siku mbili tangu tetemeko la ardhi la kipimo cha 7.8 kuathiri nchini Uturuki ambapo maelfu ya watu wamepoteza maisha yao na kujeruhiwa na majengo na miundombinu kadhaa kuharibiwa.

Akizungumza na Mwananchi leo Alhamisi Februari 9, 2023 Mjiolojia mwandamizi kutoka Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Gabriel Mbugoni amethibitisha kutokea kwa tetemeko hilo na kwamba bado wanaendelea kufuatilia iwapo kuna madhara yametokea.

“Ni kweli tetemeko limetokea lenye ukubwa wa kipimo cha 4.7. mpaka sasa bado hatujapata taarifa bado tunaendelea kufuatilia. Tetemeko hili limesikika Pemba, Tanga kwa hapa Tanzania na maeneo mengine jirani mara zote kuna kuwa na chanzo ambacho ni kimoja pekee lakini limekwenda mpaka Kenya,” amesema Mbugoni.