Shule ya Jitegemee na mkakati wa kuondoa sifuri

Thursday December 09 2021
jitegemeeepic
By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha wanafunzi wake hawapati daraja nne na sifuri Shule ya Sekondari Jitegemee imeweka mkakati wa kuhakikisha wanafunzi wanafaulu.

Uamuzi huo umekuja baada ya kiwango cha wanafunzi wanaopata daraja la nne na sifuri kuongezeka kwa miaka mitatu mfululizo.

Mkakati uliowekwa na shule hiyo ni ukarabati wa madarasa, ujenzi wa bweni lenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 80 pamoja na kuboresha miundombinu.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Tawi la Utawala la Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Brigedia Jenerali Hassan Mabena wakati akizindua bweni la wasichana leo Alhamisi Desemba 9, 2021

“Miaka ya nyuma shule hii ilikuwa miongoni mwa zile zinazotamba, hapa katikati ikatokea mdororo kidogo kwa maana ya matokeo kushuka lakini uongozi wa shule na JKT kukaa tumeona nini tunaweza kukabiliana na hali hiyo na ndiyo hatua zimeanza kuchukuliwa.” Amesema

Amesema shule hiyo kongwe inayomilikiwa na jeshi imekuwa na mwenendo wa kulegalega miaka mitatu iliyopita lakini jitihada kubwa zimefanyika kuhakikisha inakwenda vizuri na tayari mafanikio yameanza kuonekana kwa kupunguza idadi ya wanafunzi wanaopata darasa sifuri kwenye matokeo ya kidato cha nne.

Advertisement

Kwa upande wake Mkuu wa shule hiyo, Kanali Robert Kessy amesema katika kufanikisha mpango huo wa kuondoa daraja sifuri wameingia ushirikiano na shule nyingine zinazofanya vizuri kwa kufanya mitihani ya pamoja na kujifunza mbinu zinazowasaidia kufanya vizuri.

Hatua nyingine ni kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu pale wanapofanya vizuri kwenye mitihani ya mihula ili kuongeza hamasa ya kujituma zaidi ili kupata matokeo mazuri katika mitihani ya kitaifa.

Advertisement