Sikia ya mtoto aliyejifungua pacha waliotenganishwa

Muktasari:

  • Mtu kwao. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Amina Amos (17) mama wa pacha waliotenganishwa Julai mosi mwaka huu kurejea nyumbani baada ya kutoweka kwa takribani mwaka mmoja akiwa hajulikani alipo.

Dar es Salaam. Mtu kwao. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Amina Amos (17) mama wa pacha waliotenganishwa Julai mosi mwaka huu kurejea nyumbani baada ya kutoweka kwa takribani mwaka mmoja akiwa hajulikani alipo.

Amina alirejea nyumbani akiwa na ujauzito wa miezi mitano Mei mwaka jana, wakati huo akiwa umri wa miaka 16, huku familia yake ikiwa na walakini kukubali umri wa ujauzito huo kutokana na tumbo lake kuonekana kubwa katika umri mchanga wa mimba.

Amina aliyepitia mateso, kukataliwa na kukashifiwa, alieleza namna anavyopitia kipindi kigumu kutokana na mzazi mwenzake ambaye ni baba wa watoto hao kumtelekeza baada ya kujifungua watoto walioungana.

“Aliniambia kwao hawazaliwi mapacha na kwa kuwa wameungana hiyo ni laana. Tulikuwa na mawasiliano mazuri, ila nilipojifungua tu alipigiwa akaambiwa hakujibu kitu akakata simu. Baadaye nikimpigia kumuomba mahitaji ananifokea, hakuwahi kutoa ushirikiano wowote kwangu,” alimwelezea mzazi mwenzake huyo pasipo kutaja jina huku akitaja umri wake ni miaka 27.

Amina ambaye hakufanya mahojiano ya kina na gazeti hili kutokana na umri wake kuwa mdogo, mama yake Dorica Josiah (35) alizungumza kwa niaba ya binti yake kuelezea safari ya ujauzito huo na changamoto zilizojitokeza awali na baada ya binti yake kujifungua.

“Binti yangu alianza kubadilika alipokuwa kidato cha pili. Ghafla alianza kukataa shule, kutokana na kumshinikiza sana alitoroka nyumbani na kutokomea kusikojulikana,” alianza kuelezea Dorica.

Alisema wakati huo binti yake alikuwa akisoma katika Shule ya Sekondari Mwigwa iliyopo mkoani Simiyu.

“Nilikuwa sikai naye, aliacha shule na kwenda kukosikojulikana. Alirudi akiwa na mimba ya miezi mitano. Shughuli zangu za kiuchumi ninafanyia Kahama, hivyo alivyorejea nyumbani nilipigiwa simu na ndugu zangu nikafahamishwa ila walisema hili tumbo linaonekana kubwa sana kwa kuwa nilikuwa na hasira niliwaambia wamuangalie nikaendelea na shughuli zangu,” alieleza.

Dorica alikiri kwa kipindi chote cha ujauzito hakuwahi kumuona mtoto wake na alielezwa kuwa alikuwa anakwenda kliniki, lakini kwa kipindi chote alichokuwa anahudhuria hakuwahi kufanyiwa kipimo cha Utrasound.

“Nilipigiwa simu nakumbuka ilikuwa tarehe 29 nikaambiwa Amina anaumwa uchungu anatakiwa kupelekwa hospitali, nilizima simu sababu nilikuwa bado nina hasira.

“Niliwasha simu saa 7 mchana nikaambiwa anatakiwa afanyiwe upasuaji kwa kuwa njia yake ilikuwa ndogo, hivyo inahitajika hela ya upasuaji nikatuma Sh320,000 nikazima tena simu,” alisimulia.

Dorica alisema aliwasha simu saa 11 jioni akaona meseji kwamba binti yake amejifungua pacha ambao wameungana. “Nilishtuka nikauliza kila kitu kuhusu mikono yao, miguu, vichwa na viungo vingine wakasema vipo sawa ila kitovu wanacho kimoja,” alieleza.

Alisema licha ya mshtuko huo aliwaomba wawafiche watoto hao, ili kutoleta taharuki na kutozingirwa na watu wakiwashangaa.

Alisema wakati akifanya mawasiliano hayo yote, kuna baba alikuwa pembeni yake alimsikia, alipomuuliza alimweleza tatizo alilonalo akampa namba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Dorothy Gwajima ili awasiliane naye kwa msaada zaidi.

“Nikampigia simu hakupokea. Akaniambia tuma ujumbe nikajitambulisha na tatizo nililonalo sikujibiwa. Baadaye nilipokea ujumbe ukiwa na namba ya simu ya Dk Masenga wa Hospitali ya Kanda ya Ziwa, Bugando nikampigia na alijitambulisha kuwa yeye ni daktari wa watoto baada ya mazungumzo walimwamisha Amina kutoka Maswa kwenda Bugando,”alisema.Alfajiri ya siku inayofuata, alisema alipanda basi kwenda Mwanza mjini na baada ya kufika alikutana na hali ambayo ilimuumiza.

“Mwanangu nilivyomkuta alikuwa anatia huruma, mwili wake wote ulikuwa umevimba na umekua wa njano ana mabaka meusi hatamaniki. Yeye na watoto walikuwa na manjano. Amina alilia sana aliponiona nilitoa neno moja tu ‘mwanangu haya ndiyo uliyoyataka’,” alisema.

Mama huyo alisema kwa kipindi cha mwezi mmoja walichokaa hospitali ya Bugando, alitumia akiba yake yote kwa kuwa siku za mwanzo Amina aliumwa mara kwa mara, hali iliyomfanya awe na wakati mgumu kuwahudumia watoto.

Baada ya kuwasiliana na uongozi wa hospitali, alipewa watu wa ustawi wa jamii na walipomhoji alianza kupewa msaada ikiwemo chakula na mahitaji muhimu kwa ajili ya watoto.

“Siku moja Dk Masenga aliniita na kunitaarifu kuhusu safari kwamba inabidi niende Muhimbili, waliandaa tiketi ya ndege tukaongoza Dk Mariam. Tumekaa Muhimbili tangu Novemba mwaka jana tuliambiwa mpaka watoto waongezeke umri angalau wafikishe miezi sita na pia waongezeke uzito,” alisema.

Licha ya kuhitaji kwenda nyumbani, Mama Amina alielezwa kuwa watoto hao hawatakiwi kwenda nje ya hospitali kwa kuwa wanaweza kupata maambukizi. “Amina alipelekwa jengo la Magufuli na tangu hapo tulipata mahitaji yote na kazi kubwa ilikuwa kuwatunza watoto waongezeke uzito na pia umri usogee.”

Hakuhofia upasuaji

Dorica alisema wakati wajukuu zake wanatenganishwa walikuwa na umri wa miezi tisa, hivyo hakuwa na wasiwasi.

“Mwanzoni nilikuwa naogopa wasitenganishwe, Dk Zaitun akasema vipimo vinaonyesha inawezekana, tangu hapo sikuwa na wasiwasi.

“Siku ya upasuaji sikuwaza chochote kibaya, nilikuwa najishangaa kwanini niko hivi sikunyong’onyea wala kulia, niliamini Mungu ana makusudi kuamua watoto hawa wazaliwe hivyo huenda kuniunganisha na Amina sababu nilikuwa na hasira sana naye alipokataa shule na kuondoka nyumbani,” alisema.

Vitisho vya familia

Dorica alisema baadhi ya ndugu walizungumza maneno ya kashfa kutokana na hali hiyo.

“Nilikuwa napata kejeli na vitisho nilikotoka wakisema ni laana, mkosi wakisema ‘watoto gani wanazaliwa wanatazamana wanaulizana umekuja lini’ ndugu yangu Kabiza aliongea kwa hasira kwa kuwa mama alikodisha mashamba ya ekari tatu, akadhani amekodisha ili fedha zimsaidie mtoto wangu.”

Alisema maneno ya kashfa yametolewa pia na baba wa mtoto, “Sijui alipo huyu kijana, nilifanya mawasiliano na mama yake alinijibu vibaya kwamba katika familia yao hajawahi kuzaliwa mtoto au watoto walioungana.”

Dorica alisimulia akisema hata siku ambayo alimuona mwanaye amekosa raha huku akichati sana kwenye simu alichukua simu na kuona meseji alizotuma baba wa watoto akimkashifu, “Nilikutana na meseji wanabishana na yule mwanaume ananikashfu mimi, Amina anamwambia usimkashfu mama yangu.

Pamoja na hayo, Dorica aliomba msaada kwa Serikali na jamii kumwangalia kwa jicho la pili, kwani hana makazi na hajui akitoka hospitali atakwenda kuishi wapi kwa kuwa watoto hao wanahitaji msaada wa kuishi katika mazingira mazuri, ili wasipate maambukizi na baadaye waende shule.

Pacha hao--- Rehema na Neema walitenganishwa Julai mosi mwaka huu, upasuaji uliofanyika kwa ushirikiano kati ya wataalamu wa afya 31 kutoka Hospitali ya Muhimbili na Ireland wanaotokea Shirika la Operation Child Life.

Daktari bingwa wa upasuaji watoto kutoka Muhimbili, Zaituni Bokhari alisema ugumu ulikuwa katika kutenganisha ini ambalo liliungana na baadhi ya mishipa mikubwa ya ini.

“Ini ilikuwa changamoto kubwa, lakini pia ngozi inayofunika moyo ilikuwa imeungana na kufanya kitu kimoja. Ilibidi ngozi ifumuliwe, ili iweze kutenganishwa kwa ini na moyo pia.

“Tumefanikiwa kuwatenganisha na kila mtoto amebaki na ini lake na mishipa inayobaki kwenye ini wamebaki nayo kila mmoja,” alisema ndakari huyo na kuongeza kuwa baada ya upasuaji huo watoto hao watakaa chini ya uangalizi kwa zaidi ya mwezi mmoja.

Dk Zaituni alisema upasuaji huo umefanywa na madaktari bingwa wa upasuaji watoto wadogo wapatao 12.

“Madaktari wa usingizi sita, madaktari wa kutengeneza ngozi ‘plastic surgery’ wanne, madaktari ambao kazi yao kuangalia mfumo mzima wa watoto unakwenda vizuri wawili na wauguzi 6,” alisema.

Licha ya mafanikio hayo, Dk Zaitun alisema Tanzania imepata uzoefu na kujifunza mengi kutoka kwa madaktari hao wa Bahrain na Ireland na wameona changamoto kubwa kwa nchi ni ukosefu wa wabobezi katika upasuaji wa ini.

“Tumejifunza vitu vingi changamoto kubwa ni wabobezi upasuaji wa ini, ini la watoto hawa lilikuwa kama ni moja tunamshkuru Profesa ambaye ni daktari bingwa mtaalamu anayeshughulika na ini amesaidia kwa kiasi kikubwa kuokoa maisha ya hawa watoto, hii inatupa changamoto kupata utaalamu huo,” alisema.

Daktari bingwa mbobezi wa upasuaji wa ini kutoka nchini Bahrain, Profesa Martin Corbally alielezea changamoto iliyojitokeza wakati wa upasuaji hasa baada ya nyama ya kufunika kidonda kutotosheleza.

“Baada ya upasuaji kidonda kilikuwa kikubwa, changamoto ikawa kupata nyama ya kufunika eneo la kidonda ilionekana ile nyama isingeweza kutosha kufunika eneo la kidonda, lakini kwa kuwa walizaliwa na nyama kubwa chini ya kitovu kwa nje ilisaidia kwa kiasi kikubwa kufunika eneo lote la kidonda ambalo lilikuwa wazi kwa wote wawili,” alisema Profesa Corbally. Kabla ya upasuaji, watoto hao walichangia mshipa mmoja wa damu unaotoa damu kwenye ini kupeleka kwenye moyo.

Watoto hao walizaliwa kwa njia ya upasuaji katika Hospitali ya Wilaya ya Maswa Septemba 21, 2021 wakiwa na kilo 4.9 wote kwa pamoja.

Walipewa rufaa kwenda Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Ziwa Bugando na baadaye Hospitali ya Taifa Muhimbili Novemba 12, 2021 wakiwa na kilo saba. Sasa wana kilo 13.3.