Siku 34 za Dk Bashiru Ikulu

Siku 34 za Dk Bashiru Ikulu

Muktasari:

  • Siku 34 za Dk Bashiru Ally Ikulu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Dk Bashiru kuwa katibu mkuu kiongozi kwa siku 34 tu na unaweza kusema ni wa kwanza kushika wadhifa huo kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Tanzania.

Dar es Salaam. Siku 34 za Dk Bashiru Ally Ikulu. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Balozi Bashiru kuwa katibu mkuu kiongozi kwa siku 34 tu na unaweza kusema ni wa kwanza kushika wadhifa huo kwa muda mfupi zaidi katika historia ya Tanzania.

Jana Jumatano Machi 31, 2021 Rais Samia Suluhu Hassan alimteua Dk Bashiru kuwa mbunge na leo Alhamisi Aprili mosi, 2021 katibu mkuu huyo wa zamani wa CCM amekula kiapo bungeni.

Kiongozi mkuu huyo wa nchi alimteua Balozi Hussein Kattanga kuchukua nafasi ya Dk Bashiru.

Dk Bashiru aliteuliwa na Hayati John Magufuli kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Balozi John Kijazi aliyefariki Februari 17, 2021.

Kwa mujibu wa tovuti ya Serikali, katibu mkuu kiongozi wa kwanza baada ya Tanganyika kupata uhuru alikuwa Dunstan Omari aliyeitumikia nafasi hiyo kwa miaka miwili 1962 hadi 1964 akafuatiwa na Joseph Namata (1964-1967)

Wengine ni Dickson Nkembo (1967-1974), Timoth Apiyo (1974-1985), Balozi Paul Rupia (1985-1995), Marten Lumbanga (1995-2006), Philemon Luhanjo (2006-2011), Balozi Ombeni Sefue (2011-2016), Balozi John Kijazi (2016-2021) na Dk Bashiru aliyeapishwa Februari 26, 2021 na kuondolewa Aprili 31, 2021.