Simbachawene aagiza ukaguzi wateja baa, kumbi za starehe

Muktasari:

Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ameagiza wamiliki wa kumbi za starehe  nchini kuanza kuwakagua wateja wao ambao wanaingia kwenye kumbi hizo ili kujua kama wamebeba silaha.

Mufindi. Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene ameagiza wamiliki wa kumbi za starehe  nchini kuanza kuwakagua wateja wao ambao wanaingia kwenye kumbi hizo ili kujua kama wamebeba silaha.

Simbachawene ameyasema hayo leo Alhamisi Julai 22, 2021 wakati wa ziara yake Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa baada ya kutokea kwa tukio la mauaji kwa kutumia silaha yaliyotokea hivi karibuni mkoani Dar-es - Salaam.

Waziri huyo alisema kuwa wamiliki hao wanatakiwa kuanza kuwapekua wateja wao ili kupunguza matumizi mabaya ya silaha hapa nchini.

Simbachawene alifafunua kuwa mtu anayetakiwa kupewa silaha lazima aangaliwe uwezo wa akili yake kama ana kaoroso yoyote  katika ubongo wake wakati anakua hadi anafikia umri wa utu mzima.

"Kwa sasa imejitokeza vijana wanafiriki kumiliki silaha sawa na cheni ya dhahabu wanakuwa wanataka akifika sehemu kila mtu ajue kama yeye anamiliki silaha lakini mtu ambaye anatakiwa kumiliki silaha ni yule ambaye anakuwa na tishio la kiusalama  au anadhani kutokana na shughuli ambayo anaifanya  anahitaji kumiliki silaha," alifafanua Waziri huyo.

Pia alieleza kuwa adui yako hapaswi kujua kama unamiliki  ili akitaka kukudhuru ajue tu nawe uwezo  wa kujilinda  na kijikinga kwa kutumia kifaa hicho.

"Kwa sasa ni tofauti mtu anaenda baa anaonyesha silaha huo unaitwa ni ushamba  na ukiukwaji wa sheria  za umiliki wa silaha kutokana na hali hii niliagiza jeshi la polisi muda kama mwezi umepita  kazi kubwa sana inafanyika na ripoti yake ya awali imeletwa ofisini kwangu ya namna ya mianya ya umikikishaji wa silaha unavyofanyika," alisema kiongozi huo.