Simbachawene: Watakaoandaa fumanizi kukamatwa

Simbachawene aagiza Jeshi la Polisi kuwakamata watuhumiwa waliowashambulia wapenzi

Muktasari:

  • Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amekea tabia ya watu kukusanyana na kuvamia watu walioko kwenye faragha kwa kisingizio cha fumanizi akisema kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na utu na watakamatwa wakigundilika.


Dar es Salaam. Waziri wa Mambo ya Ndani George Simbachawene amekea tabia ya watu kukusanyana na kuvamia watu walioko kwenye faragha kwa kisingizio cha fumanizi akisema kufanya hivyo ni kinyume cha sheria na utu na watakamatwa wakigundilika.

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Agosti 6,2021 ambapo amesema baadhi ya watu wamejingea mazoea ya kuwavamia watu wenye uhusiano ya kimapenzi wakiwa kwenye faragha zao mahali wanapokuwa katika nyumba au hotelini.

“Tabia hii imeshamiri sasa kama ambavyo video nyingi zinarushwa rushwa mitandaoni, leo nitumie fursa hii kutoa msingi wa kisheria lakini kukemea tabia hii ambayo imeanza kuonekana inaota mizizi. Ni kinyume cha sheria kabisa kuwaingilia watu walio kwenye faragha,” alisema

“Wakati mwingine watu wanafanya hivyo kwa kisingizo kuwa wamefumania, hakuna fumanizi ambalo linaweza kupangwa na kikundi cha watu, wanawake na wanaume wanapanga kwenda kuwavamia na kuwaingilia uhuru wao waliopo faraghani, kitendo hicho ni kinyume cha sheria ,”

Amesema hata kama ni fumanizi litakuwa pale ambapo si jambo la kupangwa na huyo anayefumania awe na ndoa halali na cheti halali cha ndoa lakini sio kwa mtu ambaye ulikuwa naye tu “Huwezi kusema umemfumania hawala yako, mahusiano ya hawala ni ya kupita”.

Amesema tabia hiyo inakiuka misingi ya utawala bora, heshima na utu na hasa heshima ya wanawake kwakuwa wanaodhalilishwa sana katika hilo ni kina mama ambao walishakuwa na uhusiano na mwanaume fulani wakaachana akawa na mwingine halafu yule wa mwanzo anamfumania.

“Suala la kudhalilisha watu wako uchi wa mnyama na wanapata kipigo hilo haliwezi kukubalika katika nchi yetu, kwa nafasi yangu nachukua nafasi hii kuliagiza jeshi la polisi wahakikishe wanafuatilia matukio haya hususani hili linalozunguka kuanzia jana, wahakikishe wale wote waliohusika wanakamatwa,” amesema Simbachawene.