Simulizi Kesi ya Zombe:Ndugu watambua miili ya wafanyabiashara wa madini mochwari, polisi yawakamata

Saturday February 20 2021
zombepic
By James Magai

Askari wavamia mochwari wawakamata wanaotambua maiti Baada ya kupata taarifa za kuuawa kwa ndugu zao kutoka kwa rafiki yao Ngonyani wakiwa katika hoteli ya Bondeni, Magomeni, Dar es Salaam, Mchami (mchimba madini mwenza wa kina Jongo) na wenzake hawakutaka kupoteza muda.

Walianza safari ya kuelekea Muhimbili na walipofika waliingia sehemu ya mapokezi na kumuulizia mhudumu waliyemkuta hapo iwapo kulikuwa na maiti za watu waliokamatwa na Polisi zimeletwa..

Mhudumu alithibitisha kulikuwa na maiti za watu wanne zilizoletwa hapo na Polisi jana yake wakidaiwa kutoka Sinza, kisha akawaelekeza waingie mochwari kuzitambua.

Wote wanne waliingia na kuwatambua ndugu zao watatu. Hawakumtambua yule wa nne. Simanzi na huzuni kubwa vikawatawala. Wenzake Mchami walishindwa kujizuia na kuangua vilio.

kesi ya zombe pic

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam Abdallah Zombe akitoka Mahakama ya Rufaa jijini Dar es Salaam jana,mara baada ya notisi ya rufaa dhidi yake kugundulika ina mapungufu,kulia ni Wakili wake Richard Rweyongeza.Picha na Michael Jamson

Baada ya kuona miili ya kina Jongo, Mchami alimpigia simu mkewe, Jane kumpa taarifa. “Huku mambo ni mazito, lakini vumilia na usinipigie simu tena maana hawa ndugu zetu tayari ni marehemu,” alisema Mchami akimweleza mkewe kwa uchungu.

Advertisement

Baadaye yule mhudumu wa mochwari alichukua kalamu na karatasi akampatia Mchami ili awatambue ndugu zao kwa majina, kisha yeye akatoka kidogo.

Aliporudi yule mhudumu Mchami alimwomba mashuka ili awafunike. Walilazwa sakafuni wakiwa uchi. Alimweleza mhudumu kuwa watu wale hawakuwa majambazi kama ilivyoripotiwa na Polisi.

zombepicc

Aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Wilaya ya Kinondoni (OC-CID), Christopher Bageni, akitoka mahakama ya rufani mara baada ya kuhukumiwa kunyongwa baada ya kutiwa hatiani katika kesi ya mauaji ya wafanyabiashara wanne wa madini, jijni Dar es Salaam jana. Picha na Said Khamis

Kisha Mchami alianza kutaja jina la Mathias Lukombe. Ghafla walisikia mtu anagonga mlango wa mochwari. Wakati wakijiuliza ni nani, mara mlango ulifunguliwa kwa nguvu. Watu wawili

waliingia huku mmoja akiwa amevaa kofia ya soksi iliyofunika sura yake (kofia ya kininja). Hao walikuwa ni askari polisi. Baada ya Mchami kumaliza kutaja majina yote ya marehemu hao, askari wale walimtia mbaroni kwa madai kuwa naye ni jambazi kwa kuwa aliwafahamu marehemu wale.

Askari waliwakamata Mchami na wenzake. Wote wanne wakabebwa juu juu na kurushwa ndani ya gari lao aina ya Landrover. Kisha ilianza safari kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi, Dar es Salaam.

Zombe atamba kuua majambazi Katika kituo Kikuu cha Polisi, Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dar es Salaam, ACP Zombe alikuwa ameitisha mkutano na waandishi wa habari kwa ajili ya kutoa taarifa ya matukio mbalimbali ya uhalifu kama ilivyo ada.

Katika taarifa yake mbele ya wanahabari, ACP Zombe pamoja na matukio mengine ya siku hiyo, akatangaza kuwaua kwa majambazi wanne waliopora pesa za kampuni ya Bidco.

Alidai kuwa ‘majambazi’ hao waliuawa jana wakati wakirushiana risasi na askari polisi katika jitihada za kukimbia.

Kwa mujibu wa ACP Zombe watu hao aliowaita walipigwa risasi na polisi katika ukuta wa Posta eneo la Sinza, wakati wakijaribu kuruka ukuta huo ili wakimbie wasitiwe mbaroni.

Zombe alinukuliwa akisema: “Kabla ya uporaji wa pesa hizo za kampuni ya Bidco majambazi hao walivamia na kupora katika duka la sonara liitwalo Aljabir Jewellers linalomilikiwa na mfanyabiashara mwenye asili ya Asia, Jaffar Amir.

“Walifanya uhalifu huo katika duka hilo lililoko kwenye makutano ya mitaa ya Livingistone na Mkunguni, Kariakoo muda wa saa 6:00 mchana.

msitumwambepic

Baadhi ya waandishi wa habari ambao walifuatilia na kuripoti tukio hilo kwa karibu wakati kesi hiyo ilipokuwa ikiendelea kwenye Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. Pichaya Mtandao

“Baada ya kufika katika duka hilo walijifanya wateja wanaotaka kutengenezewa mkufu wa dhahabu, lakini mlinzi wa duka hilo, Adamu Ally, aliwazuia kuingia ndani.

“Jambazi mmoja aliomba kuingia ndani ili kuangalia vito na baada ya kuingia aliwaamuru watu wote waliokuwemo ndani humo kulala chini na ndipo wakafanya uporaji huo.

“Walifanikiwa kuiba fedha taslimu Sh300,000, saa mbili za mkononi, bastola moja pamoja na simu tatu za mkononi.

“Katika tukio hilo watu kadhaa walijeruhiwa, akiwemo mlinzi aliyejeruhiwa tumboni na majambazi waliokuwa wamebaki nje, wakati akiomba msaada kutoka kwa wananchi.

“Wengine waliojeruhiwa ni Rajabu Jadi, mlinzi katika duka lingine jirani la simu ambaye alijeruhiwa puani na mpita njia Francis Richard, aliyejeruhiwa mguuni.

“Adamu na Francis waliruhusiwa baada ya kutibiwa lakini Rajabu hali yake si nzuri na amelazwa katika chumba cha wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU).

“Askari walilipata gari lililotumiwa na majambazi hao katika tukio hilo, aina ya Toyota Cresta lenye rangi ya fedha likiwa na namba za usajili T352 AGS kwa mbele na kwa nyuma namba T957 AGX. “Askari walifanya upekuzi ndani ya gari hilo na kukuta nyaraka mbalimbali zikiwemo risiti ya mafuta na hati ya usajili wa namba mpya ya TRA.

Gari hilo linasadikiwa kuwa lilitokea Kenya kutokana na risiti hiyo ya mafuta ambayo inaonesha kwa walijaza mafuta katika kituo kimoja, Desemba 10, 2005, kwa malipo ya fedha za Kenya, kiasi cha Sh3,547.69, wakihudumiwa na mfanyakazi Patrick.

“Muda wa saa 11:30 jioni, polisi walifanya msako ambapo katika barabara ya Mandela waliona gari likienda kwa mwendo wa kasi ndipo wakaamua kulifuatilia.

“Walipofika eneo la tukio, walikuta gari hilo likiwa limeegeshwa maeneo karibu na Msikiti wa Palestina na kukuta wizi ukiwa umeshafanyika. Majambazi hao walipora Sh5 milioni za kampuni ya Bidco. Askari waliokota maganda matano ya SMG na ganda moja la risasi ya bastola,” alisema Zombe mbele ya waandishi wa habari.

Safari ya Mchami na wenzake waliotiwa mbaroni na askari polisi wakati wakitambua miili ya jamaa zao iliendelea kuelekea Kituo Kikuu cha Polisi.

Nini itakuwa hatma yao baada ya kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi baada ya kudaiwa ni sehemu ya ‘majambazi’ waliouawa? Endelea kufuatilia kesho ndani ya gazeti hili kufahamu zaidi.

Advertisement