Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Simulizi moto ulivyokatisha maisha ya bibi, wajukuu wawili

Muktasari:

  • Simanzi na vilio vimetawala Kijiji cha Mji Mwema, Usa River wilayani Arumeru baada ya bibi mwenye umri wa  miaka 85 na wajukuu zake wawili kupoteza maisha kwa kuteketea ndani ya nyumba.



Arusha. “Bibi kwa umri wake asingeweza kujiokoa. Kuna muda alikuwa anapiga kelele akisema, nisaidieni, muwaokoe hata wajukuu wangu, mimi nife, lakini moto ulikuwa mkubwa tukashindwa kuwaokoa.”

Hiyo ni sehemu ya simulizi ya Shedrack Antony, mkazi wa Kijiji cha Mjimwema, Kata ya Usa River, wilayani Arumeru, akizungumzia tukio la moto lililosababisha vifo vya watu watatu lililotokea alfajiri ya Jumanne, Aprili 28, 2026.

Moto huo ambao chanzo chake bado hakijajulikana, uliteketeza nyumba na kusababisha vifo vya Mkunde Efatha (85) na wajukuu zake wawili, Jackson Geofrey (26) na Lerato Shabani (11).

Akisimulia tukio hilo leo Jumatano Aprili 29, 2026, Antony amesema alfajiri  ya siku hiyo walisikia kelele za kuomba msaada, walipotoka nje walikuta moto mkubwa ukiwaka katika nyumba ya marehemu huyo aliyekuwa akiishi na wajukuu zake.

Bibi Mkunde Efatha (85), mkazi wa Kijiji cha Mjimwema, Usariver wilayani Arumeru aliyefariki dunia baada ya nyumba aliyokuwa akiishi na wajukuu zake wawili kuteketea kwa moto.

Amesema walijaribu kuwaamsha majirani na kushirikiana kuokoa maisha ya waliokuwa ndani, lakini juhudi hizo ziligonga mwamba kutokana na ukubwa wa moto na moshi mzito uliotanda ndani ya nyumba.

“Huyu mama ni jirani yangu. Ilikuwa saa 11 alfajiri tulisikia kelele za kuomba msaada. Tulipotoka nje tukakuta moto umeshika nyumba upande mmoja. Tukaanza kung’ang’ana kuvunja mlango ili kuwaokoa, lakini tulipofanikiwa kuuvunja, kulikuwa na moshi mwingi umetanda ndani,” amesema.

Antony amesema walijaribu kutafuta vitambaa vya kujifunga vyenye maji ili kuingia ndani kuwaokoa, lakini hali ilizidi kuwa mbaya baada ya umeme kuanza kutoa cheche, jambo lililowazuia kuendelea na jitihada hizo.

Antony amesema walizunguka upande wa nyuma wa nyumba wakijaribu kuvunja mlango wa jikoni, lakini walipoufikia, moto ulikuwa tayari umeenea na gesi kulipuka na kuwafanya kukimbia kuokoa maisha yao.

Jackson Geofrey (26) aliyefariki kwa ajali ya moto.

“Baada ya kusikia mlipuko wa gesi tulikimbia. Tayari tulishawasiliana na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, ambao walifika haraka pamoja na polisi. Walidhibiti moto, lakini tulipoingia ndani tulikuta wote wameshafariki dunia. Tulishindwa kuwaokoa, japokuwa walipiga kelele sana za kutuomba sisi majirani msaada, tulishindwa kuoka maisha yao, inaumiza sana,” amesimulia jirani huyo.

Antony amesema walipofika walisikia mmoja wa watoto hao akipiga kelele hukua akiita majirani akisema mdogo wake anashindwa kupumua kutokana na moshi mwingi.

“Alisema eneo walilokuwa lilikuwa limejaa moshi na akawa anasema bado moto haujafika,”amesema  Antony na kuongeza kuwa, kijana Jackson alionekana akijaribu kuvunja mlango ili kujinusuru, lakini alishindwa kutokana na moshi na alikutwa amefia mlangoni baada ya moto kuzimwa.

“Tukakuta maiti ya mtoto mwingine mdogo nje ya mlango, inaonekana alikuwa anataka kumfuata bibi yake chumbani. Bibi amekutwa ameungulia kitandani. Miili yao imeharibika vibaya. Ni tukio la kusikitisha sana,” amesema.

Mtoto wa marehemu, Neema Msuya amesema familia imepata pigo kubwa, akieleza kuwa binti yake Lerato alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba katika Shule ya Msingi Amani, huku Jackson akiwa mtoto wa kaka yake.

“Tunapitia wakati mgumu. Hili ni pigo kubwa kwetu, lakini tunaamini ni mapenzi ya Mungu. Tunaomba ushirikiano wa ndugu, jamaa na marafiki ili tuweze kukabiliana na msiba huu,” amesema.

Ameongeza kuwa mtoto huyo alikuwa kipenzi cha bibi yake, jambo lililomfanya abaki kuishi naye.

“Alikuwa anampenda sana bibi yake, ndiyo maana nilimuacha aendelee kuishi naye. Nilipanga kumchukua baada ya kumaliza darasa la saba,” amesema.

Mwanafamilia mwingine aliyezungumza na Mwananchi, Kitia Wilderson amesema kutokana na hali ya miili ilivyoathirika, familia imelazimika kupanga maziko ya haraka, yatakayofanyika Ijumaa, Mei mosi, 2026, katika eneo la Ugweno Msangeni.

Amesema kabla ya safari ya kwenda kuzika, kutakuwa na ibada fupi ya kuaga miili hiyo katika eneo la tukio na baadaye ibada ya maziko itafanyika Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Msangeni, wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro.

“Hata baada ya nyumba kuungua, tumeamua kuendelea na shughuli za msiba hapa hapa nyumbani. Tumejenga mahema na tutakaa hapa hadi siku ya maziko. Tunasikitika pia kuwapoteza vijana wetu. Tunaomba vyombo husika vifuatilie chanzo cha moto huu,” amesema.

Jirani mwingine, Rose Mwambo amesema marehemu Mkunde alikuwa mtu mwenye upendo kwa majirani na jamii kwa jumla.

“Alikuwa mtu wa watu, mwenye kujali. Hata akisikia tukio lolote, alikuwa wa kwanza kufika kusaidia. Nilikuwa naye Jumapili iliyopita, kifo chake kimeniumiza sana,” amesema.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Mjimwema, Dalton Lema amesema alipokea taarifa za tukio hilo alfajiri na alipofika alikuta juhudi za kudhibiti moto zikiendelea.

“Nilipofika, wananchi na zimamoto walikuwa tayari wanaendelea na juhudi za kuzima moto. Tulikumbana na changamoto ya umeme, lakini baadaye ulizimwa na wahusika na ndipo tukafanikiwa kudhibiti moto. Baada ya hapo, miili mitatu ilipatikana,” amesema.

Lerato Shaban (11)ambaye alikuwa mwanafunzi wa darasa la saba,aliyefariki katika ajali hiyo.

Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji Mkoa wa Arusha, Oswald Mwanjegele amesema chanzo cha moto huo bado hakijajulikana.

“Tulipokea taarifa ya tukio la moto katika eneo la Usa River kwenye nyumba ya Mkunde Kitio. Moto ulianza na kuenea haraka na dalili zinaonesha ulianzia sebuleni. Waliokuwa ndani walijikuta wamezingirwa na moto na kuanza kuomba msaada,” amesema.

Ameongeza kuwa majirani walijaribu kuuzima moto huo kabla ya kuwasiliana na kikosi cha zimamoto, ambacho kilifika na kufanikiwa kuudhibiti, ingawa maisha ya watu watatu yalikuwa tayari yamepotea.