Prime
Simulizi mwanafamilia aliyepotea akitoka msibani Bagamoyo
Muktasari:
- Safari ya kuhudhuria mazishi Bagamoyo yageuka fumbo la kutoweka kwa mwanaume wa Tanga, familia ikisalia na maswali yasiyo na majibu.
Tanga. “Tulivyomuambia kwamba mzigo wake tumeuacha, akatujibu kuwa basi hakuna neno, ataukuta…”
Kauli hiyo ya mwisho ndiyo imeendelea kugonga vichwa vya wanafamilia wa Rashed Mohamed, mwanaume mkulima kutoka Tanga, ambaye hadi leo hajulikani alipo baada ya safari ya mazishi iliyogeuka kuwa mwanzo wa kitendawili kizito.
Mdogo wake, Mohamed Salim, akianza kusimulia mkasa huo anasema familia yao ilipata taarifa za msiba wa mwanafamilia Desemba 3, 2026 katika kijiji cha Miono kilichopo Bagamoyo, Mkoa wa Pwani.
Anasema baada ya taarifa hiyo, siku iliyofuata ndugu na jamaa walikubaliana kuungana kuelekea mazishini. Miongoni mwao alikuwa Rashed Mohamed, ambaye sasa ndiye mhusika mkuu wa tukio hili la kutoweka, kaka yake mkubwa Joseph Salimu pamoja na yeye mwenyewe.
“Ndugu yangu anaishi Mapojoni, kata ya Kirare, na mimi naishi Amboni, Kata ya Mzizima jijini Tanga. Tulipokubaliana kwenda kuzika, yeye alitoka na pikipiki hadi Lusanga wilayani Muheza kwa ajili ya kuhifadhi pikipiki, kisha akapanda gari,” anasema Mohamed Salim.
“Yeye alitutangulia wakati sisi tukiwa nyuma yake na gari,” anasimulia Mohamed.
Safari yao ilianza kwa mawasiliano ya mara kwa mara kwa njia ya simu, kila mmoja akijulishana alipo njiani. Mohamed aliwasili mapema msibani na baada ya mazishi walipanga kurejea Tanga siku ya Ijumaa, Desemba 5.
Mohamed anasimulia kuwa siku hiyo walianza safari kutoka Miono hadi Kibao cha Mandela, Bagamoyo, Pwani, wakitafuta usafiri wa moja kwa moja kwenda Tanga, lakini walikumbana na changamoto kubwa ya usafiri kutokana na msongamano wa watu wakati wa Desemba.
“Tulikaa barabarani hadi muda ukaenda, tukashauriana kupanda gari lolote hata kama linaishia Mkata ili tupate usafiri mwingine wa kuunganisha hadi Tanga,” anasema.
Anasema hatimaye walipata gari lililokuwa linaelekea Mkata, licha ya kuwa limejaa kupita kiasi. Walifika Mkata majira ya saa 11 jioni kuelekea saa 12, wakashuka stendi kusubiri basi la Tanga. Hapo ndipo mambo yalipoanza kubadilika.
Kwa mujibu wa Mohamed Mohamed, kaka yake Rashed Mohamed alionekana kuwa na hamu ya kwenda Korogwe kuangalia shamba lake la mihogo. Hata hivyo, kabla ya kufanya uamuzi huo, aliondoka kwenda msalani.
Anasema wakati huo, ghafla gari la mizigo lililokuwa linaelekea kiwanda cha saruji cha Tanga Rhino lilipita, na kutokana na ugumu wa usafiri waliamua kupanda. Walipokuwa njiani, walimpigia simu Mohamed kumjulisha wameondoka.
“Alituuliza, ‘Nilikuwa nimeacha kimfuko changu pale tulipokuwa tumekaa, mmeondoka nacho?’ Tukamjibu tumekiacha hapo hapo. Tulivyomuambia hivyo, akasema hakuna neno, ataukuta. Hiyo ndiyo ilikuwa mara ya mwisho kuwasiliana naye,” anasimulia Mohamed.
Akisimulia zaidi, Mohamed anasema walifika Rhino na kurejea nyumbani wakiamini kuwa ndugu yao angefuata nyuma. Lakini siku zikapita Ijumaa, Jumamosi, Jumapili bila taarifa yoyote, na wasiwasi ukaanza kuongezeka pale mke wake alipopigiwa simu na rafiki wa Rashed kutoka Korogwe.
Kwenye simu hiyo, rafiki huyo alisema:
“Shemeji vipi, kaka ana matatizo gani? Aliwasiliana na mimi akadai anakuja huku lakini hajafika. Baadaye akanipigia akisema hataweza kuja kwa kuwa jua lilikuwa limechwa, akaahirisha, akaniahidi kunitumia hela ya shamba, lakini sasa hapokei simu.”
Anasema kauli hiyo ilizua taharuki, familia ikaanza kujiuliza kama hakufika Korogwe wala nyumbani Mapojoni, ameishia wapi?
Jitihada za kumtafuta zilianza siku ya Jumatatu, wakirejea Mkata mahali walipoachana naye. Walitafuta mfuko wake lakini haukuonekana. Pia, walifika hospitali wakihofia huenda alipata ajali, lakini hakuna taarifa yoyote iliyopatikana.
Mama mzazi wa Mohamed, Mwanaidi Husein, anasema kupotea kwa mwanawe ni pigo kubwa kwa familia.
“Alikuwa akinipigia simu mara kwa mara na kunipatia mahitaji. Mimi sasa ni mtu wa kutunzwa kutokana na umri wangu. Hatujui nini kimemkuta, tunaomba serikali itusaidie kumpata au hata kujua kama amekufa,” anasema kwa uchungu.
Anaeleza kuwa mwanawe alikuwa mkulima wa ufuta, hoho na mkonge na alikuwa tegemeo kubwa la familia na kupotea kwake kumeacha pengo lisilozibika.
“Mwanangu hana ukorofi wowote. Analima mihogo na mahindi Kwasunga, Handeni, na alikuwa akituletea mazao. Kutokumuona kumetuchanganya sana,” anaongeza.
Mama huyo pia anaibua wasiwasi kuhusu baadhi ya marafiki wa mwanawe, akihisi huenda wanajua zaidi ya wanavyosema.
“Vyombo vya uchunguzi viwaanze na marafiki zake wa karibu. Kuna mmoja aliwahi kukaa kwake mwezi mzima, lakini ameonekana shambani kwake bila hata kufika nyumbani kusalimia au kuulizia,” anasema.
Kwa upande wake, mke wa Mohamed, Tukae Mohamed, anasema mara ya mwisho kuwasiliana na mumewe ilikuwa usiku wa siku aliyoondoka. Baada ya hapo alikaa siku tatu bila taarifa hadi alipopigiwa simu na rafiki huyo kutoka Korogwe.
“Nilishtuka sana. Ilibidi niazime simu kwa jirani kumpigia, lakini hakupatikana. Ndipo nikaanza kutoa taarifa kwa ndugu, jamaa na vyombo vya dola,” anasema.
Anaongeza kuwa ana mashaka na mienendo ya rafiki huyo:
“Yeye ndiye wa kwanza kuniambia mume wangu hapatikani, lakini haoneshi ushirikiano. Alienda hadi shambani anapolima mume wangu alifuata nini kama si yeye mwenye kujua kitu?”
Tukae anasema tukio hilo limeiacha familia katika hali ngumu, kwani alikuwa kichwa cha familia.
“Naomba serikali na jamii kwa ujumla itusaidie kumpata mume wangu akiwa hai au amekufa, tupate kujua ukweli,” anasisitiza.
Mwenyekiti wa mtaa alipokuwa anaishi Mohamed na familia yake Mapojoni, jijini Tanga, Rajab Mbelwa, amekiri ofisi yake kuwa na taarifa za kupotea kwa mtu huyo na kwamba jitihada zinaendelea za kumtafuta.
Mwenyekiti huyo anasema anamtambua kama mkazi wake ambaye hakuwa na historia ya aina yoyote ya uhalifu, na alikuwa amejikita kwenye kilimo cha mihogo na biashara ya kuuza vinywaji.
“Ofisi yangu haina taarifa zozote kuwa Mohamed alikuwa na changamoto au matukio yoyote. Kupotea kwake kwa kweli kumetusikitisha sana, na tunaomba vyombo vya dola kuchunguza kwa kina kilichotokea na hatua zaidi kuchukuliwa,” anasema Mwenyekiti wa mtaa wa Mapojoni, jijini Tanga.
Akizungumzia tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga (RPC), Almachius Mchunguzi, amesema uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kwa lengo la kubaini chanzo cha kupotea Mohamed.
Hadi sasa, hatima ya Mohamed bado ni kitendawili kisichopatiwa majibu. Familia inaendelea kuishi kati ya matumaini na hofu, wakisubiri siku ambayo ukweli utawekwa wazi.