Simulizi tamu na chungu ya muosha magari

Wednesday April 07 2021
tamupic

Muosha magari, Robert Simba akiwa katika eneo lake la kazi lililopo Mabibo jijini Dar es Salaam. Picha na Elizabeth Edward

By Elizabeth Edward

Dar es Salaam. Uwanja wa wazi eneo la Mabibo External la kuegesha magari aina ya Coaster yanayokodishwa kubeba watu kwenye shughuli mbalimbali, kuna vijana wachache wanalitumia eneo hilo kuwa sehemu yao ya kupata mkate wao wa kila siku kwa kuosha magari.

Robert Simba ni mmoja wa vijana hawa ambaye amefanikiwa kuendesha familia yake kwa kutegemea kazi hiyo.Bila kujali kejeli za wateja, vijana wenzake na watu wanaomdharau, Simba ameifanya kazi hiyo kwa uaminifu kwa takribani miaka 10 na ndiye mwosha magari anayeaminika zaidi katika eneo hilo.

Simba ambaye elimu yake ni ya darasa la saba anaeleza alianza kazi hiyo baada ya kushindwa kwenye kazi za ujenzi ambazo zilimleta jijini Dar es Salaam. “Nyumbani kwetu ni Mdaula, nilikuja Dar kuna ndugu yangu ni fundi ujenzi, akaniambia nije kujiunga naye ili nimsaidie anapopata kazi, nilifanya kwa muda nikaona ni kazi ni ngumu na zilikuwa hazipatikani mara kwa mara,” Mwaka 2009 akaanza rasmi kuosha magari wakati huo akiosha gari moja kwa Sh1,000 hadi Sh2,000 kiwango ambacho kiliendelea hadi mwaka 2014. Wakati wengine wakilia hali mbaya miaka mitano iliyopita, kwake ilikuwa neema kwani kiwango cha kuosha magari kilipanda hadi Sh3,000 kwa magari madogo na coaster kuoshwa kwa Sh10,000.

Malipo haya humfanya kuingiza kati ya Sh30,000 hadi Sh50,000 kwa siku kiwango ambacho ukikokotoa kwa mwezi ni kati ya Sh900,000 hadi Sh1.5 milioni. Shughuli hiyo imemuwezesha kuendesha familia yake ikiwemo kumsomesha mtoto wake, kulipa kodi na kuhakikisha mahitaji yote ya familia yanapatikana. Kubwa zaidi amenunua kiwanja na ameanza ujenzi wa nyumba yake, ili kuondokana na adha ya nyumba za kupanga.

Pamoja na mafanikio hayo, Simba anaeleza kazi hiyo ina changamoto nyingi ambazo huwafanya wengi wanaofanya kuangukia mikononi mwa polisi. Anasema mteja kuacha gari aoshewe na baadae kurudi kudai ameibiwa fedha na vitu vya thamani kwenye gari ni miongoni mwa mambo wanayokutana nayo waosha magari.

“Uaminifu ni kitu cha muhimu zaidi kwenye kazi hii, kinyume na hapo unaweza kujikuta kila siku unapelekwa polisi. Nashukuru Mungu sijawahi kufikia hatua hiyo ila niliwahi kupata kisanga. “Wateja wangu wengi huwa wananiamini, wakati mwingine wanaacha magari na kuyafuata baadae, sasa siku moja kuna mteja kaacha gari nimeosha, alivyorudi nyumbani kwake usiku akasema haoni fedha zake aliweka chini ya kiti,” alisema.

Advertisement

Taarifa hiyo ilimpa hofu akitambua lazima ataingia kwenye misukosuko. Hata hivyo, mambo yalikuwa tofauti baada ya kuhojiwa ilionekana hausiki na akaachwa kuendelea na shughuli zake. Changamoto nyingine hukutana nayo ni kutolipwa fedha zao hasa na watu ambao huenda mara chache kwenye vijiwe vyao.

“Hii pia haijawahi kunitokea ila nashuhudia kwa wengine,” alisema.

Advertisement