Simulizi vifaa saidizi vikirejesha tabasamu ya wenye ulemavu Tanga
Mbunge wa viti Maalimu mkoa wa Tanga Mwanaisha Ulenge akishikana mkono mmoja wa watu wenye ulemavu wakati wa hafla ya kukabidhi vifaa saidiazi. Picha na Mbonea Herman
Muktasari:
- Msaada wa vifaa hivyo si tu umewafanya wenye ulemavu kufurahia maisha, bali pia utawawezesha kujihisi ni sehemu ya jamii na kuwapunguzia utegemezi katika kufanya baadhi ya mambo ambayo wangeweza kuyamudu wenyewe.
Tanga. Baada ya dhiki faraja. Katika maisha ya hapa duniani binadamu inakubidi ujiandae kwani lolote linaweza kutokea na kukufanya ama uwe na maisha yenye furaha au yenye majuto na shida, lakini muhimu ni kujipa moyo na kuwa tayari kuyakabiri.
Jana, watu wenye ulemavu ambao kwa muda wameishi kwenye shida na mahangaiko, wamerudishiwa tabasamu baada ya kupatiwa msaada wa viti mwendo vitakavyowasaidia kuzunguka katika maeneo mbalimbali na kufanya shughuli zao kama watu wengine.
Taasisi ya Ng’arisha Maisha kwa kushirikiana na Taasisi ya Kamal, imewagawaa vifaa saidizi vya aina mbalimbali vyenye thamani ya Sh170 milioni, vikijumuisha viti mwendo 31, miguu bandia 100 kwa wenye ulemavu wa viuongo na fimbo 25 kwa ajili ya wasioona.
Msaada huo si tu umewafanya wenye ulemavu hao kufurahia maisha, bali pia utawawezesha kujihisi ni sehemu ya jamii, achia mbali kuwapunguzia utegemezi katika kufanya baadhi ya mambo ambayo wangeweza kuyafanya wenyewe.
Mariam Siafu, msichana mwenye ulemavu, anasimulia kwamba maisha yake yalikuwa machungu kutokana na kukosa kiti mwendo, ambacho kingemwezesha kufanya baadhi ya mambo kama binadamu wengine.
Kwa miaka mingi, amekuwa akiishi maisha ambayo kila hatua ilikuwa mapambano. Alikuwa anakosa uhuru wa kuchangamana na watu wengine na hata kufanya shughuli zake za kawaida kama watu wengine.
Mmoja wa watu wenye mahitaji maalumu mara baada ya kupatiwa kitimwendo. Picha na Mbonea Herman
Kwa sasa amefanikiwa kupata kiti mwendo ambacho anasema atakitumia katika mizunguko yake na shughuli zake, jambo ambalo limekuwa ni ndoto yake kutokana na ugumu ambao amekuwa akikabiliana nao kutokana na tatizo alilonalo na ulemavu wa viungo na kiti mwendo cha awali.
Amesema kiti alichokuwa akikitegemea kilikuwa kimechakaa kiasi cha kufungwa kwa vitambaa ili kiendelee kutumika. Hakikuweza tena kumpeleka kwenye shughuli za kiuchumi, bali kilitosha kumfikisha tu msalani, tena kwa shida.
Kutokana na hali hiyo, alilazimika kuzunguka sehemu mbalimbali akiomba msaada wa kupata kiti kipya bila mafanikio. Amesema maisha ya kutegemea watu wengine yalimnyima uhuru, heshima na hata ujasiri wa kushiriki shughuli za kijamii.
“Nilikuwa natumia kiti kilichochakaa. Nilizunguka sehemu nyingi kuomba msaada lakini sikuweza kufanikiwa. Leo nimepata kiti kipya na najiona tena ni sehemu ya jamii. Sasa naweza kutoka nyumbani, kupanda gari na kufanya shughuli zangu bila kumtegemea mtu,” amesema Mariam.
Simulizi ya Mariam si ya kipekee miongoni mwa waliopata misaada hiyo. Anna Gabriel, mama wa mtoto wenye ulemavu, Abdul Rafael amesema changamoto haikuwa ya mwanawe pekee, bali na kwake pia, kwani kama mzazi amekuwa akimwangalia mtoto anavyoteseka kila siku kutokana na kutumia kiti mwendo kisichokuwa na uwezo wa kumbeba.
Amesema kila safari ya kwenda hospitalini, shuleni au kutembelea ndugu ilikuwa mateso kwa mtoto na familia nzima kutokana na uchakavu wa kiti alichokuwa akikitumia kwa miaka mingi.
“Tulikuwa tunaumia kumwona mtoto wetu akiteseka. Kiti alichokuwa anakitumia kilikuwa kimechakaa sana na hakikuwa salama tena. Leo tumepata kiti kipya ambacho kimeturudishia matumaini kuwa Abdul ataweza kuendelea na maisha yake kwa urahisi zaidi,” amesema mama huyo.
Si hao tu wanaosimulia mateso na mahangaiko ambayo yanaenda kuwa historia. Chidi Sarai naye ana simulizi yake, anasema kwa muda mrefu alijikuta akitegemea ndugu na majirani kila alipotaka kutoka nyumbani kwa sababu hakuwa na kiti mwendo kinachofaa kumsaidia.
Amesema hali hiyo ilimnyima nafasi ya kushiriki shughuli nyingi za maendeleo na kujiongezea kipato na wakati mwingine alilazimika kubaki nyumbani kwa sababu hakukuwa na mtu wa kumsukuma.
“Kiti hiki kimenipa uhuru ambao nilikuwa nimeupoteza kwa muda mrefu. Sasa ninaweza kwenda kufanya shughuli zangu na kushiriki maendeleo kama watu wengine bila kuwa mzigo kwa familia yangu,” amesema Chidi.
Simulizi hizo zinaakisi hali hali wanayokabiliana nayo watu wenye ulemavu, suala linaloungwa mkono na Subira Hozza, katibu wa Shirikisho la Vyama vya Watu wenye Ulemavu Mkoa wa Tanga (Shivyawata).
Hozza amesema watu wenye ulemavu wanashindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii kutokana na ukosefu wa vifaa saidizi, kama vilivyotolewa kwenye msaada huyo.
Amesema wengi hushindwa hata kuhudhuria mikutano ya maendeleo kwa sababu ya kukosa viti mwendo au vifaa vingine, huku wengine wakilazimika kubebwa, jambo linalowaondolea heshima na kuwafanya wasijiamini.
“Tunaomba wasamaria wema waendelee kujitokeza kutusaidia vifaa saidizi. Mwenye ulemavu anahitaji kufanya kazi, kutunza familia yake na kushiriki maendeleo kama mtu mwingine yeyote. Vifaa saidizi ndiyo vinavyompa uwezo huo,” amesema Subira.
Kutokana na umuhimu huo, hata hafla ya ugawaji msaada huo ilipewa kipaumbele na kuwakusanya watu mbalimbali, akiwemo Mbunge wa Viti Maalumu, Mwanaisha Ulenge ambaye amesema lengo la msaada huo ni kuacha alama katika maisha ya watu wenye ulemavu na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha makundi yenye mahitaji maalumu yanapata fursa sawa za kushiriki maendeleo.
“Ng’arisha Maisha imeanzishwa kwa lengo la kuwaleta pamoja wadau wa maendeleo ili kuisaidia jamii. Ninaamini kiongozi bora ni yule anayeacha alama. Nami nataka kuacha alama kupitia maisha ya watu ninaowahudumia,” amesema Ulenge.
Amesema kupitia Taasisi ya Ng’arisha Maisha na Taasisi ya Kamal, wamefanikisha kugawa vifaa saidizi vyenye thamani ya Sh170 milioni, vikijumuisha viti mwendo 31, miguu bandia 100 na fimbo 25.
Pamoja na msaada huo kurejesha furaha ya watu hao, bado hauwezi kutatua changamoto iliyopo moja kwa moja, na Mkurugenzi wa Taasisi ya Kamal, Sameer Santosh Gupta amesema taasisi hiyo itaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau wengine kuhakikisha watu wenye ulemavu popote walipo wanapata vifaa saidizi vinavyowarejeshea matumaini ya maisha.
Amesema taasisi hiyo inaamini vifaa saidizi si msaada wa kawaida, bali ni uwekezaji unaowawezesha walengwa kujitegemea, kufanya kazi na kuchangia maendeleo ya jamii badala ya kuendelea kuwa tegemezi.
“Tunafurahi kushirikiana na Taasisi ya Ng’arisha Maisha katika kubadilisha maisha ya watu wenye ulemavu. Tunapochangia vifaa saidizi, tunarudisha heshima, uhuru na uwezo wa watu hawa kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya jamii,” amesema Gupta.
Msaada huo ulimkuna mgeni rasmi katika hafla hiyo, Waziri wa Fedha, Khamis Mussa Omar na akatumia fursa hiyo kumpongeza mbunge Ulenge na Taasisi ya Kamal kwa kuifikiria jamii ya watu wenye ulemavu, akisema msaada huo umefungua fursa mpya za maisha kwa walengwa.
Sawa na waliomtangulia, Waziri Omar amesema vifaa saidizi vinawapa watu wenye ulemavu uwezo wa kuishi kwa kujitegemea, kushiriki shughuli za kiuchumi na kurejesha heshima yao ndani ya jamii.
“Msaada huu si wa vifaa pekee, bali ni wa kurejesha matumaini na utu kwa watu wenye ulemavu. Serikali itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wanaowagusa wananchi wenye mahitaji maalumu na kuwapa fursa ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa,” amesema Balozi Omar.