Simulizi ya kisima cha wivu wa mapenzi cha Mkamandume

Mfanyakazi wa idara ya Makumbusho, Kombo Hamis Kombo akichota maji kwenye kisima cha wivu wa mapenzi ambacho kilitengenezwa na Mkamandume karne ya 15 kwa ajili ya wake zake wawili ili wasijuane kutokana na wivu wa mapenzi katika kijiji cha Pujini Mkoa wa Kusini Pemba. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

  • Katika kusaka historia hiyo, Mwananchi ilifunga safari ya kilomita zaidi ya saba kutoka senta maarufu ya Machomanne, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, kwenda kukisaka Kijiji cha Pujini chenye historia ya pekee ya mapenzi.

Kwa nini watu hufikia hatua ya kuuana kutokana na wivu wa mapenzi?

Hilo ni miongoni mwa maswali ambayo watu wengi hujiuliza bila kupata majibu ya moja kwa moja.

Lakini! Ukatili huu unatokana na nini?

Wazee waliokula chumvi nyingi wanasema kwa vijana wa sasa, si rahisi kuelezea hilo.

Hata hivyo, historia inafichua kwamba wivu wa mapenzi haujaanza karne hii ya 21, bali ulikuwapo tangu enzi na enzi.

Hilo linakuja kuthibitika katika karne ya 15, zaidi ya miaka 600 iliyopita.

Katika kusaka historia hiyo, Mwananchi ilifunga safari ya kilomita zaidi ya saba kutoka senta maarufu ya Machomanne, Wilaya ya Chake Chake Mkoa wa Kusini Pemba, Zanzibar, kwenda kukisaka Kijiji cha Pujini chenye historia ya pekee ya mapenzi.

Katika kijiji hicho, kuna eneo maarufu linalohifadhiwa, kulindwa na kutunzwa na watu wa idara ya mambo ya kale lenye ukubwa wa eka mbili likiwa limezungushiwa uzio.

Ndani ya uzio huo kumejengwa kibanda ambacho ndani yake kuna kisima cha maji kinachoitwa Kisima cha Wivu wa Mapenzi.


Kwa nini wivu wa mapenzi?

Kombo Hamis Kombo ni mfanyakazi wa idara ya makumbusho anayehudumia eneo hilo kwa sasa.

Katika mazungumzo na Kombo anasimulia historia ya kisima hicho, aliyekijenga.

“Mkamandume jina lake halisi ni Mohamed Abdulrahman, huyu ni Mpashia kutoka Iran, katika kutembea kwake alifika katika kijiji hiki cha Pujini akaweka makazi baada ya kupendezeshwa na maeneo hayo,” anasema Kombo.

Anasema aliitwa jina hilo kutokana na tabia yake ya kuwatesa na kuwanyanyasa kwa kutawala wakazi wa eneo hilo, wanaume alikuwa akiwakamua sehemu zao za siri, kwa hiyo akaitwa mkamua waume, lakini kutokana na matamshi ikaitwa Mkamandume.

Kombo anasema baada ya Mkamadume kuanzisha makazi yake katika eneo hilo karne ya 15, alioa wanawake wawili aliokuwa akiishi nao katika jengo hilo lililokuwa na majengo mengi ndani yake.

Hata hivyo, kwa sasa hakuna jengo hata moja, maana yameporomoka na kubaki eneo hilo kama kiwanja isipokuwa kisima hicho cha wivu wa mapenzi.

Kombo anasema baada ya Mkamandume kuanzisha koloni lake hapo alikuwa akiwatumikisha wananchi na mtu aliyetaka kumfikia.

Katika hekalu lake kulikuwa na mageti matatu ambayo kila moja lilikuwa na mlinzi wake. Iwapo mlinzi wa geti la kwanza akiruhusu kuingia lakini wale wa mageti yanayofuatia wakagoma, hivyo mtu huyo atatoka nje.

“Mkamandume alikuwa mtawala wa eneo hilo, kwa hiyo wananchi wote wakawa chini yake na akawa ndiye anawaongoza na kuamua,” anasema Kombo.


Kisima cha wivu

Mfanyakazi huyo wa Idara ya Makumbusho anasema, licha ya Mkamandume kuwa na wanawake wawili, lakini aliwaficha siri kiasi kwamba hakuna aliyemjua mwenzake, badala yake kila mmoja akawa anaamini yupo peke yake kwa kigogo huyo, licha ya kuishi katika eneo hilo.

Anasema kila mmoja alikuwa ana sehemu yake, hivyo alikuwa akienda kwa mmoja baada ya mwingine alipokuwa akiwahitaji.

Kutokana na hali hiyo, Mkamandume alihisi sehemu pekee wanayoweza kuonana wake zake hao ni wakati wa kuchota maji kisimani, hivyo kisima hicho akakitengeneza kwa mfumo ambao wasiweze kuonana na kukiwekea ukuta katikati.

Katika kisima hicho upande mmoja wa kusini alitengeneza ngazi za kushuka hadi chini na upande mwingine wa Kaskazini ukabaki juu, kwa hiyo mwanamke mmoja alikuwa akitumia upande wa ngazi na mwingine anatumia upande uliobaki juu kwa kufunga ndoo kamba na kutumbukiza ndani ya kisima kutokana na urefu.

Mwanamke aliyekuwa akitumia ngazi alikuwa akichota maji kwa kutumia kata kutokana na ufupi wa kisima hicho.

Licha ya kujenga ukuta huo, Mkamandume hakuishia hapo, bali aliwapangia wake zake hao wawili zamu za kuwa wanachota maji kila mmoja kwa muda wake, mmoja alipangiwa kuchota maji kuanzia saa 12:00 asubuhi hadi saa 6:00 mchana na mwingine kuanzia saa 6:00 mchana hadi saa 12:00 jioni.

Alikuwa akiwaeleza iwapo wataenda kuchota maji tofauti na muda huo, huenda wangepata madhara kwa sababu kuna hali ya hatari katika kisima hicho, lakini kumbe lengo lake kubwa ilikuwa wasiweze kuonana na kukaibuka mtafaruku.

Hata hivyo, wake zake walikuwa wakipata shauku ya kutaka kujua ukweli wa jambo hilo, kwahiyo ilitokea siku moja wakavunja taratibu hizo wakaenda kuchota maji kila mmoja kwa muda ambao hakupangiwa, bahati mbaya wote wakajikuta wanaenda muda mmoja.

Hata hivyo, licha ya kukutana kisimani hawakuweza kuonana uso kwa uso, bali walipokuwa wakichota maji kila mmoja alianza kushangaa ndani ya kisima kile kwa kukutanisha ndoo na kata kisha wakapata mshtuko.

Walivyorudi ndani bila kuonana kila mmoja kwa wakati wake alimsimulia mume wake jinsi alivyokutana na maajabu kule kisimani.

“Mkamandume aliendelea kufoka akisema nilishakwambia usiende kuchota maji tofauti na muda ambao nimekupangia pale kuna mambo ya vitisho na mashetani utapata matatizo,” anasimulia Kombo.

Maneno hayohayo aliyasema kwa mwanamke mwingine, hivyo wanawake wale waliamini kweli kisimani si shwari, kwa hiyo wakaendelea kuchota maji kwa muda ambao kila mmoja alikuwa amepangiwa.


Watoto wake wafa kiajabu

Kombo anasema Mkamandume alikuwa na watoto watatu, huku wawili wakiwa wa mwanamke mmoja.

Hata hivyo, anasema mtoto mmoja alifariki dunia akiwa mchanga na wengine wawili wanadaiwa walikufa katika mazingira ya utata kwa kuomba ardhi ipasuke kisha ikawafunika.

Hatima yake katika kijiji hicho Kombo anasema Mkamadume alikimbia eneo hilo baada ya kupata taarifa kwamba anakuja kukamatwa, kwa hiyo akakimbilia kusikojulikana.

Hata hivyo, Kombo anasema eneo hilo linahitaji jitihada za makusudi ili kuliboresha na kutunza historia yake, jambo litakaloweza kuvuta watalii wengi kutoka ndani na nje ya nchi kutembelea.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Shukuna Khatib anasema wapo watu ambao hufika katika kijiji hicho kuchukua maji hayo wakiamini yanaweza kuwasaidia, ingawa wengi hawajui historia yake.