Sintofahamu uwanja wa ndege Dodoma kutokuwa na taa

Dodoma. Sintofahamu imeibuka kuhusu uwanja wa ndege wa Dodoma kutokuwa na taa za kuwezesha ndege kuruka na kutua usiku.

Sintofahamu hiyo pia imeongezeka baada ya jana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) kutoa taarifa kwamba uwanja wa ndege wa Songwe mkoani Songwe umewekwa taa na huduma za ndege zinatolewa kwa saa 24.

Ukosefu wa taa kwenye uwanja huo ulibainika baada ya ndege ya Precision namba PW 602 iliyosafiri Mei mosi kutoka uwanja wa kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam kwenda Dodoma ikiwa na abiria 72 kugeuza njiani kwa maelezo uwanja hauna taa.

Ndege hiyo kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), Hamza Johari iliondoka Uwanja wa JNIA saa 12:11 jioni na ilitarajiwa kutua Dodoma saa 01:13, wakati mwisho wa kutua ndege ni saa 12:30 jioni.

Kwa mujibu wa Johari, uwanja wa ndege wa Dodoma unafanya kazi kuanzia mawio hadi machweo.

“Ilipofika saa 12:48 jioni, rubani wa ndege hiyo alilazimika kugeuza na kurudi uwanja wa JNIA baada ya kushauriwa na muongoza ndege wa zamu,” ilieleza taarifa ya Johari.
Alisema kilichofanyika ni ukiukwaji wa taratibu za kiuendeshaji na kwamba TCAA inaendelea na uchunguzi kuangalia kama kuna uvunjaji wa kanuni za usafiri wa anga katika safari hiyo na endapo itabainika mamlaka haitasika kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa sheria.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana, Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura alisema kimsingi ndege inayosafiri kwa kuchelewa kwenda kwenye uwanja wa ndege ambao hauna taa huwa hairuhusiwi kutua.

“Kimsingi huwa hairuhusiwi na ndiyo maana regulator (Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania - TCAA) kwenye taarifa yake amesema atafanya uchunguzi kwa kuwa huwa hairuhusiwi,” alisema Mbura.

Msemaji wa Shirika la Ndege la Precision alipoulizwa kuhusu tukio la ndege yao kugeuza angani kwa kuwa haikuweza kutua uwanja wa ndege wa Dodoma kwa kuwa hakuna taa alisema: “TCAA ni mamlaka wanaotusimamia, tumeona tuwape kwanza heshima kwa kuwa tayari wamesema wanafanya uchunguzi. Wacha kwanza wamalize uchunguzi wao,” alisema Hillary.

Makao makuu

Dodoma ndio makao makuu ya nchi yaliyotangazwa mwaka 1973 na Rais wa awamu ya kwanza, Mwalimu Nyerere na Julai 2016 Rais wa awamu ya tano, John Magufuli alitoa amri ya Serikali kuhamia Dodoma.

Kiongozi wa kwanza kuhamia Dodoma alikuwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Rashid Kawawa na alifuatiwa na Edward Sokoine, Cleopa Msuya, Salim Ahmed Salim na Joseph Warioba.
Mwaka 1991, nchi ikiongozwa na Rais Ali Hassan Mwinyi, Waziri Mkuu, John Malecela alirejesha makazi ya Waziri Mkuu Dar es Salaam.

Hata hivyo, baada ya miaka 42 Rais Magufuli Julai 2016 alitoa amri ya Serikali kuhamia Dodoma na Oktoba 12, 2019 alijiandikisha katika daftari la orodha ya wapiga kura katika kijiji cha Chamwino mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alihamia rasmi Dodoma Septemba 26, 2016.

Maoni ya wadau

Baadhi ya wasomi, wafanyabiashara na wanasiasa wameonyesha kushitushwa na taarifa za ukosefu wa taa kwenye uwanja wa ndege ambao ni muhimu kwa viongozi, wanasiasa na wafanyabiashara.

“Kuna abiria wengine wanakuja Dodoma kwa shughuli za siku moja, anakuja asubuhi anataka arudi siku hiyo hiyo, kama ndege mwisho wa kuruka na kutua ni saa 12:30 jioni, hiyo ni changamoto kwa maendeleo ya kiuchumi ya Taifa na mkoa,” alisema msomi wa masuala ya biashara, George Maganga ambaye pia ni mwanasheria.

Mbali na Maganga, Ashrafu Juma, mfanyabiashara wa Dodoma alisema ukosefu wa taa unawakosesha wafanyabiashara fursa za uwekezaji.

“Unajua unaweza kumshawishi mwekezaji kutoka nje ya Dodoma, na huyu si lazima alale Dodoma, anaweza kuja na kurudi kwa kutumia ndege za usiku, hivyo uwepo wa ndege za usiku ni muhimu kiuchumi,” alisema.

Mtumishi wa umma ambaye hakupenda kutaja jina lake, alisema Dodoma bado haijawa na hoteli za kutosha na zenye hadhi ya kimataifa, zinapokuwa zimejaa wageni wenye hadhi hiyo wanashindwa kuja Dodoma kwa safari ya siku moja.

“Mfano, shughuli nyingi zinazoalika viongozi wa mataifa mengine zinashindwa kufanyika hapa na hata zikifanyika ratiba zao zinakuwa za mbio mbio,” alisema.

Taa kuwekwa Septemba

Kutokana na sintofahamu hiyo, jana Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA) ilitoa taarifa ikisema kiwanja cha ndege Dodoma kitaanza kutoa huduma za ndege kuruka na kutua kwa saa 24 kuanzia Septemba mwaka huu.

Kauli hiyo imo kwenye taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa TAA, Mussa Mbura alipokuwa akitoa ufafanuzi kuhusu ndege ya Precision kushindwa kutua katika kiwanja hicho kwa sababu ilifika usiku.

Mbura alisema mahitaji ya huduma za usafiri wa ndege Dodoma ni makubwa na awali walikuwa na mruko mmoja kwa safari za ndege ya abiria kwa siku.

Mbura alisema kwa sasa ndege haziwezi kutua usiku katika kiwanja hicho kwa sababu hakina miundombinu ya taa za kuongozea ndege.

Alisema mfumo wa taa za kuongozea ndege ulianza kufungwa Machi mwaka huu baada ya Serikali kutoa Sh12 bilioni kuwalipa fidia wananchi waliokuwa wakiishi jirani na eneo la kiwanja hicho.

Mbura alisema kazi ya kuweka taa za kuongozea ndege imefikia asilimia 40 na sasa wanasubiri taa zinazotengenezwa nchini Hispania.

“Katika majaribio ya kuziwasha tunakwenda na timu ya wataalamu wetu kuzikagua wakati wa kuziwasha na Mei 13 baada ya majaribio ya mwisho tutazisafirisha kuja Tanzania, ni mzigo mkubwa na mzito. Ni zaidi ya kontena mbili hizo taa,” alisema.

Mbura alisema kwa sasa uwanja wa ndege Dodoma unaruhusu ndege kuruka na kutua kuanzia saa 1:00 asubuhi hadi saa 12:30 jioni kwa mujibu wa waraka uendeshaji uwanja huo NOTAM namba B 0027/23, B 0026/23, B0025/23, B0024/23 na B0023/23.

Alisema uwanja huo unaendeshwa kwa kuangalia mawio na machweo ya jua kulingana na taarifa za usalama wa anga namba GEN 2.7-4 ya Januari 5, 2017 na ndege haziruhusiwi kuruka wala kutua baada ya saa 12:30 jioni.