Sintofahamu wanafunzi kuingilia mfumo UoI, kujilipia ada kinyemela

Iringa. Wanafunzi wanaokadiriwa kuwa 262 wanaosomea kozi ya teknolojia ya habari (Information Technology) katika Chuo Kikuu Iringa (UoI), wanatuhumiwa kughushi mfumo wa SAMIS na kujilipia ada huku chuo kikiingilia kati suala hilo.

Mkuu wa Chuo Kikuu Iringa (UoI), Profesa Ndelerio Urio alikiri juu ya tatizo hilo kutokea na kwamba uongozi ulichukua hatua kwa kuunda tume ya watu wanne ambao wanaendelea kufanya uchunguza wa tukio hilo ambapo limekikoseha chuo mamilioni ya fedha.

Mfumo wa SAMIS unaodaiwa kuingiliwa na wanafunzi hao unatumika na chuo hicho katika masuala ya malipo ya ada, kuweka kumbukumbu za wanafunzi na masomo.

“Wanafunzi waliingilia mfumo, waghushi malipo ya ada na hivyo kuonekana hawadaiwi. Hii imekikosesha UoI mamilioni ya shilingi. Pia wanadaiwa kughushi stakabadhi za malipo na mihuri ya benki ili kuridhisha kuwa hawadaiwi ada,” amesema Profesa huyo.

Kwa mujibu wa uchunguzi ulifanywa na Mwananchi na kuthibitishwa na uongozi wa chuo, imebainika wanafunzi waliofanya hujuma hiyo ni wale wanaosomea cheti na shahada ya awali (bachelor) hali ambayo imeleta taharuki chuoni hapo.

Taarifa zinatanabaisha kuwa ada wanayopaswa kulipa wanafunzi wanaosomea kwa mwaka katika ngazi za cheti (certificate) ni Sh840, 000 huku wale wanaosomea shahada kwanza wakitakiwa kulipa Sh1, 670,400 katika mwaka wao wa kwanza.

Huku Sh1, 610,400 na Sh1, 760,400 zikitakiwa kulipwa mwaka wa pili na wa tatu wa masomo chuoni hapo.

Hata hivyo Mkuu huyo wa UoI ameiambia Mwananchi Digital kuwa uchunguzi wa awali uliofanywa ulibaini wanafunzi 262 ndio walihusika katika kadhaa hiyo ambao baada ya kufanikiwa na ukaonyesha wamelipa ada, waliruhusiwa kufanya mitihani kabla chuo hakijashtukia hujuma hiyo.

"Baada ya kuwabaini wanafunzi waliofanya hujuma hiyo huku wakiwa tayari walishafanya mitihani, tumezuia matokeo yao hadi watakapolipa ada kamili wanayodaiwa," alisema Profesa Urio