Siri kupungua matukio ya ukatili kwa watoto Mara

Baadhi ya majeraha ya Melesiana Nestory (16) anayedai kufanyiwa ukatili na mwajiri wake wa kazi za ndani

Muktasari:

  • Jumla ya matukio 605 vya ukatili kwa watoto yameripotiwa mkoani Mara mwaka 2022/23 na kati ya hayo, 402 yalikuwa ya ukatili wa kimwili na 109 wa kingono.

Musoma. Wakati mkoa wa Mara ukifahamika kwa matukio ya ukatili nchini, takwimu zinaonyesha jumla ya matukio 605 ya ukatili dhidi ya watoto yameripotiwa mkoani humo katika kipindi cha mwaka 2022/23.

Matukio hayo yamepungua kutoka matukio 816 yaliyoripotiwa mkoani humo mwaka 2021/22. Hata hivyo, wito umetolewa wa kuendeleza mapambano dhidi ya vitendo vya ukatili kwa watoto kwani bado vipo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Aprili 21, 2024, Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mara, Elizabeth Mahinya amesema licha ya matukio hayo kuonekana kupungua hali bado sio nzuri, hivyo jitihada zaidi bado zinahitajika.

“Bado hatuwezi kusherehekea kuwa matukio yamepungua, hali bado si nzuri katika jamii, kuna kipindi matukio yanaonekena kupungua na kuna kipindi yanaongezeka na hii inategemanana na matukio katika jamii, mfano kuna mwaka koo nyingi zinafanya ukeketaji na kuna mwaka ukeketaji unafanywa na wachache,” amesema.

Amesema halmashauri ya Wilaya ya Bunda Vijijini inaongoza kwa kuwa na matukio mengi kati ya halmashauri zote tisa za mkoa wa Mara ambapo katika kipindi hicho, jumla ya matukio 192 yaliripotiwa.

Halmashauri ya wilaya ya Butiama imeripotiwa kuwa na matukio machache zaidi, yakifikia 25 katika kipindi hicho.

Mahinya amesema kati ya matukio hayo, vitendo vya ukatili wa kimwili vimeonekana kuwa vingi zaidi vikifuatiwa na matukio ya ukatili wa kingono kwa watoto.

Ofisa huyo amesema katika kipindi hicho wamebaini kuwa vitendo vingi vya ukatili kwa watoto vinafanywa na watu wa karibu na waathirika wa ukatili huo wakiwepo wazazi, walezi na ndugu wa karibu.

Kuhusu sababu za vitendo hivyo, alisema hali ngumu ya uchumi ni moja ya sababu ambapo baadhi ya ndugu au wazazi wamejikuta kwenye msongo wa mawazo hivyo kusababisha kuchukua hatua kali na kuwaadhibu watoto bila kufikiria madhara yake.

“Mfano unakuta mtoto amechomwa na moto kisa tu ameiba Sh100, yaani mtoto anapewa adhabu kubwa mno kuliko kosa lenyewe na hii ina maana kama kusingekuwa na umasikini, basi mzazi au mlezi asingemuadhibu kiasi hicho.

Imani za kishirikina pia ni chanzo kingine cha uwepo wa vitendo hivyo ambapo baadhi ya watu wamekuwa wakidanganywa na waganga wa kienyeji kufanya ngono na watoto, hatua ambayo inasababisha watoto kubakwa na kulawitiwa.


Changamoto kuyakabili

Ofisa huyo amesema zipo changamoto wanazokumbana nazo katika utatuzi wa masuala ya ukatili huo.

“Mfano kwenye suala la kutelekeza watoto tumekuwa tukifanya vizuri na wahusika wamekuwa wakikubali kuwajibika kwa kutoa mahitaji ya msingi katika malezi ya watoto au kurejea katika familia zao na kuungana katika malezi ya watoto,” amesema

Amesema changamoto ipo katika kesi za ubakaji na ulawiti ambapo mara nyingi ushahidi unakosekana baada ya wahusika kuamua kumaliza masuala hayo katika ngazi ya familia.

“Matukio mengi yanafanywa na watu wa karibu kwa hiyo mtoto akibakwa au kulawitiwa wanakutana na kuzungumza kisha mtoto anakataa kutoa ushirikiano” amesema.


Kesi kortini

Amesema katika kipindi hicho, jumla ya kesi 18 za ukatili zilifikishwa mahakamani na kati ya hizo 12 zilitolewa hukumu na wahusika kuhukumiwa kutumikia adhabu tofauti t huku kesi nyingine sita zikiendelea.

Mratibu wa Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto Mkoa wa Mara, Charles Mashauri amesema watoto wengi wameathirika na adhabu kali zinazotolewa kwao hususan za viboko.

Mashauri amesema programu hiyo inayotekelezwa na serikali kwa kushirikiana na wadau, pamoja na mambo mengine  inalenga kuimarisha ulinzi na usalama wa mtoto ili kuwa na kizazi bora kwa ustawi wa Taifa.

Amesema adhabu ya viboko imekuwa ikitolewa katika ngazi ya familia na hata shuleni na kwamba utoaji huo wa adhabu hauzingatii utaratibu badala yake watoto wamekuwa wakiathirika badala ya kuadabishwa.

“Wakati nafanyakazi sehemu moja kwenye kitengo cha watu wenye ulemavu, wapo watoto waliokuwa wakiletwa pale wakiwa wamepata ulemavu kutokana na adhabu, sasa badala ya kumuadabisha anaumizwa kimwili kwa adhabu zilizopitiliza,” amesema.

Wakizungumza kuhusu vitendo hivyo, baadhi ya wadau wa masuala ya haki za watoto wamesema ukatili dhidi ya watoto unapaswa kukomeshwa kwani una athari kubwa katika ustawi wa jamii na taifa kwa ujumla.

Davis Dominic amesema moja ya madhara ya vitendo hivyo ni ongezeko la watoto wa mitaani kwani wengi wanalazimika kutoroka majumbani na kukimbilia mitaani, jambo ambalo lina athari kubwa katika jamii.

“Sote tunajua tabia za watoto wa mitaani na wale wakikua hivyo hivyo mwisho wao unakuwa sio mzuri,” amesema.

Ulinzi wa mtoto

Paroko wa Parokia ya Kristo Mfalme Rwamlimi Manispaa ya Musoma, Padri Agostino Mapambano amesema mtoto anatakiwa kulindwa tangu anapozaliwa hadi anapofikia umri wa utu uzima.

Amesema vitendo vya ukatili kwa watoto vipo ila vimegubikwa na usiri mkubwa, hali inayoleta ugumu katika kuwawajibisha wale wanaohusika na vitendo hivyo.

“Wale wanaotendewa wanakuwa hawako tayari kuzungumza labda kwa kuogopa ama kuamua kuyamaliza katika ngazi ya jamii na hii inawapa mwanya watendaji wa vitendo hivyo kuendelea kufanya hivyo wakijua hakuna hatua zitakazochuliwa dhidi yao,” amesema.

Mdau mwingine Kumbi Makanyanga amependekeza ili kukabiliana na vitendo hivyo ni vema ukawepo utaratibu maalumu wa kufuatulia vitendo hivyo kuanzia ngazi ya vijiji na mitaa.

Mwanaharakati wa haki za wanawake na watoto, Rhobi Samuel amesema mbali na kuathirika kisaikolojia lakini pia vitendo vya ukatili kwa watoto ni chanzo cha maambukizi ya magonjwa ya ngono kwa watoto.

“Unashangaa mtoto amezaliwa mzima wa afya njema lakini baadaye akiwa na miaka hata sita anakuwa na ugonjwa wa Ukimwi, ukifuatulia ni mwathirika wa ubakaji au ulawiti,” amesema.

Amesema vitendo hivyo vikiachwa upo uwezekano mkubwa wa kuwa na kizazi kisichojali haki na utu wa mtoto kwani waathirika wa vitendo hivyo watakapokuwa watu wazima nao watawalea watoto wao katika misingi hiyo ya ukatili.