Siri mafuriko ya watalii, mawakala wakiuza mali

Watalii wakimwangalia tembo akivuka barabara ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara wilaya ya Monduli mkoa wa Arusha juzi. Watalii wa ndani na kutoka nje wameendelea kutembelea vivutio vya kitalii katika maeneo mbalimbali nchini. Picha na Filbert Rweyemamu

Muktasari:

  • Wakati taasisi za uhifadhi zikifurahia mafuriko ya watalii wanaoingia nchini kwa sasa, hali ni tofauti kwa baadhi ya mawakala wa utalii wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao wanalazimika kuuza mali zao na kukopa fedha ili kuwahudumia wageni hao.

Arusha. Wakati taasisi za uhifadhi zikifurahia mafuriko ya watalii wanaoingia nchini kwa sasa, hali ni tofauti kwa baadhi ya mawakala wa utalii wa mikoa ya Arusha na Kilimanjaro ambao wanalazimika kuuza mali zao na kukopa fedha ili kuwahudumia wageni hao.

Uchunguzi uliofanywa na Mwananchi kwa baadhi ya kampuni na mawakala wa utalii umebaini idadi kubwa ya watalii wanaoingia nchini hivi sasa ni wale waliositisha safari zao mwaka 2019 na 2020 kutokana na kuibuka kwa janga la Uviko-19 lililosababisha mipaka ifungwe na usafiri wa anga kusitishwa kudhibiti maambukizi mapya.

Watalii hao, wengi kutoka mataifa ya Marekani, Uingereza, Ujerumani na Italia, walikuwa wameshalipia zaidi ya asilimia 50 ya gharama husika kabla ya kuingia nchini kupitia mawakala wa nje ya nchi ambao wana ubia na kampuni za ndani, huku wengine wakilipa mojamoja kwa mawakala wa ndani.

Baadhi ya wakurugenzi wa kampuni za utalii na wadau wa sekta hiyo wameomba itolewe ahueni kwa baadhi ya kampuni ambazo hivi sasa zinakabiliwa na ukata ili kugharamia mahitaji ya wageni zinaowapokea ambao walilipa kabla ya kuibuka kwa Uviko-19.

Mkurugenzi wa kampuni ya Big Expedition & Safaris, Angel Minja alisema ingawa kampuni yake haina changamoto kubwa, anatarajia kupokea zaidi ya watalii 250 ambao walishindwa kuja nchini kati ya mwaka 2019 na 2020 lakini walilipia safari zao.

Minja alisema changamoto iliyopo ni kwamba wageni hao walilipa kwa viwango vilivyokuwapo mwaka 2019 na 2020, lakini hali ni tofauti sasa hivi kutokana na kupanda kwa gharama za vitu vingi, yakiwamo mafuta na ada za kuingia hifadhini.

Hata hivyo, alisema wanaomba taasisi za uhifadhi na Serikali kuwafikiria wenye kampuni ambazo zitakuwa na changamoto ya fedha katika kipindi hiki, hasa kutokana na kuongezeka kwa gharama za utalii kwa ujumla.

“Watalii wanaokuja leo huwezi kuwadai fedha zaidi ama kuwapandishia bei ya kutalii kutokana na ongezeko la kodi za ndani hivyo hii ni changamoto,” alisema.

Mkurugenzi mwingine wa kampuni ya utalii aliyeomba kuhifadhiwa jina alisema amepokea kundi la watalii 105 ambao walilipa asilimia 50 tangu mwaka 2019, hivyo imekuwa changamoto kwake.

“Kaka huwezi amini, nimeuza mali zangu kadhaa na bado ninadaiwa ili niweze kuwapa huduma bora kama nilivyowaahidi hawa wageni wangu na tayari wameondoka nchini salama,” alisema.

Mkurugenzi huyo alisema kazi nzuri aliyofanya Rais Samia Suluhu Hassan katika filamu ya Royal Tour imekuwa na faida, lakini wageni wapya wataanza kuingia nchini kuanzia mwakani.

“Haya mafuriko ya watalii wa sasa wengi ni waliokuwa wamelipia nyuma, lakini tunatarajia kupata mafuriko makubwa zaidi miaka ijayo, kwani kwa kawaida watalii wengi hupanga safari zao mwaka mmoja kabla ya safari,” alisema.


Deni la Sh20 milioni

Katibu Mtendaji wa Chama cha Wapagazi Mlima Kilimanjaro na Meru (TPO), Loshiye Mollel alisema hadi sasa kinazidai baadhi ya kampuni za utalii zaidi ya Sh20 milioni ambazo bado hazijalipwa.

Mollel alisema sababu za kampuni kushindwa kuwalipa wasaidizi hao wa watalii wanaopanda Mlima Kilimanjaro na Meru ni zenyewe kulipwa kabla ya janga la Uviko-19 hivyo baadhi kutokuwa na fedha za kutosha hivi sasa.

“Wameomba wapagazi waendelee na kazi huku wakiwadai kwa kuwa watapokea watalii wengine siku si nyingi ambao watawalipa na tumeona ili kutoharibu utalii waendelee kutoa huduma,” alisema Mollel.

Mwenyekiti wa Chama cha Waongoza Watalii Tanzania (TTGA), Emmanuel Mollel alisema kupanda kwa gharama za uendeshaji, ikiwamo mafuta kumeathiri sekta ya utalii, kwani zimeongezeka tofauti na mwanzo.

Mollel alisema kampuni nyingi zimeongezewa mzigo kutokana na gharama za mafuta, kwani kwa sasa huwezi kudai fedha nyingine kwa watalii ambao tayari walishaingia nao makubaliano na wakalipa sehemu ya fedha.

“Naona hata gharama za kukodi magari kwenda hifadhini zimeongezeka sana, lakini kuhusiana na ada za kuingia hifadhini nyingi zimepanda, ingawa baadhi ya kampuni ziliwapa taarifa wageni wao juu ya mabadiliko hayo,” alisema Mollel.


Tato yawaita wanachama

Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Utalii Tanzania (Tato), Sirili Akko akizungumzia changamoto zinawakabili mawakala wa utalii, alisema wanawapokea wageni walioahirisha safari zao mwaka 2019 na 2020 hivyo kukuta baadhi ya mawakala wakiwa hawana kitu hivyo kuwataka wenye changamoto hiyo kwenda ofisini kwake.

“Ili wasiharibu soko la utalii wetu, tunaomba wanachama wenye changamoto ya kushindwa kulipia mahitaji ya wageni wao waje ofisini tujadiliane nao na Serikali ione jinsi gani waendelee na kazi vizuri,” alisema Akko.

Katibu mtendaji huyo alikiri kuwa gharama za uendeshaji kwa mawakala wa utalii ni changamoto kubwa kutokana na kupanda kwa bei za huduma na bidhaa, hasa mafuta tofauti na ilivyokuwa katika miaka miwili ya nyuma. Hali hiyo, alisema inaleta changamoto katika utekelezaji wa mkataba kwa baadhi ya kampuni zilizokuwa zimepokea maombi ya wateja waliolipia.

“Ingawa hadi sasa sijapata malalamiko rasmi ya wanachama wetu kushindwa kutoa huduma, lakini ni kweli kuna changamoto kwa baadhi ya kampuni ambazo hazikuwa zimejiandaa kupokea wimbi kubwa la watalii,” alisema.

Akko alisema kuna changamoto kwa baadhi ya kampuni zinapopokea malipo ya awali ya watalii zinatumia kwenye mambo mengine kwa kuamini watapata fedha nyingine, ila zikikosekana kama ilivyokuwa wakati wa janga la Uviko-19 inakuwa shida.

“Tunashauri wenye kampuni kuwa na matumizi mazuri ya fedha kama ilivyokusudiwa na makubaliano jinsi watakavyotatua shida inapotokea mtu wa tatu kuwa tayari amelipwa na mtalii akasitisha safari,” alisema.


Royal Tour yaleta wawekezaji

Akko alisema hivi sasa sambamba na kuongezeka kwa watalii nchini, wameanza kupokea wawekezaji wapya ambao wanataka kunufaika na fursa zilizopo kwenye sekta ya utalii.

“Tunamshukuru sana Rais Samia kwa kuandaa filamu ya Royal Tour, kwani sasa kuna wawekezaji wanakuja kuulizia taratibu za kuwekeza. Tayari tumewapokea na kuzungumza na baadhi yao hapa ofisini,” alisema.

Akko alisema wanatarajia katika miaka ijayo, kutakuwa na mafuriko makubwa ya watalii, kutoka mataifa mbalimbali kutokana na Tanzania kutangazwa vizuri na filamu hiyo.