Siri mpango wa kuwalipua bomu askari, watupwa jela

Songea. Mahakama Kuu Kanda ya Songea, imewahukumu watu watatu kifungo cha miaka 15 jela kwa kuwashambulia askari polisi watano kwa mabomu na kuwasababishia majeraha mwilini, mmoja akikatwa vidole vya mguu.

Moja kati ya mabomu hayo yaliyolipuliwa yaliwalenga askari polisi kati ya Januari 1, 2014 na Desemba 25, 2014, lilitegeshwa kwenye kibanda wanachopumzikia askari wa usalama barabarani (trafiki), lakini liligunduliwa mapema na kuharibiwa.

Hukumu dhidi ya mshtakiwa wa kwanza, Juma Msabila, wa pili Hamza Yusuph na wa tatu Yasini Mussa, ilitolewa Desemba 22, 2023 na Jaji Elinaza Luvanda na kuwekwa mtandaoni wiki hii.

Washtakiwa wawili walioachiwa huru baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao kwa viwango visivyoacha shaka ni Hassan Mponda (wa nne) na Said Muhando (wa tano).

Mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kula njama ya kutenda kosa la ugaidi, kushiriki mkutano wa kupanga ugaidi, kukusanya Sh1.6 milioni za kununua milipuko na kujaribu kuwaua askari polisi.

Mshtakiwa wa tano, Muhando, alikuwa akikabiliwa na kosa la kumficha mtuhumiwa aliyetekeleza kitendo cha kigaidi aliyetajwa kwa jina moja la Zuberi, huku akijua lilikuwa ni kosa la jinai.


Maelezo ya makosa

Makosa ya ulipuaji mabomu na kujaribu kuua askari polisi yanadaiwa kufanywa na mshtakiwa wa kwanza hadi wa nne, ikielezwa mabomu yaliyotengenezwa kienyeji yaliwajeruhi askari watano.

Polisi hao ni Felister Abel, Ramadhan Ally, G 5515 PC John, WP 8616 PC Mariam, G9703 PC Mselem. Walijeruhiwa kati ya Septemba 16 na Desemba 25, 2014 na askari mmoja kati yao alikuwa na majeraha mabaya zaidi.

Majeraha hayo inaelezwa yalikuwa mabaya kwamba, mguu ulijeruhiwa, vidole vitatu vilikatwa, hivyo kulazimika kufanyiwa upasuaji mkubwa ili kuondoa vyuma vya bomu vilivyoingia mwilini mwake.

Kulingana na ushahidi wa upande wa mashtaka, mwaka 2014, matukio matatu ya ugaidi yalitokea Songea, moja ni Septemba 16 saa 1.04 usiku mtaa wa Maliatabu, ambako polisi wakiwa doria kwa miguu walibaini watu wawili wanawafuatilia.

Baada ya kuwashuku, watu hao waliwapita kwa kasi na kuwashambulia kwa bomu askari watatu, mmoja ndiye alijeruhiwa zaidi na kukatika vidole vitatu.

Oktoba 27, 2014 saa 10 alasiri katika eneo la Mshangao, trafiki alibaini bomu lililokuwa limetegwa katika kibanda wanachokitumia kupumzikia.

Inaelezwa aliona waya ukitokea msituni hadi katika kibanda bomu hilo lilipotegeshwa.

Siku ya Krismasi Desemba 25, 2014 kati ya saa 1.30 na saa mbili usiku katika eneo la Majengo, wakati polisi wengine watatu wakifanya doria, ilitokea pikipiki ikiwa mwendo mkali na kukaribia kuwagonga askari hao watatu.

Watu wawili waliokuwa kwenye pikipiki hiyo, mmoja mwanamke akiwa amevaa hijabu, aliwashutumu askari hao kwa kutembea barabara yote, baadaye kidogo walishambuliwa kwa bomu lililosababisha vumbi jingi katika eneo hilo.

Bomu hilo liliwajeruhi askari hao na wawili walipoteza fahamu eneo la tukio.

Katika utetezi, washitakiwa wote watano walikana kula njama, kushiriki katika mikutano ya kupanga ugaidi, kukusanya fedha kununua silaha na milipuko na kujaribu kuwaua askari polisi kwa kuwashambulia kwa mabomu.


Kifungo jela

Akisoma hukumu, Jaji Luvanda alisema ni vyema kielelezo namba 11 cha upande wa mashitaka ambayo ni maelezo ya kukiri kosa ya mshitakiwa wa kwanza, Msabila kizingatiwe. Mshitakiwa alikiri kushiriki makosa hayo.

Jaji alisema katika maelezo hayo, mshitakiwa alikiri kushiriki mafunzo na mikutano ya kupanga kutekeleza vitendo vya ugaidi, kutafuta silaha, kufanya harambee kutoka kwa washirika wao kwa lengo la kununua silaha.

Pia alikiri kushiriki mafunzo maalumu ya kutengeneza bomu kienyeji na kutekeleza shambulio lililofanyika Septemba 14 huko Mabatini katika mji wa Songea na tukio lingine la shambulio kwa polisi la Desemba 25.

Vivyo hivyo Jaji alisema mshitakiwa wa pili, Yusuph, alikiri kushiriki mikutano ya kupanga matukio ya kigaidi na kushiriki tukio la Septemba 16, 2014 kwa kuwashambulia askari kwa bomu la kurusha kwa mkono.

Kulingana na maelezo hayo, ndiye aliyekiri kutega bomu katika kituo cha Mshangamo ambacho trafiki hupumzika na kulipua bomu Desemba 25, 2014 na kuwajeruhi polisi watatu.

Mshtakiwa wa tatu anaelezwa kukiri katika maelezo yake kuwa alishiriki mikutano ya kuanzisha vikundi vya jihad kutekeleza vitendo vya kigaidi ili kuanzisha Dola la Kiislamu (Islamic State) katika mji wa Songea mkoani Ruvuma.

Katika maelezo hayo, alikiri kuwashambulia polisi wakiwa doria ili kuwapoka silaha, kutengeneza mabomu na kulipua bomu Septemba 16, 2014 huko Mabatini na kutega bomu eneo la Mshangamo.

“Kwa kuzingatia maelezo hayo ya kukiri kosa, nawaona mshitakiwa wa kwanza (Msabila), wa pili (Yusuph) na wa tatu (Mussa) wana hatia ya makosa waliyoshitakiwa nayo. Mshitakiwa wa nne na watano wanaachiwa,” alisema Jaji na kuongeza:

“Kwa hiyo nawahukumu kama ifuatavyo. Kwamba katika shtaka la kwanza na la tatu watatumikia kifungo cha miaka 15 jela. Kwa shtaka namba 11, 12, 13 na 14 kila mmoja atatumikia miaka 15 na vifungo vyote vitatumikiwa kwa pamoja.”