Sita kortini wakidaiwa kuvunja duka, kuiba mali za Sh31 milioni


Watu sita akiwemo Katibu wa Chama cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania, Wilaya Temeke, Michael Kateka na wenzake wakiwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuvunja duka na kuiba vitu mbalimbali vyenye thamani ya zaidi ya Sh 31milioni.

Muktasari:


  • Katibu wa Chama cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania na watu wengine watano wamefikishwa mahakamani Temeke kwa kuvunja duka na kuiba mali yenye thamani ya zaidi ya Sh 31 milioni.

Dar es Salaam. Watu sita akiwemo Katibu wa Chama cha Wamiliki Ardhi na Nyumba Tanzania, Wilaya ya Temeke, Michael Kateka (68) wamefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke wakikabiliwa na mashtaka mawili likiwemo la kuvunja duka na kuiba vitu vyenye thamani ya zaidi ya Sh 31 milioni.

 Mbali na  Kateka, wengine ni Bilali Juma (32), mkazi wa Mtoni, Isiaka Kapemba (32), Hemed Kapemba(32),  Fadhili Kapemba na mjumbe wa shina, Hassan Kitigi, wote wakazi wa Magurumbasi.


Akisoma hati ya mashtaka, Wakili wa Serikali, Nicas Kihemba alidai kati ya Novemba 2, 2022 maeneo ya Keko Makurumbasi, washtakiwa walivunja  na kuingia kwenye duka la Isack Mtenga.

Pia anadaiwa siku hiyo waliiba vitu mbalimbali vya dukani ikiwemo tairi saba za gari, vioo vya gari vya scania, dawa za ng'ombe, nyaraka mbalimbali pamoja na spana moja ambavyo vina  jumla ya  thamani  zaidi ya Sh31 milioni.

Washtakiwa walikana tuhuma hizo mbele ya mbele ya Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Ally Mkama.

Wakili Kihemba alida kuwa upelelezi umekamilka, hivyo kuiomba Mahakama ipange tarehe ya kuwasomea maelezo ya awali.

Washtakiwa wamepelekwa rumande baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana ambayo ni kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua zinazotambulika, mmoja atoe fedha taslimu Sh5 milioni au hati ya mali isiyohamishika yenye thamani hiyo. Kesi itatajwa Machi 27, 2024.