Skauti waomba kurudishwa katika bajeti ya Serikali

Skauti waomba kurudishwa katika bajeti ya Serikali

Muktasari:

  • Chama cha Skauti Tanzania, kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kukirudisha chama hicho katika bajeti ya Serikali ili kiweze kujiendesha.

  

Dar es Salaam. Chama cha Skauti Tanzania, kimemuomba Rais Samia Suluhu Hassan, kukirudisha chama hicho katika bajeti ya Serikali ili kiweze kujiendesha.

Ombi wamelitoa leo Jumamosi Oktoba 2, 2021 na Skauti Mkuu, Mwantumu Mahiza, wakati wa siku ya mlezi wa Skauti Tanzania inayofanyika jijini Dodoma

Mahiza amesema miaka kumi iliyopita chama hicho kilikuwa kikipata bajeti kupitia Wizara ya Elimu lakini waliondolewa na hivyo kujikuta wakijiendesha kwa shida.

“Tunaomba kama itakupendeza Rais, turudishwe katika bajeti ya Wizara ya Elimu au Tamisemi kama ilivyokuwa awali, kwakuwa tunajiendesha kwa tabu kutokana na ukosefu wa fedha” amesema Mahiza.

“Kwa mujibu wa waraka namba nne wa mwaka 2015 kila shule ni kundi la skauti na linapaswa kulipa ada ya Sh12, 000 kwa mwaka. Endapo ada hiyo ingelipwa kwa wakati ingewezesha chama kujiendesha,”amesema Mahiza.

Siku ya mlezi wa Skauti ni siku ambayo chama hicho hupata nafasi ya kukutana na mlezi wao ambaye huwa ni Rais aliyepo madarakani kueleza mafanikio, matarajio na changamoto wanazokabiliana nazo.

Mahiza amesema mara ya mwisho kufanyika sherehe hizo ni miaka 25 iliyopita.