Soko la Kariakoo kukamilika Oktoba

Muktasari:

  • Makalla awahakikishia usalama wa biashara Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, huku akiwataka kuwa na ushirikiano mzuri na wakuu wilaya wapya na kuwaahidi  katika kongamano la Wamachinga Taifa  linalotarajiwa  kufanyika jijini hapa, atahakikisha anamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwa mgeni rasmi wa kongamano hilo.

Dar es Salaam. Katika kuhakikisha wafanyabiashara wadogo wadogo maarufu kama Wamachinga wanafanya biashara zao kwa usalama, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla amewataka wafanyabiashara hao kuwa na ushirikiano na viongozi wao huku akisema Soko la Kariakoo linatarajiwa kukamilika Oktoba mwaka huu.

Makalla amewaahidi kwamba atahakikisha katika kongamano la Wamachinga Taifa litakalofanyika jijini hapa, atamuomba Rais Samia Suluhu Hassan ili aweze kuhudhuria.

"Nitamueleza kulikuwa na kongamano zuri, na wamekuomba ukutane nao kama mgeni rasmi katika kongamano lao la kitaifa litakalofanyika Dar es Salaam, natumaini atakuwa muelewa, " amesema.

Makalla ameyasema hayo leo Machi 11, 2023 akiwa mgeni rasmi katika Kongamano la Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam lililohudhuriwa na Wamachinga zaidi ya 2,000 katika Viwanja vya Sabasaba jijini hapa.
Makalla pia amewahaidi kukamilika kwa ujenzi wa soko la Kariakoo mwezi Oktoba huku wakitajarajia wafanyabiashara 3,500 kufanya biashara zao katika soko hilo.

"Soko la KariaKoo litakamilika mwezi Oktoba na linatarajiwa kuwa na wafanyabiashara 3500, hivyo wafanyabiashara mliohamishiwa kwenda Kisutu, Machinga Complex bado mna nafasi yenu, wengine tutatoa fursa mpate maeneo," amesema.

Makalla ambaye amekuwa mlezi wa Wamachinga amewataka pia wakuu wa Wilaya jijini Dar es Salaam kuhakikisha kuwa wanasikiliza kero na changamoto zinazowakabili wafanyabiashara hao.

"Ninatoa wito kwa kila mkuu wa wilaya katika eneo lake ahakikishe changamoto za miundombinu kama umeme, maji, vyoo katika masoko zinamalizika ili wafanyabiashara waweze kufanya kazi zao kwa usalama pamoja na kusikiliza kero zao mbalimbali," amesema.

Hata hivyo, katika kuhakikisha anaondoa vilio vya Wamachinga wengi jijini hapa. Makalla amewahakikishia wafanyabiashara wote kwamba atahakikisha Latra wanasimamia route zote za magari kufika katika masoko.
Makalla pia alitoa wito kwa Wamachinga kuhakikisha kuwa wanatoa ushirikiano wa kutosha kwa wakuu wapya wa wilaya kama walivyofanya kwa wale waliotangulia.

"Sasa hivi kuna usalama mzuri hii ni kutokana na kuwapanga vizuri, katika biashara zenu na hata kupelekea mapato ya serikali kuongezeka hivyo hakikisheni mnatoa ushirikiano mzuri kwa viongozi wenu," amesema.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jami kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, jinsia Wanawake na Makundi, David Malebeto ambaye alihudhuria kama mwakilishi amesema wao kama wizara wanaendelea na mchakato wa kuhakikisha Wamachinga wote wanapata vitambulisho vya biashara ambavyo vitawasaidia kufanikisha mambo mbalimbali kama kukopa mikopo benki.

"Mwezi Julai kama mfumo utakwenda vizuri tunatarajia kutoa vitambulisho kwa Wamachinga, vitambulisho vya N card," amesema.

Naye Meneja Biashara kutoka N card, Jackson Jacka amesema watahakikisha wanawapatia Wamachinga vitambulisho vya kisasa yani kidigitali ambavyo vitakuwa ni utambulisho katika biashara zao.

"Tumepewa dhamana ya kutengeneza vitambulisho vya kidigitali kwani malipo ya biashara na utunzaji wa taarifa za fedha zitakuwa kwa mfumo wa kidigitali," amesema.

Mwenyekiti wa Wamachinga Mkoa wa Dar es Salaam, Yusuph Namoto alisema watahakikisha wanashirikiana vyema na serikali kupitia mamlaka husika ili kuweza kuleta maendeleo katika jamii.

Nao wadhamini wa Kongamano hilo ambao ni wadau wakuu katika kutoa mikopo kwa Wamachinga, Maendeleo Benki kupitia Mkurugenzi wao Mkuu, Ibrahim Mwangalaba wamesema wao wamefanya kwa vitendo kwa kuwapatia mikopo Wamachinga 2,898 ili kuweza kufanikisha maendeleo katika biashara zao.

"Takribani Sh3.8 bilioni zimetolewa kwa wamachinga na wamekuwa ni wakopaji wazuri kwa kurejesha kwa muda sahihi hivyo benki itaendelea kutoa msaada na elimu kuhusu matumizi sahihi ya mikopo kwa ajili ya biashara," amesema  Mwangalaba.