Soko la Karume laungua tena

Mafundi kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) wakifanya maandalizi kwa ajili ya kubadilisha nguzo iliyoteketezwa kwa moto katika soko hilo la Karume. Picha na ELizabeth Joachim

Muktasari:

Vibanda 36 vimeteketea katika Soko la Karume lililopo Dar es Salaam baada ya moto kuunguza sehemu ya soko hilo.

Dar es Salaam. Vibanda 36 vimeteketea katika Soko la Karume lililopo Dar es Salaam baada ya moto kuunguza sehemu ya soko hilo.

Muto huo umeanza leo Ijumaa Aprili 8, 2022 alfajiri na kuunguza maduka ya wafanyabiashara ndogondogo wanaouza mabegi.

Jumapili Januari 16, 2022 Soko la Karume (soko la mchikichini) liliteketea moto na kuharibu mali mbalimbali ikiwamo miundombinu ya umeme.

Leo alfajiri moto mwingine umeunguza tena eneo ambalo wafanyabiashara ndogondogo wanapouza mabegi ambapo vibanda 36 kati ya 96 vimeteketea.

Kwa mujibu wa naibu Katibu wa wajasimali walemavu mkoa wa Dar es Salaam (UWAWADA) Mohamed Sona amesema moto huo umesababishwa na hitilafu ya umeme.

"Vibanda hivi vinamilikiwa na wafanyabiashara walemavu, ingawa kuna wafanyabiashara zaidi 600 walihamishwa kutoka Kariakoo," amesema Sona.

" Pamoja na jitihada za kikosi cha zimamoto na ukoaji zipo baadhi ya mali zimeteketea hasa maeneo ambayo moto umeleta madhara kwa sehemu.

“Moto umeenza saa 11 alfajiri na vibanda 36 kati ya 96 vimeteketea lakini hakuna madhara kwa binadamu” amesema Sona

Amesema kuwa moto huo ulidhibitiwa na kikosi cha Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Ilala.

Mfanyabiashara, Godfrey Eliya  amesema mali yenye thamani ya 25 milioni zimeteketea yakiwemo mazulia na mapazia.

Mwananchi imefika katika eneo la tukio na kukuta eneo hilo likiwa limewekwa uzio huku mafundi kutoka Shirika la Umeme (Tanesco) wakifanya maandalizi kwa ajili ya kubadilisha nguzo iliyoteketezwa kwa moto katika soko hilo.


Endelea kufuatilia Mwananchi