Soko la tanzanite kuitangaza Tanzania kimataifa-Naibu Spika

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma (kushoto) akizungumza baada ya kutembelea ujenzi wa soko la madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro, katikati ni Mkuu wa mkoa wa Manyara Queen Sendiga. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma amesema soko la madini ya tanzanite linalojengwa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, litaitangaza Tanzania na kuvutia watalii zaidi.

Mirerani. Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma amesema soko la madini ya tanzanite linalojengwa mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, litaitangaza Tanzania na kuvutia watalii zaidi.

Naibu Spika Mgeni ameyasema hay oleo Agosti 5 baada ya kutembelea soko la madini ya tanzanite linalojengwa mji mdogo wa Mirerani, akiwa na Mawaziri watatu na manaibu mawaziri watano na wajumbe wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar.

Amesema ujenzi wa soko hilo utaitangaza zaidi Tanzania kupitia madini ya Tanzanite kwani wale waliokuwa na dhana potofu kuwa madini hayo yanapatikana nje ya Tanzania wataelewa.

"Tumeambiwa Tanzanite ni madini pekee duniani yanayopatikana Tanzania hivyo soko hilo la madini hayo litakapokamilika hapa Mirerani litaongeza sifa ya nchi na zaidi kuitangaza Tanzania kimataifa," amesema Mgeni.

Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga amesema ujenzi wa soko hilo umefikia asilimia 65 ili jengo likamilike na wanatarajia hadi mwezi Oktoba mwaka 2023 litamalizika.

"Tunatarajia jengo la soko la madini kukamilika kwenye kilele cha mbio za mwenge wa uhuru mwaka huu wa 2023 itakuwa hapa Manyara," amesema Sendiga.

Hata hivyo, amemshuku serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa namna inavyofanikisha miradi mingi mikubwa na midogo mkoani Manyara.


Naye Mhandisi wa ujenzi wa soko hilo, Goodluck Masika amesema walianza shughuli za ujenzi Mei 22 mwaka 2022 na wanatarajia kukamilisha mwezi Oktoba mwaka 2023.

Mhandisi Masika amesema mradi wa soko hilo unatekelezwa na shirika la nyumba la Taifa (NHC) kwa thamani ya Sh5.49 bilioni chini ya mshauri chuo cha ufundi Arusha.

Ofisa madini mkazi (RMO) Mirerani, mhandisi Menard Msengi amesema kukamilika kwa soko hilo kutaongeza tija kwenye mnyororo wa thamani ya madini ya Tanzanite.