Viongozi Zanzibar watembelea madini ya Tanzanite

Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Onesmo Mbise (kushoto) alipotembelea mgodi wa madini ya Tanzanite Kitalu C, Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro, wa pili kulia ni Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, amewaongoza wajumbe 163 wa Baraza la Wawakilishi, mawaziri watatu na manaibu mawaziri watano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutembelea migodi ya madini ya Tanzanite Mirerani.

Mirerani. Naibu Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mgeni Hassan Juma, amewaongoza wajumbe 163 wa Baraza la Wawakilishi, mawaziri watatu na manaibu mawaziri watano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kutembelea migodi ya madini ya Tanzanite Mirerani.

Naibu Spika Mgeni, akiwa na Mkuu wa mkoa wa Manyara, Queen Sendiga ameongoza msafara huo leo Agosti 4 na kutembelea mgodi wa Kitalu C wa kampuni ya Franone Mining and Gems LTD uliopo mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro.

Akizungumza baada ya kutembelea eneo hilo ameipongeza Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD kwa kutoa ajira 328 wakiwemo wanawake.

Amesema wamejifunza mengi ikiwemo uchimbaji wa madini ya Tanzanite unavyofanyika na kuona ukuta unaozunguka migodi ya madini hayo uliojengwa kipindi cha uongozi wa hayati John Magufuli.

"Kule Zanzibar tunazungumzia uchumi wa bluu kupitia bahari, tumekuja kujifunza namna uchumi wa migodi unavyonufaisha Watanzania," amesema Spika Mgeni.

Ofisa madini mkazi (RMO) Mirerani, mhandisi Menard Msengi, amesema eneo hilo la machimbo ya madini ya Tanzanite limetengwa kwenye vitalu vinne.

"Eneo la kitalu B na D wanachimba wachimbaji wadogo na eneo la kitalu C hapa tulipo wanachimba wawekezaji Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD," amesema mhandisi Msengi.

Mkurugenzi wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Onesmo Mbise amewakaribisha wageni hao na kusema kuwa wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuwaamini wawekezaji wazawa hadi kuwakabidhi kitalu C.

"Nikiwa na wenzangu Francis Matunda na mtaalamu wetu Vitus Ndakize, tunafanya kazi ipasavyo huku tukishirikiana na Serikali," amesema Mbise.

Meneja wa Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, Vitus amesema pamoja na kutoa ajira rasmi 328 pia wametoa ajira zisizo rasmi 1,000.