Tanzanite kufanyiwa mnada ili kuyaongezea thamani

Waziri wa Madini Dotto Biteko (katikati) akizungumza baada ya kutembelea machimbo ya madini ya Tanzanite mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara eneo la kitalu C kinachomilikiwa na Kampuni ya Franone Mining and Gems LTD, kulia ni Mkurugenzi wa kampuni hiyo Onesmo Mbise. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

  • Ili kuyaongezea thamani madini ya Tanzanite, Serikali imejipanga kufanya mnada wa kitaifa na kimataifa.

Mirerani. Waziri wa Madini, Dotto Biteko amesema wanaandaa mnada wa madini ya tanzanite yanayochimbwa mji mdogo wa Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara, ili kuyaongezea thamani madini hayo.

 Biteko ameyasema hayo leo Julai 8 baada ya kufanya ziara ya siku moja mji mdogo wa Mirerani, kuzungumza na wadau wa madini, kutembelea kitalu C kinachomilikiwa na kampuni ya Franone Mining LTD na jengo la soko la madini ya Tanzanite.

Amesema madini ya kito ya Tanzanite, yanapaswa kufanyiwa mnada kwa lengo la kuyaongezea thamani kimataifa hivyo wataanzisha mnada wa kwanza baada ya jengo la soko la madini kukamilika Mirerani.

"Tunahitaji kufanya maonyesho ya mnada wa madini hayo ili jiwe la tanzanite liweze kuwa na thamani zaidi kwani hata mtu mwenye binti mzuri aliyepo ndani tuu asiyeonekana hawezi kuolewa," amesema Biteko.

Hata hivyo, amesema agizo la Serikali la madini ya tanzanite kuchakatwa na biashara yake kufanyiwa Mirerani pekee litaendelea kutekelezwa na jengo la soko la madini hayo linaendelea kujengwa.

"Hao wanaodhani kuwa biashara ya madini ya tanzanite itahama Mirerani na kwenda eneo lingine wanajidanganya kwani hilo halitafanyika na jengo linaendelea kujengwa," amesema Biteko.

Pia, ameipongeza kampuni ya Franone Mining and Gems LTD inayochimba madini ya Tanzanite kitalu C kwa namna wanavyofanya shughuli zao za uchimbaji kwa umakini.


Kwa upande wake Mkuu wa wilaya ya Simanjiro, Dk Suleiman Serera, akimkaribisha Waziri Biteko mji mdogo wa Mirerani, amempongeza kwa namna anavyoongoza sekta hiyo.

Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka amemshuku Waziri Biteko kwa kufanikisha upekuzi wa staha kwani hivi sasa watu hawavuliwi nguo.

Mkurugenzi wa kampuni inayomiliki kitalu C ya Franone Mining Gem's LTD, Onesmo Mbise amewaahidi watu wengi uhitaji maalum na wanawake wachekechaji kuwaongezea udongo wa kuchekecha pindi ukiongezeka.