Somalia mwananchama mpya EAC

Muktasari:

  • Viongozi wa EAC waliokutana jijini Arusha nchini Tanzania kwa ajili ya mkutano wao wa 23 wa mwaka, wameamua kukubali maombi ya nchi ya Somalia kuwa sehemu ya jumuiya hiyo. Hata hivyo, Somalia ilitamani kujiunga tangu mwaka 2012.

Arusha. Sasa ni rasmi, Somalia ni mwanachama mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hivyo kuifanya jumuiya hiyo kuwa na nchi wananchama nane huku duru za kisiasa zikijiuliza kuhusiana na hali ya amani katika taifa hilo.

Viongozi wa EAC waliokutana jijini Arusha, Tanzania kwa ajili ya mkutano wao wa 23 wa mwaka, wameamua kukubali maombi ya nchi hiyo kuwa sehemu ya jumuiya hiyo, hata hivyo, Somalia ilitamani kujiunga tangu 2012, japo mazungumzo madhubuti yamefanyika mapema mwanzoni mwa mwaka huu.

Hata hivyo, kukubaliwa kwa Somalia katika jumuiya hiyo kumeonekana kutowashanga wengi, japo pia siyo wachambuzi wengi waliochukua kwa uzito matamshi yaliyotolewa siku chache zilizopita na Katibu Mkuu wa EAC, Peter Mathuki pale aliposema upo uwezekano Somalia kujiunga na EAC.

Tangazo la maombi ya Somalia kukubaliwa ndani ya jumuiya, lilitolewa na Mwenyekiti wa EAC anayemaliza muda wake ambaye pia ni Rais wa Burundi, Evariste Ndayishimiye kabla ya kuondoka kwenye kiti hicho, leo Ijumaa, Novemba 24, 2023.

"Somalia sasa ni mwanachama mpya wa EAC. Viongozi walifanya uamuzi huo wakati wa majadiliano yaliyofanyika faragha," amesema

Kukubalika kwake kwa mara nyingine kunaharakisha upanuzi wa EAC ambayo hadi 2007 ilikuwa na wanachama waanzilishi watatu; Tanzania, Uganda na Kenya.

Hii inaifanya EAC kuwa na mataifa nane ikienea sio tu kutoka Bahari ya Hindi hadi Atlantiki lakini pia hadi Pembe ya Afrika huku Katibu Mtendaji wa jumuiya hiyo Dk Mathuki akipongezwa kwani katika miaka yake miwili ya uongozi, ameweza kuandikishwa wanachama wawili wapya.

Wanachama hapo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ambayo ni nchi kubwa katikati mwa Afrika, ilijiunga na umoja huo Machi 2023 na Somalia leo Ijumaa.

Inaelezwa Dk Mathuki mara nyingi amekuwa akitetea ombi la Somalia, akisema nchi hiyo ina uhusiano mkubwa wa kibiashara, kiuchumi, kihistoria na kijamii na kiutamaduni katika ukanda huo wa Afrika Mashariki.

Hivyo kukubalika kwake katika kambi hiyo kunaweza kukuza biashara ya ndani ya kanda kutokana na rasilimali zake hasa za uvuvi.

Kwa mantiki hiyo, EAC ya miongo miwili sasa ina jumla ya nchi nane wanachama ambazo ni Tanzania, Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda, Sudan Kusini, DR Congo na Somalia.

Kwa upande wa idadi ya watu na nguvu za kiuchumi, EAC sasa inafuata jumuiya ya Comesa, pamoja na ile ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc), Maghreb na Ecowas.

Hata hivyo, Dk Mathuki, mara kadhaa amenukuliwa akisema kuwa nchi nyingine pia zimeonyesha nia ya kujiunga na EAC, zikiwemo Ethiopia na Comoro.

Marais wa nchi ya Afrika Mashariki, katika mkutano wa leo, walimkaribisha mwanachama huyo mpya, wakisema kukubaliwa kwake, kunatokana na moyo wa mtangamano.

Mwenyeji wa marais hao, Rais Samia Suluhu Hassan alimpongeza Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia kwa kujiunga na viongozi hao.

Katika hotuba yake, Rais Mohamud amesema nchi yake itafanya kila liwezekanalo, kuhakikisha inafanya kazi kwa amani na mataifa mengine ya EAC.

Alikiri kuwepo kwa changamoto ambazo taifa lake linalokumbwa na migogoro kwa miaka mingi, hata hivyo, anaamini siku moja machafuko hayo yatakwisha.

Kwa upande wake, Rais William Ruto wa Kenya amesema anaamini kuingia kwa Somalia katika EAC kutakuja na manufaa makubwa kiuchumi.

"Kukubaliwa kwao kutaimarisha kambi yetu hasa biashara za kikanda", amesema Ruto ambaye nchi yake imekuwa katika nyakati tofauti ikikumbwa na mashambulizi kutoka kwa kundi la kigaidi la al Shabaab lenye makao yake Somalia.

Rais Paul Kagame wa Rwanda na Felix Tshisekedi wa DR Congo hawakuhudhuria mkutano huo lakini waliwakilishwa katika mktano huo na viongozi wa juu wa mataifa hayo.

Waziri Mkuu wa Rwanda, Eduardo Ngerente alimwakilisha kiongozi wa Rwanda huku mwanasiasa machachari wa DRC, Jean Pierre Bemba alimwakilisha Rais Tshisekedi.

Bemba alivuta hisia za mamia ya wajumbe pale alipogusia ghasia nchini kwake akisema “ghasia hizo tayari zimewafanya zaidi ya watu milioni mbili kuwa wakimbizi wa ndani katika eneo lake la mashariki, hasa katika Kivu Kaskazini.”

Rais Yoweri Museveni wa Uganda ametoa changamoto kwa viongozi wa EAC kuelekeza nguvu zao katika uzalishaji mali na ustawi.