Songwe kurejesha maonesho ya kimondo

Mwezeshaji katika warsha ya wadau wa utalii, Joyce Mgaya wakati akiwasilisha mada ya utalii mbele ya wanahabari.
Muktasari:
- Mkoa wa Songwe umerejesha maonesho ya siku ya kimondo ili kuwakutanisha wadau mbalimbali sambamba na siku ya vimondo Duniani yanayofanyika kila ifikapo Juni 30 kila mwaka.
Songwe. Mkoa wa Songwe umerejesha maonesho ya siku ya kimondo ili kuwakutanisha wadau mbalimbali sambamba na siku ya vimondo Duniani yanayofanyika kila ifikapo Juni 30 kila mwaka.
Karibu Tawala mkoani hapa Misaille Musa amewaambia waandishi wa habari wanaohudhuria kikao Cha wadau wa utalii kuwa mkoa umechukua hatua hiyo ikiwa ni moja ya njia ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani hapa.
Amesema maonesho ya kimondo yalikuwa yakifanyika miaka ya nyuma lakini kufuatia mlipuko wa ugonjwa wa Uviko 19 yalisitishwa Ili kupisha mikusanyiko ya watu.
Musa ameongeza kuwa katika za kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan za kutangaza utalii kupitia filamu ya Royal Tour, mkoa unaandaa filamu ya makala maalumu itakayoelezea vivutio vya utalii vilivyopo Mkoani hapa.
Awali Mshauri wa Maliasili, Mazingira na Utalii Zakayo Mwaitosya amesema mkoa wa Songwe umebahatika kuwa na vivutio vingi vya utalii ambavyo bado havijulikani ikiwa ni pamoja na Kimondo Cha Mbozi, Maporoko ya maji, makanisa ya kale, na mlima wa machimbo ya dhahabu unaojulikana kwa jina la Quen Elizabeth na vingine vingi ambavyo bado havijulikani.
Vivutio vingine ni Mapango ya Popo, maji moto, misitu, Mlima ng'amba uliopo Mbozi ambao Kwa Sasa unatumika Kwa ibada na matambiko.
Mmoja wa waandishi wa habari Haika Rayman amesema amekuwa akisikia uhifadhi wa Ngorongoro kuhusiana na Utalii wa wanyama pamoja na binadamu waishio katika hifadhi hiyo kama wahadzabe,wadatoga na wamaasai hivyo kupitia ujio wa mamlaka ya Ngorongoro Mkoani Songwe inaenda kuleta fursa Kwa wanahabari katika kutangaza vivutio vilivyopo Mkoani hapa hasa kimondo ambacho kimekuwa ni nembo ya mkoa wa Songwe.